Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatimaye Baraza laidhinisha shehena ziendelee kupelekewa Syria kupitia Uturuki

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA wakivuka kutoka Uturuki kuingia Syria kutathimini mahitaji ya jamii za wakimbizi wa ndani.
UNOCHA
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA wakivuka kutoka Uturuki kuingia Syria kutathimini mahitaji ya jamii za wakimbizi wa ndani.

Hatimaye Baraza laidhinisha shehena ziendelee kupelekewa Syria kupitia Uturuki

Msaada wa Kibinadamu

Baada ya vuta nikuvute ya siku kadhaa, hatimaye hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kuidhinisha tena usafirishaji wa shehena za misaada ya kibinadamu kwenda nchini Syria kupitia eneo la Bab al-Hawa lililoko kwenye mpaka wa taifa hilo na Uturuki.

Azimio hilo limepitishwa leo baada ya azimio la awali namba 2585 kumalizika Jumapili tarehe 10 mwezi Julai na sasa muda umeongezwa kwa miezi sita hadi tarehe 10 mwezi Januari mwaka ujao wa 2023.

Azimio hilo limepitishwa kwa kura 12 huku ikiwa hakuna mjumbe yeyote aliyetumia kura turufu miongoni mwa wajumbe watano wenye kura hiyo, huku mataifa matatu: Uingereza, Marekani na Ufaransa yote yakiwa na kura turufu, wakijiengua katika upigaji kura.

Ilikuwa ni vuta nikuvute

Rasimu ya azimio hilo iliwalisilishwa na Syria, Ireland na Norway.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Mwakilishi wa kudumu wa Ireland kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Geraldine Byrne Nason, amesema, “azimio limepita baada ya mijadala mikali na ya kina..”

“Siyo siri kwamba yamekuwa ni mashauriano magumu. Kama waandaaji wa rasimu ya azimio hili, Ireland na Norway tumekuwa na mashauriano ya kina nay a dhati na wajumbe wote wa Baraza. Baada ya rasimu ya azimio kuwekwa mezani wiki iliyopita, lilipigiwa kura ya turufu. Tuliongeza juhudi zetu maradufu kusaka njia sahihi ili Baraza lipitishe azimio hili ambalo litaruhusu watoa huduma za kibinadamu waendelee kufikia wale wenye uhitafaji nchini Syria,” amesema Balozi Nason.

Baba na mwanae wakiwa wamebeba hema la familia kwenye kambi ya Kerama huko Kaskazini mwa Syria karibu na eneo la Bab Al-Hawa mpakani na Uturuki.
UNHCR
Baba na mwanae wakiwa wamebeba hema la familia kwenye kambi ya Kerama huko Kaskazini mwa Syria karibu na eneo la Bab Al-Hawa mpakani na Uturuki.

Amesisitiza kuwa kwa wananchi wa Syria na watoa huduma za kibinadamu, siku mbili zilizopita zilikuwa za kutokuwa na uhakika wa kinachofuatia akiongeza kuwa hofu ni kwamba misaada muhimu ingalikoma na hivyo kutokuwa na matumaini na hofu ilijengeka.

Mwakilishi huyo wa kudumu wa Ireland amesema kipindi hicho cha nyongeza cha miezi sita ni kifupi kuliko kile ambacho azimio lilipendekeza na kwamba wajumbe wengi wa Baraza nao walikuwa na mtazamo huo.

Ingawa hivyo Balozi Nason amesema, “kile muhimu kwa leo ni kwamba Baraza limepitisha azimio la kuona mpaka unakuwa wazi na misaada inaendelea kupitishwa ili kufikia wahitaji.”

Kupitishwa kwa azimio ni nuru kwa wananchi wa Syria

Akihutubia Baraza hilo, Mwakilishi wa Kudumu wa Norway kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mona Juul, amesema azimio lililopitishwa linaruhusu operesheni za kuokoa maisha kaskazini-magharibi mwa Syria, ambako wahitaji walikumbwa na tashwishwi wakati wote mazungumzo na mashauriano yalipokuwa yanaendelea.

“Tunaweza kuwahakikishia hivi sasa na hilo ndilo la msingi. Operesheni hizo za kusambaza huduma za kibinadamu kupitia mpakani ndio uhai wao. Na leo hii operesheni hizo zimefunguka,” amesema Juul.

Ijumaa iliyopita ya tarehe 8 mwezi huu wa Julai, Baraza lilishindwa kupitisha rasimu mbili za maazimio ambayo yangaliongeza muda huo, ambapo rasimu moja iliyowasilishwa na Norway, Syria na Ireland ilipigiwa kura turufu na Urusi huku ile iliyowasilishwa na Urusi ilipitishwa kwa kura mbili tu turufu ambazo ni ya Urusi yenyewe na China.

Vita nchini Syria ilianza mwaka 2011 na hadi sasa suluhu ya kudumu bado haijapatikana.