Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS yatiwa hofu na mauaji ya binadamu na uporaji wa mifugo Equatoria Mashariki

Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini
UNMISS
Watu walioyakimbia makazi yao katika eneo la Equatoria Magharibi Sudan Kusini

UNMISS yatiwa hofu na mauaji ya binadamu na uporaji wa mifugo Equatoria Mashariki

Amani na Usalama

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS umeelezea masikitiko yake makubwa kutokana na vitendo vya uporaji wa mifugo vinavyoambatana na mauaji ya raia na utekaji nyara katika jimbo la Equatoria Mashariki nchini humo.

Hayo yameelezwa na msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric wakati akizungumza na waandishi wa habari hii leo jijini New York, Marekani.

Amenukuu UNMISS ikisema kuwa tayari imepeleka walinda amani wa Umoja wa Mataifa eneo hilo ilikuendesha doria ya masafa marefu ya siku nne kama njia ya kutokomeza ghasia na kurejesha Imani ya usalama miongoni mwa wanajamii.

“Halikadhalika UNMISS inaendelea kuwepo kwenye eneo hilo na kushirikiana na mamlaka husika za maenoe hayo pamoja na jamii zilizoathirika ili kutathmini kwa kina kilichotokea na kisha kuepusha mashambulizi ya kulipiza kisasi,” amesema Bwana Dujarric.

Kwa mujibu wa Bwana Dujarric, hofu kubwa ya UNMISS ni kwamba baadhi ya vijana wanajipanga na kuhamasishana kufanya kampeni ya mashambulizi ya kurejesha mifugo yao iliyoibwa na hivyo, “UNMISS inaomba serikali ya kitaifa Sudan Kusini, serikali ya jimbo na viongozi wa kijamii wachukue hatua za dharura kuepusha kusambaa kwa ghasia.”