UNMISS yaendesha mafunzo ya kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia

11 Julai 2022

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini UNMISS umeendesha mafunzo ya kukabiliana na unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ubakaji katika eneo la makutano la  Aru jimboni Equatoria ya Kati ikiwa ni njia mojawapo ya kuwaandaa wananchi kujilinda kwa kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vimekuwa vikijirudia na kuathiri zaidi wanawake na wasichana. 

Katika taifa changa zaidi duniani Sudan Kusini , Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo UNMISS umeweka dhamira ya dhati ya kukuza ufahamu kuhusu kukomesha unyanyasaji wa kingono unaohusiana na migogoro ambapo kiongozi wa jumuiya katika eneo la Aru Rose Luri Sarafino anasema "unyanyasaji wa kijinsia ni jambo la kawaida linatokea Aru kama ilivyo kuwa katika maeneo mengine ya nchi kwa hiyo mafunzo wanayopatiwa na UNMISS yamekuja muda muafaka." 
 
Sarafino ameongeza kuwa “Nimeona semina hii kuwa ni muhimu sana. Miongoni mwa mambo ambayo tumesikia hapa ni umuhimu wa haki na sisi hatutaki mambo mabaya yatokee. Tunafurahi na watu wa UNMISS waliokuja kuzungumza nasi” 

Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wake kwa waume na Alfred Madoghadegho baba huyu mwenye watoto wa kike anasema amahakika mafunzo yamemfungua macho. "Ikiwa binti amebakwa au kutekwa nyara na mtu hana chochote mkononi, basi hawezi kujitetea. Lakini sasa najua msichana wa namna hiyo akibakwa au kutekwa naweza kwenda kwa chifu wa mtaa ambaye ataweza kunisindikiza hadi niwafikie nyinyi. Nimefurahiya sana na nitatumia habari hii. Pia nitawajulisha watoto wangu nyumbani kuhusu hili.” 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter