Watu 236,000 hupoteza maisha kila mwaka duniani kwa kuzama, bara Ulaya likiongoza:WHO
Watu 236,000 hupoteza maisha kila mwaka duniani kwa kuzama, bara Ulaya likiongoza:WHO
Kuelekea siku ya kuzuia watu kuzama duniani, itakayoadhimishwa hapo kesho Julai 25, shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO kanda ya Ulaya, limesema takriban watu 236,000 hupoteza maisha kila mwaka duniani kote kwa kuzama huku 20,000 kati yao barani Ulaya , vifo ambavyo vinaweza kuzuilika.
Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Copenhagen mkurugenzi wa WHO Kanda ya ulaya, Dkt. Hans Henri P. Kluge amesema “Wengi wetu mara chache, kama itawahi kutokea, hufikiri juu ya kuzama kama hatari ya afya ya umma yenye athari kubwa. Lakini hivi karibuni kupinduka kwa meli ya Adriana kwenye maji kati ya Ugiriki na Italia, meli ndogo ya wavuvi iliyojaa mamia ya watu wanaotafuta maisha mapya Ulaya, kumebadilisha hilo. Katika janga hilo moja zaidi ya watu 600 waliokuwemo katika hali ya kukata tamaa walizama Pamoja na maiti nyingi hazitapatikana tena.”
Lakini amesema ni kawaida zaidi, wanaume, wanawake na watoto kuzama kimya kimya na peke yao katika hali nyingi.
Sababu zinazochangia kuzama
Kwa mujibu wa WHO kuruka bila usimamizi ndani ya mabwawa ya kuogelea ya nyuma ya nyumba yasiyo na uzio, kwa mfano huchangia vifo vya kuzama, au kubebwa na mkondo wa maji ufukweni ambapo ujuzi wa kuogelea pekee hauwezi kuwakomboa watu katika hilo.
Pia shirika hilo limesema kuteleza kwemye meli au michezo ya kwenye maji bila kuvaa majaketi ya kuokoa maisha na kuanguka ndani ya maji wakati unatembea nyumbani peke yako ni baadhi tu ya sababu lakini kuna sababu nyingi zinazochangia watu kupoteza Maisha kwa kuzama.
Siku ya kuzuia watu kuzama ambayo ni 25 Julai ilipitishwa na Baraza Kuu la umoja wa Mataifa kwa mtazamo mmoja tu wa kuzuia kabisa watu kuzama ili vifo visitokee.
Takwimu za vifo vitokanavyo na kuzama
Ulimwenguni kote, WHO inakadiria kuwa angalau watu 236,000 hupoteza maisha yao kutokana na kuzama kila mwaka.
Kluge anasema “Ninasema angalau kwani nambari hizi zinawakilisha kuzama bila kukusudia. Kulingana na hali ya uainishaji, matukio ya kuzama yanayohusiana na usafiri wa maji, maafa ya mazingira, kujidhuru au mashambulizi hayajajumuishwa hapa. Hii kwa kweli inapunguza idadi kamili ya mzigo wa kimataifa wa kuzama kwa kati ya asilimia 30-50.”
Katika Kanda ya Ulaya ya WHO, kufa maji kunapoteza Maisha ya takriban watu 20,000 kila mwaka.
“Hii inaweza kuonekana kama sehemu ndogo ya idadi yote ya ulimwengu, lakini bado ni sababu ya pili ya vifo kwa watoto wa kati ya miaka 5-14.”
Ameongeza kuwa kuzama pia ni suala muhimu la usawa, kukiwa na tofauti ya mara 20 ya viwango vya vifo katika nchi 53 za Kanda ya Ulaya huku nchi za mashariki kwa ujumla zikiwa na viwango vya juu zaidi.
Takwimu sahihi ni muhimu katika kuelewa upeo wa changamoto na mambo mengi yanayohusika amesisitiza.
Kwa mfano, kwa kuzingatia mzigo wa kweli wa vifo vya kuzama nchini Uingereza ambako visababishi vyote vya kuzama majini vimehesabiwa, kwa hakika ni asilimia 165 zaidi kuliko wigo mdogo uliokadiriwa na WHO, pamoja na vifo vya kuzama kwa sababu ya kujidhuru kwa makusudi kwa wasiwasi fulani na kuongezeka kwa kipaumbele cha kitaifa kama janga linalopaswa kushughulikiwa.
Tofauti miongoni mwa nchi
Ongezeko la kuzama majini katika Kanda ya Ulaya ya WHO pia ni tofauti sana na ulimwengu wote.
“Vifo vya kuzama kwa wanaume wenye umri wa miaka 30-49 ni kubwa zaidi kati ya kanda zote sita za WHO. Hii inaonyesha ukweli kwamba kuzama kunahusishwa zaidi na burudani ya maji badala ya kuishi.”
Kisha, vifo vinavyoripotiwa vikiwa juu tu ya ncha ya barafu, kuzama pia husababisha wigo mpana wa majeraha yasiyoweza kusababisha kifo na athari kubwa za kiafya, kuanzia kuharibika kwa mfumo wa upumuaji kwa sababu ya kuvuta pumzi ya maji hadi majeraha ya ubongo na athari za muda mrefu maishani
Ulaya pia ina unywaji wa pombe wa juu zaidi ya kila mtu wa Kanda yoyote ya WHO. Hii inawakilisha sababu kuu ya hatari kwa aina zote za vurugu na majeraha. Pombe inahusishwa na asilimia 26 ya vifo vyote vya kuzama katika Kanda ya Ulaya, kuanzia asilimia 3 hadi zaidi ya asilimia 55 katika nchi za Kanda hiyo.
Isitoshe, shirika hilo la afya linasema tuna changamoto ya uhamiaji na viungo vyake vya kuzama, kama janga la hivi karibuni la Mediterania lilivyodhihirisha.
Kwa mujibu wa mradi wa watu waliopotea wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM takriban watu 34,000 wamezama katika kipindi cha uhamiaji tangu rekodi zilipoanza kukusanywa mwaka wa 2014. Hii inawakilisha asilimia 60 ya vifo vyote vinavyohusishwa na uhamiaji vilivyorekodiwa, na kati ya hivi, karibu wanne kati ya watano sawa na asilimia 76 vimetokea katika Kanda ya Ulaya English Channel na Mediterania.
Kuna dalili kuwa suala la kuzama majini linawekwa zaidi kwenye ajenda za afya na usalama.
Mwezi Mei 2023, Baraza la afya Ulimwenguni, lilipitisha azimio la kihistoria juu ya kuzuia kuzama, lililosimamiwa na nchi 72 zikiwemo 42 kati ya nchi 53 za Kanda ya Ulaya.