Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuzama majini ni sababu kuu ya vifo vitokanavyo na ajali:WHO

Mtoto akiogelea huko Myanmar
© Ocean Image Bank/Ben Jones
Mtoto akiogelea huko Myanmar

Kuzama majini ni sababu kuu ya vifo vitokanavyo na ajali:WHO

Afya

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kuzuia kuzama majini duniani Shirika la Umoja wa Afya duniani WHO limetoa wito kwa watu wote duniani kuongeza juhudi za kupunguza vifo vitokanavyo na watu kuzama kwenye maji, huku likitoa mapendekezo sita ya kusaidia kupunguza vifo na ajali zinazosababishwa na watu kuzama majini duniani kote. 

“Fanya jambo moja kuzuia kuzama” ndio kauli mbiu ya mwaka huu ya Siku ya Kimataifa ya kuzuia kuzama ikiwa ni moja ya sababu kuu ya vifo ulimwenguni kwa watoto na vijana wenye umri wa kati ya mwaka 1 mpaka miaka 24 na vilevile ni sababu ya tatu ya vifo vinavyohusiana na majeraha kwa ujumla.

Taarifa iliyotolewa na WHO kutoka Geneva Uswisi imeeleza kuzama kunasababisha vifo vya zaidi ya watu 236,000 kila mwaka na asilimia 90 ya vifo hivyo vikitokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati huku watoto walio chini ya umria wa miaka mitano wakiwa katika hatari kubwa zaidi.

Sababu za watu kuzama majini

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus sababu kubwa vya vifo hivi ni watu kwenda kuteka maji kwa ajili ya matumizi ya kawaida nyumbani, watu kwenda kuogelea, watu kusafiri kwa njia ya maji kwakutumia boti na meli pamoja uvuvi bila kusahau athari za hali mbaya ya hewa ikiwa ni pamoja na mafuriko.

Dkt Tedros ameeleza kuwa “Vifo hivi vinaweza kuzuilika kupitia kutafuta suluhu za msingi zenye ushahidi n aza gharama ya chini. Leo miji na majiji mengi ulimwenguni yatawasha taa yenye mwanga wa rangi ya bluu kuandishiria wito wa kuchukua hatua za kuzuia na kukomesha watu kuzama.”

Ubia na Bloomberg na wadau wengine

WHO imesema katika kuzuia vifo vitokanavyo na kuzama wameungana na shirika la Bloomberg pamoja na washirika wengine katika kuhamasisha kutelekeza suluhu zitakazozuia watu kuzama na wametangaza mapendekezo sita ambayo ni  kuweka vizuizi vya kudhibiti upatikanaji wa maji, kutoa mafunzo ya kuogelea kwa wanaotazama waogeleaji, kufundisha watoto walio katika shule za msingi kuogelea na usalama wa maji, kutoa huduma ya usimamizi mahala ambapo watoto wanaogelea, kuweka kanuni salama kwenye maboti, meli na feri , kuboresha udhibiti wa hatari za mafuriko.

Lengo la Kaulimbiu

Kauli mbiu ya mwaka huu ya mwaka huu ni “Fanya  jambo moja “ili kuzuia kuzama imelenga kila mwana jamii kwa kuweka katika makundi matatu, lakwanza ni mtu binafsi kujilinda usizame kwa kujifunza kuogelea na kushauri wanafamilia kufanya hivyo, pili kikundi cha watu kufanya kampeni za kutoa elimu ya kujilinda usizame na tatu ni serikali za kila nchi kuweka será za kuzuia kuzama na kuweka ahadi za kusaidia programu za kuzuia kuzama.