Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen njaa na magonjwa vinakatili maisha ya watu wengi kuliko vita:UNDP

Uharibifu uliosababishwa na mzozo wa muda mrefu nchini Yemen.
UNDP Yemen
Uharibifu uliosababishwa na mzozo wa muda mrefu nchini Yemen.

Yemen njaa na magonjwa vinakatili maisha ya watu wengi kuliko vita:UNDP

Amani na Usalama

Vifo vingi nchini Yemen vinatokea kutokana na athari za mzozo kwa bei ya vyakula na kuzorota kwa hali ya usafi.  

Ripoti ya shirika la Umoja wa Mataifa la mango wa maendeleo duniani UNDP imeonya leo kwamba zaidi ya watu milioni moja wanaweza kufa iwapo vita vitaendelea hadi mwaka 2030.  

Limeongeza kuwa ikiwa vita vitaweza kusitishwa na kuwekezwa katika maendeleo, basi inawezekana kutokomeza umaskini uliokithiri.

Takriban asilimia 60 ya waaathirika 377,000 wa mzozo wa Yemen hadi sasa hawajapoteza maisha kutokana na mabomu au risasi, bali kutokana na athari za kijamii za mgogoro huo, kama vile njaa na magonjwa yanayoweza kuzuilika.  

Ripoti hiyo ya UNDP imesema idadi hiyo inaweza kufikia asilimia 75% ikiwa mzozo huo utaendelea hadi 2030, wakati inakadiriwa kuwa watu milioni 1.3 wanaweza kufa.

Idadi kubwa ya vifo hivi vimekuwa vya watoto, ambao wako hatarini zaidi kwa utapiamlo.

Mwaka huu wa 2021, raia mmoja wa Yemeni aliye chini ya umri wa miaka mitano hufa kila dakika tis ana ifikapo mwaka 2030, mtotommoja nchini humo atakufa kila dakika tano.

Tusipime gharama ya vita kwa vifo vya mapigano

Mkuu wa UNDP Achim Steiner amesema "Huu ni moja ya ujumbe muhimu wa ripoti. Mara nyingi tunapima gharama ya vita kwa waathirika wa mapigano, lakini kwa upande wa Yemen idadi ya watu waliokufa kutokana na matokeo ya mzozo huo inazidi wale waliokufa kwenye uwanja wa vita".

Ripoti hiyo "inatoa mwanga juu ya athari za mgogoro katika maendeleo na ustawi wa jamii. Mgogoro huo tayari umesukuma watu milioni 4.9 kwenye utapiamlo, na idadi hii itapanda hadi milioni 9.2 ifikapo 2030 ikiwa vita vitaendelea.”

Utafiti huo unatabiri kuwa, ifikapo mwisho wa mwaka 2021, Wayemeni milioni 15.6 wataishi katika umaskini uliokithiri, na idadi hiyo itaongezeka hadi milioni 22.2 mwaka 2030, saw ana asilimia 65% ya watu wote.
Kwa mujibu wa UNDP ripoti katika kipindi cha miaka sita iliyopita, mgogoro huo unakadiriwa kusababisha Yemen kupoteza dola bilioni 126 za ukuaji wa uchumi unaowezekana.

Imeonya kwamba ikiwa vita itaendelea, hadi mwaka 2030 Pato la Taifa la Yemen lililopotea linaweza kuwa karibu dola milioni 422,000, yaani sawa na dola milioni 28,100 kwa mwaka.

Mwanamke aliyekimbia makazi yake na watoto wake wakiwa katika makazi ya muda kwenye pwani ya magharibi ya Yemen.
IOM/Rami Ibrahim
Mwanamke aliyekimbia makazi yake na watoto wake wakiwa katika makazi ya muda kwenye pwani ya magharibi ya Yemen.

Matumaini kwa Yemen

Hati hiyo ripoti inatuma ujumbe wa matumaini kwamba yote hayajapotea nchini Yemen na pia inaweka wazi kuwa hakuna muda wa kupoteza huku nchi ikiendelea kuzorota.
"Kumaliza mzozo ndiyo njia pekee inayoweza kumaliza gharama hizi za juu kwa watu walio katika hatari zaidi ya Yemen," amesema Jonathan Moyer, mtafiti katika chuo kikuu cha Denver, na mwandishi mkuu wa uchambuzi na ripoti hii.

Ripoti hiyo inabainisha faida zinazowezekana za amani. Kupitia mifano ya kitakwimu inayochambua hali za siku zijazo, inaonyesha kuwa kupatikana kwa amani ifikapo Januari 2022, pamoja na mchakato wa uokoaji wa pamoja na wa jumla, kunaweza kuiona Yemen ikiruka hadi hadhi ya nchi ya kipato cha kati ifikapo 2050.

Wakati huohuo imesema umaskini, ambao sasa unaathiri watu milioni 15.6, utaweza kutokomezwa, utapiamlo unaweza kupunguzwa kwa nusu ifikapo mwaka 2025, na nchi inaweza kufikia ukuaji wa uchumi wa dola bilioni 450 ifikapo mwaka 2050 katika mazingira jumuishi ya amani na kupona.

"Wanawake ni muhimu kwa ajili ya kujikwamua kwa ufanisi," imesema ripoti na kuwataka wajumuishwe katika mazungumzo ya amani, katika mipango ya kiuchumi na katika juhudi za ujenzi upya."

Kushughulikia kukosekana kwa usawa wa kijinsia na kuongeza kiwango cha ushiriki wa nguvu kazi ya wanawake  kwa sasa asilimia 6%, moja ya nchi za chini zaidi duniani ina uwezo wa kufungua mafanikio makubwa ya kiuchumi.

"Watu wanahitaji msaada, lakini pia matumaini ya siku zijazo, hivyo ripoti inachunguza fursa kwa Yemen katika siku zijazo," alisema mkurugenzi wa kanda wa UNDP Khalida Bouzar.

Mzozo nchini Yemen umewalazimu mamilioni ya watu kuyahama makazi yao kwenda kuishi kwenye kambi za muda.
© UNICEF/Hisham Al-Helali
Mzozo nchini Yemen umewalazimu mamilioni ya watu kuyahama makazi yao kwenda kuishi kwenye kambi za muda.

Mapendekezo ya ripoti

Ripoti imetoa mapendekezo saba katika suala hili:
1. Kutoa kipaumbele kwa amani endelevu na ya kudumu. Ili kuweka misingi ya amani ya kudumu, makubaliano mapya lazima yajumuishe katika mazungumzo yake na masharti yake. Na mara tu mzozo huo utakapomalizika, sera za uokoaji lazima zilete maendeleo makubwa katika maisha ya Wayemen.
2. Kuratibu juhudi za kimataifa, kitaifa na uokoaji.
3. Kuwekeza katika afya, elimu, maji na usafi wa mazingira kwa maendeleo endelevu ya muda mrefu.
4. Kuhimiza na kuunga mkono ushiriki mkubwa wa wanawake katika kazi na katika jamii.
5. Kushughulikia njaa kali na kuendeleza kilimo salama na endelevu zaidi.
6. Kutumia fursa ya sekta binafsi kuzalisha ukuaji wa ajira na ufadhili.
7. Kufuata mbinu jumuishi za kujikwamua baada ya mzozo.
TAGS: Yemen, njaa, vita, magonjwa, UNDP , ripoti