Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watoto na vijana hatarini kupoteza uwezo wa kusikia, kulikoni?

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linataka serikali ziwekeze katika huduma za kuepusha watu kupoteza uwezo wa masikio yao kusikia.
The London School of Hygiene & Tropical Medicine (LSHTM)/A. Smith
Shirika la afya la Umoja wa Mataifa linataka serikali ziwekeze katika huduma za kuepusha watu kupoteza uwezo wa masikio yao kusikia.

Mamilioni ya watoto na vijana hatarini kupoteza uwezo wa kusikia, kulikoni?

Afya

Je wafahamu zaidi ya watu bilioni 1 wenye umri wa kuanzia miaka 12 hadi 35 wako hatarini kupoteza uwezo wa masikio yao kusikia kutokana na masikio hayo kupata sauti kubwa kupita kiasi iwe kwa mtu kusikiliza mwenyewe au sauti zitokazo katika vipaza sauti vya shughuli za kijamii au umma?
 

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO limetanabaisha hilo leo kulekea siku ya kimataifa ya usikivu wa masikio kesho tarehe 3 mwezi Machi,maudhui yakiwa, Masikio kusikia maishani, sikiliza kwa ungalifu.

WHO inasema kuwa iwapo mwelekeo wa sasa wa kusikiliza kitu masikioni kwa sauti kubwa utaendelea, basi kuna madhara makubwa kwa afya ya mwili na akili pamoja na elimu na fursa za ajira.

Mkurugenzi wa Idara ya WHO ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza, Dkt. Bente Mikkelsen amesema mamilioni ya watoto na barubaru pamoja na vijana wako hatarini kupoteza uwezo wao wa kusikia kutokana na matumizi yasiyo salama ya vifaa vya kusikilizia sauti masikioni sambamba na sauti kubwa kwenye kumbi za vilabu vya usiku, matamasha na michezo.

Amesema hatari inaongezeka zaidi kwa kuwa vifaa vingi vya kusikilizia sauti, kumbi na matukio ya umma hayana maonyo au viwango vya usikilizaji na hivyo kusababisha hatari ya kupoteza usikivu kwa kuwa sauti huwa kubwa kupindukia.

WHO yaweka viwango vipya vya sauti 

Ni kwa mantiki hiyo, WHO imeweka mapendekezo sita ya viwango vipya vya sauti ya kusikiliza katika kumbi za starehe na michezo ili kulinda watoto na vijana dhidi ya kupoteza uwezo wa kusikia.

1. Wastani wa kiwango cha juu kisizidi 100 katika kipimo cha sauti.
2. Kuwepo kwa mfanyakazi anayefuatilia kiwango cha sauti kisizidi kiwango hicho cha 100.
3. Kuwepo kwa vifaa vya kudhibiti sauti kuenea maeneo mengine nje ya eneo husika ili usikivu usiwe wa vurugu.
4. Kuhakikisha kuna vifaa vya mtu kuweza kusikiliza binafsi na kuweko na maelezo ya matumizi.
5. Kuweko na eneo tulivu kwa watu wasiopenda kelele ili kupunguza hatari ya kupoteza usikivu
6. Wafanyakazi kupatiwa mafunzo na taarifa kuhusu umuhimu wa kulinda usikivu bora

Ukipoteza uwezo wa kusikia hakuna tiba, bali kuna kinga

WHO inasema kuwa kupoteza uwezo wa kusikia ni tatizo ambazo haliwezi kupatiwa tiba lakini linaweza kuzuilika. Ni kwa mantiki hiyo shirika hilo linataka vijana kuchukua hatua kwa kuhakikisha sauti inakuwa ya chini pindi wanapotumia vifaa vya kusikilizia masikioni. Halikadhalika vifaa hivyo viwe ni vile vinavyokata sauti za nje, kuvaa vizuia sauti kwenye kumbi zenye kelele kubwa na kufanya mara kwa mara uchunguzi wa uwezo wa sikio kusikia.

Serikali zichukue hatua

WHO inasihi serikali kuandaa sheria za usikikilizaji ulio salama na kuelimisha jamii kuhusu changamozo za kupoteza usikivu. Sekta binafsi nazo zinapaswa kujumuisha mapendekezo ya WHO kwenye bidhaa zao, kumbi na matukio. Na ili kuchagiza usikilizaji usio hatarini, WHO inataka uhamasishaji wa ubadilishaji tabia ufanywe na mashirika ya kiraia, wazazi, walimu, madaktari na kadhalika.