Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama laongeza mwaka mmoja wa kuingiza misaada ya kuokoa maisha Syria

Ahmad mwenye miaka 7 (kushoto ) na mdogo wake Saad mwenye miaka 5 wakiwa wamebeba vifaa vya kujisafi kuelekea kwenye hema lao katika kambi ya Fafin Kaskazini mwa jimbo la Aleppo vijijini Syria.
© UNICEF/Ali Almatar

Amani na Usalama

Leo Jumamosi Julai 11 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa katika jaribio la nne limefanikiwa kupiga kura na kupitisha mswada wa azimio nambari 2533 (2020)  lililowasilishwa na Ujerumani,  ambalo linaidhinisha makubaliano ya shughuli za kuvusha misaada ya kibinadamu kupitia mpaka wa Uturuki kuingia Syria kwa mwaka mmoja zaidi.

Mswada huo umepita baada ya kupigiwa kura ya ndiyo na wajumbe 12 wa baraza hilo huku wajumbe watatu wakiwemo Urusi, Jamhuri ya Dominica na Uchina wakijizuia kupiga kura.

Azimio hilo lililokfanyiwa marekebisho litaruhusu uingizaji wa chakula, madawa na misaada mingine ya kuokoa maisha kupitia eneo la mpakani la Bab al-Hawa.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ambao ndio waliodhamini kwa pamoja na Ubelgiji azimio hilo Bwana. Heiko Maas amesema wamefurahishwa na hatua hiyo “Ni Habari njema kwa mamilioni ya raia wa Syria kwamba Baraza la Usalama limeweza kuafikiana katika mapendekezo yetu.”

Mwezi uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakiwa katika kikao kwa njia ya video kwa ajili ya kuijadili hali ya kisiasa nchini Syria.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Mwezi uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wakiwa katika kikao kwa njia ya video kwa ajili ya kuijadili hali ya kisiasa nchini Syria.

Kumekuwa na shinikizo kubwa kwa Baraza la Usalama kuongeza muda zaidi wa kuvush misaada ya kibinadamu kuingia Syria kutokana na umuhimu wa misaada hiyo katika kuokoa maisha ya mamilioni ya watu hasa katika eneo la Kaskazini Magharibi mwa taifa hilo ambako hali ya usalama bado ni tete na raia wengi wamekwama kutokana na mapigano.

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharira OCHA, watu milioni 2.8 wanawake, wanaume na watoto wanahitaji msaada wa kibinadamu Kaskazini Magharibi mwa Syria.

Azimio la awali nambari 2504 lililoruhusu operesheni za kibinadamu Syria kwa miaka 6 lilifikia ukomo usiku wa kuamkia jana tarehe 10 Julai na kuwaacha mamilioni ya raia wa Syria njiapanda.