Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Benki ya dunia yatoa msaada wa dola milioni 100 kwa WFP nchini Sudan

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linasambaza biskuti zenye nishati nyingi kwa zaidi ya wakimbizi 900 wa Ethiopia walioko Sudan baada ya kukimbia vita katika kijiji cha Basunga.
© WFP
Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linasambaza biskuti zenye nishati nyingi kwa zaidi ya wakimbizi 900 wa Ethiopia walioko Sudan baada ya kukimbia vita katika kijiji cha Basunga.

Benki ya dunia yatoa msaada wa dola milioni 100 kwa WFP nchini Sudan

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP nchini Sudan limetangaza kupokea mchango wa dola milioni 100 kutoka Benki ya Dunia kwa ajili ya kutekeleza program yake ya dharura ya kusaidia nchi hiyo.

Taarifa ya WFP kutoka Khartoum imemnukuu Mkurugenzi na mwakilishi wa WFP nchini humo Eddie Rowe akishukuru kwa mchango huo kwa mara ya kwanza kutoka Benki ya dunia kuja kwa shirika lake nchini humo. 

“WFP inashukuru sana Benki ya Dunia kwa mchango huu wa ukarimu ambao umekuja kwa wakati muhimu nchini Sudan ambapo wananchi wengi hawajui mlo wao wa kesho utatoka wapi.”

Rowe amesema kwa msaada huo wataweza kutoa fedha taslimu za chakula kwa zaidi ya watu milioni mbili nchini kote wakiwemo wakimbizi wa ndani na wakazi wa maeneo husika.

Fedha hizo zilizotolewa na Benki ya dunia zimetolewa na Mfuko wa dhamana wa Msaada wa mpito na urejeshaji wa Sudan (STARS) ambao unasimamiwa na Benki ya Dunia lakini wafadhili wake ni Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Uswisi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uholanzi, Canada, Hispania, Finland, Ireland pamoja na fedha za Benki ya dunia katika hazina ya kujenga amani.

“Tunatoa shukran zetu za dhati kwa wafadhili wote ambao wamewekeza katika mfuko wa STARS. Ufadhili huu utasaidia kupunguza janga la njaa linalokuja nchini Sudan na kusaidia mifumo ya usalama ya kijamii kwa siku zijazo kwa walio hatarini zaidi nchini humo ambayo sio tu yatasaidia kuokoa Maisha bali pia kubadili Maisha” alisema mwakilishi huyo wa WFP nchini Sudan 

Lishe maalum inayotolewa na WFP imeboresha hatua kwa hatua utapiamlo mkubwa nchini Sudan, na familia pia zimepokea chakula kama vile unga, maharagwe makavu, mafuta na chumvi.
© WFP/Mohammed Awadh
Lishe maalum inayotolewa na WFP imeboresha hatua kwa hatua utapiamlo mkubwa nchini Sudan, na familia pia zimepokea chakula kama vile unga, maharagwe makavu, mafuta na chumvi.

Hali ilivyo sasa nchini Sudan

Taarifa ya WFP kutoka Sudan inaeleaza njaa inaendelea kuongezeka kwa kasi ya kutisha na kila mchango unaotolewa utasaidia WFP kuweza kuwasaidia watu walio hatarini zaidi nchini humi.

“Hivi sasa, theluthi moja ya watu wa Sudan wanakabiliwa na uhaba wa chakula. Kufikia Septemba, hadi watu milioni 18, sawa na asilimia 40 ya idadi ya watu nchini humu wanaweza kutumbukia kwenye njaa, kulingana na Tathmini Kabambe ya Usalama wa Chakula na Mazingira Hatarishi iliyotolewa mwezi Juni.” Ameeleza Rowe.

Miongoni mwa vitu vinavyo chochea uhaba wa chakula nchini Sudan ni mzozo wa kiuchumi na kisiasa, mfumuko wa bei, migogoro na watu kuyahama makazi yao, majanga yatokanayo na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni pamoja na ukame na mafuriko, na mavuno duni katika msimu wa kilimo uliopita. 

Watoto wa Sudan katika mpango wa kulisha shuleni
WFP
Watoto wa Sudan katika mpango wa kulisha shuleni

Mradi utafanya nini?

Kazi ya WFP nchini Sudan inalenga kuokoa maisha ya watu wanaokabiliwa na njaa huku ikishughulikia sababu kuu za uhaba wa chakula.

Mradi huu mpya uliozinduliwa utaiwezesha WFP kuokoa maisha huku ikiweka msingi wa mfumo wa usalama wa kijamii unaolengwa zaidi nchini Sudan, kushughulikia sababu kuu za ukosefu wa chakula kwa kusaidia walio hatarini zaidi kuhimili mishtuko na kujenga maisha zaidi ya kudumu kwa muda mrefu.

Licha ya mchango huu kutoka kwa Benki ya Dunia na wafadhili wa STARS, WFP imesema bado inahitaji angalau dola milioni 266 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa 2022 ili wawewze kufikia zaidi ya watu milioni 10 walio hatarini kama ilivyopangwa mwanzoni mwa mwaka. 

Tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2022, WFP imefikia watu milioni 4.8 kote Sudan kwa kuwapatia chakula cha kuokoa maisha au pesa taslimu na lishe, milo ya shule na fursa za kujikimu.