Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku 5 za machungu kwa wakazi wa Lume, DRC: Watu 20 wauawa

Walnda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wako chonjo kuhakikisha kuna usalama na hapa ni Djugu jimboni Ituru ambako walifika kuweka doria baada ya ripoti za kuweko kwa kikundi cha CODECO ambacho hushambulia raia.
MONUSCO/Force
Walnda amani wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini DRC, MONUSCO wako chonjo kuhakikisha kuna usalama na hapa ni Djugu jimboni Ituru ambako walifika kuweka doria baada ya ripoti za kuweko kwa kikundi cha CODECO ambacho hushambulia raia.

Siku 5 za machungu kwa wakazi wa Lume, DRC: Watu 20 wauawa

Amani na Usalama

Kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO umeripoti kuwa watu wapatao 20 wakiwemo watoto wawili wameuawa wakati wa mashambulizi yaliyofanywa na wafuasi wanaodaiwa kuwa wa kikundi kilichojihami cha Allied Democrait Forces, au ADF katika siku tano zilizopita huko eneo la Lume, jimboni Kivu Kaskazini.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amewaambia waandishi wa habari mjini New York, Marekani hii leo kuwa mauaji hayo yametokea baada ya watu hao waliojihami kushambulia kituo cha afya cha Lume na vijiji kadhaa jimboni Kivu Kaskazini.

“Watu hao pia waliteka idadi kubwa ya raia wakiwemo watoto 3, huku wakiteketeza kwa moto mamia ya nyumba za wakazi wa eneo hilo,” amesema Bwana Dujarric.

Kufuatia kitendo hicho, MONUSCO ilituma kikosi chake cha kuchukua hatua haraka, QRF ili kuimarisha ulinzi na kusaidia wale walioathirika kwenye mashambulio hayo.

Jimboni Ituri nako mashambulizi

Bwana Dujarric amesema katika hatua nyingine, huko eneo la Busiyo, takribani kilometa 72 kusini-magharibi mwa Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri, walinda amani wa Umoja wa Mataifa walikabiliana na washambuliaji ambao hatimaye walilazimika kukimbia katika kijji walichokuwa wamevamia.

“Na tukirejea Kivu Kaskazini, usiku walinda amani walipelekwa kuchukua hatua za haraka huko Matonge baada ya watu wanaoshukiwa kuwa kikosi cha ADF kupambana na askari wa jeshi la DRC, FARDC,” amesema Bwana Dujarric.

Hata hivyo amesema ujumbe huo unaendelea kuweko kweneye eneo hilo na kuhakikisha hatua za Umoja wa Mataifa za kudhibiti mashambulizi zinakuwa za kina sambamba na kusaidia juhudi za mashariki za tathmini ya usaidizi.

Ameongeza kuwa juhudi zinaendelea kuimarisha mifumo ya kijamii ya kutoa taarifa mapema ili waweze kubaini vitisho vya usalama na hivyo kuweza kuchukua hatua haraka sambamba na kuweka uwezo wa taifa hilo kuchunguza mashambulizi hayo na wahusika wawajibishwe.