Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNMISS na wadau wafanya msako kubaini iwapo wanawake na watoto wanatumikishwa jeshini

Timu ya pamoja kuhusu ulinzi wa watoto na wanawake nchini Sudan Kusini imetembelea kambi ya Sue jimboni Gbudue huko Equatoria Magharibi kuchunguza iwapo kuna watoto au wanawake waliotumikishwa jeshini.
UN Photo/ Denis Louro

Amani na Usalama

Ujumbe wa maafisa wa Umoja wa Mataifa na wadau wa Sudan Kusini uliokwenda kusaka iwapo kuna watoto au wanawake wanaotumikishwa na vikundi vilivyojihami kwenye eneo Equatoria Magharibi nchini humo, umebaini kutokuwepo hata mmoja aliyesajiliwa kinguvu. 

Msafara wa maafisa wa Umoja wa Mataifa na na wale serikali na vikundi vya upinzani Sudan Kusini ukipita mito, mabonde na misitu minene ya eneo la Equatoria magharibi nchi hiyo, kwa takribani saa 5. Ingawa barabara si nzuri, hatimaye waliwasili kwenye kambi ya Sue.

Jukumu lao ni kuona iwapo katika kambi hii ya kijeshi kuna watoto au wanawake waliotumikishwa kwenye kikosi cha SPLA upande wa upinzani.

Kambi hii ilianzishwa mwezi Agosti mwaka huu kama sehemu ya utekelezaji wa mkataba mpya wa amani mwezi Septemba mwaka 2018 wenye lengo la kusuluhisha mzozo wa Sudan Kusini.

Takribani askari 491 walipiga gwaride, wakiwemo wanawake 441 wakichunguzwa iwapo kuna wavulana, wasichana au wanawake waliojiunga na kikundi hicho kinyume na matakwa yao.

Timu ya pamoja kuhusu ulinzi wa watoto na wanawake nchini Sudan Kusini imetembelea kambi ya Sue jimboni Gbudue huko Equatoria Magharibi kuchunguza iwapo kuna watoto au wanawake waliotumikishwa jeshini.
UN Photo/ Denis Louro
Timu ya pamoja kuhusu ulinzi wa watoto na wanawake nchini Sudan Kusini imetembelea kambi ya Sue jimboni Gbudue huko Equatoria Magharibi kuchunguza iwapo kuna watoto au wanawake waliotumikishwa jeshini.

Magloire Agoua, ni afisa wa ulinzi wa mtoto, kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS ambaye amesema, “ujumbe tunaopitisha hapa ni kwamba, hebu na tulinde watoto, hili ni moja ya jukumu la UNMISS  ambalo ni kulinda watoto na raia- na si tu watoto au wavulana bali pia wanawake kwa kuwa tupo hapa kwa lengo hilo.”

Gwaride hili lilitoa fursa nzuri ya timu ya kutathmini kufanya kazi yake ikiwemo kuzungumza na askari hao. Philip Ghazy anatoka kamisheni ya kupokonya silaha, kuvunja makundi na kujumuisha askari kwenye jamii naye amesema, “tumekuwa tukijaribu kuona iwapo tutapata watu tunaowatafuta. Lakini hakuna hata mmoja, hatukupata mtoto au mwanamke aliyetekwa. Wanawake waliopo hapa ni wake wa wanajeshi au hata watoto waliopo hapa ni watoto wa wanajeshi. Hii ni baada ya mashauriano na makundi mbalimbali.”

Afisa mwandamizi wa SPLA upande wa upinzani, Luteni Jenerali Alfred Fitio Karaba Malisi amekanusha madai ya kutumikisha watoto akisema.. “nashukuru Mungu wamefika hapa na tupo eneo hili la kambi ya Sue. Tumetafuta na hakuna mtu yeyote aliyetekwa. Hakuna mwanamke aliyetekwa. Machifu wote wapo nasi, halikadhalika raia.”

Jopo hili la tathmini linatarajia kutembelea maeneo mengine nchini Sudan Kusini huku likiomba kupatiwa taarifa kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za watoto na wanawake.