Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukatili wa kutisha waendelea kuripotiwa Tarhuna- Ripoti

Raia wamelipa gharama kubwa ya vita nchini Libya
UNMAS/Giovanni Diffidenti
Raia wamelipa gharama kubwa ya vita nchini Libya

Ukatili wa kutisha waendelea kuripotiwa Tarhuna- Ripoti

Haki za binadamu

Makaburi mapya yanayoshukiwa kuzika watu wengi kwa pamoja yamebainika huko Tarhuna nchini Libya, imesema ripoti mpya ya uchunguzi iliyotolewa leo na Tume Huru iliyoundwa na Baraza la  Umoja wa Mataifa la haki za binadamu.

Tume hiyo iliyoundwa na Baraza hilo tarehe 22 mwezi Juni mwaka 2020 kufuatia ombi la serikali ya Libya imewasilisha ripoti hyo leo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Mohammed Auajjar amesema kubainika kwa makaburi hayo ni dalili ya kuendelea kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu katika taifa hilo ambako waathirika wakubwa ni watoto na watu wazima.

“Kitendo cha ukwepaji sheria kimeendelea kuenea katika taifa hilo lililogubikwa na vita na hivyo kuwa ni kikwazo kikubwa cha maridhiano ya kitaifa, ukweli, na haki kwa waathirika na familia zao,” amesema Bwana Auajjar.

Kuhusu Tarhuna, ripoti yao imekusanya shuhuda na kubaini Ushahidi wa “kuenea kwa mfumo wa watu kutoweshwa, uuaji, utesaji na ufungaji wa watu jela vitendo ambavyo ni uhalifu dhidi ya binadamu uliofanywa na Al Kani au wanamgambo wa Kaniyat.”

Kati ya mwaka 2015 na 2020, wanamgambo hao walitawala eneo la Tarhuna kupitia kampeni ya vitisho, kujenga hofu na uonevu dhidi ya wakazi wa mji huo na hata kuwaua.

Teknolojia imefanikisha 

Matumizi ya teknolojia ya kisasa yaliwezesha timu ya Tume hiyo kuweza kubaini makaburi ya pamoja ambayo awali kwenye mji huo wa Tarhuna. “Eneo hilo liko kilometa 65 kutoka mji mkuu wa Libya, Tripoli. Hata hivyo hatufahamu idadi  ya makaburi hayo ya pamoja, yanahitaji kufukuliwa. Lakini hadi sasa kuna mamia ya watu ambao hawajajulikana wlaiko, ambao wametoweka.” Amesema Bwana Auajjar.

Zaidi ya watu 200 bado hawajulikani waliko huko Tarhuna na maeneo ya Jirani na hivyo kusababisha, “machungu na majonzi yasiyoelezeka kwa familia zao ambazo zina haki ya kujua ukweli juu hatma ya wapendwa wao,” ameendelea kusema Bwana Auajjar.

Mtoto wa miaka 14 mkimbizi kutoka Niher akiwa ameweka mkono wake katika geti akiwa kizuizini nchini Libya
© UNICEF/Alessio Romenzi
Mtoto wa miaka 14 mkimbizi kutoka Niher akiwa ameweka mkono wake katika geti akiwa kizuizini nchini Libya

Wapazao sauti wanalengwa

Wanawake na wasichana nao wamekumbwa na zahma zilizofuatia tangu kuangushwa kutoka madarakani Rais wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi mwaka 2011.

Hii leo licha ya maendeleo yaliyopatikana katika kumaliza tofauti kati ya pande kinzani nchini Libya, serikali ya Libya inayotambulika kimataifa bado iko katika mvutano na utawala kinzani na mamlaka za bunge mashariki mwa taifa hilo la kaskazini mwa Afrika.

Miongoni mwa yaliyobainishwa na ripoti ya Tume hiyo ni kwamba pale wanawake wanapojitokeza kutaka kushiriki kwenye uchaguzi wa kitaifa ambao bado kufanyika, wanalengwa kwa kubaguuliwa au kunyanyaswa.

Baadhi yao wametekwa, ikiwa sehemu ya mlolongo wa matukio ya watu kutoweshwa ambayo hayachukuliwi hatua yoyote nchini Libya ambapo Bwana Auajjar amemtaja mbunge Sihem Sirgiwa ambaye alitekwa mwaka 2019.

“Ubaguzi na ghasia ni moja ya mambo yanayotokea kila siku kwa wanawake na wasichana zaidi nchini Libya,” amefafanua Bwana Auajjar akisema, “hofu kubwa ya Tume ni kushindwa kwa sheria za nchi kulinda raia dhidi ya ukatili wa kingono na kijinsia.”

Ukosefu wa nguvu ya kisheria

Licha ya kukaribisha kuundwa kwa mahakama mbili za kuhusika na ukatili dhidi ya wanawke na watoto, tume hiyo inayojumuisha wataalamu wa haki imeonya kuwa vijana wanakabiliwa na kuuawa, kuwekwa ndani kiholela, ukatili wa kijinsia na kingono sambamba na kuteswa.

Miongoni mwao ni wale wanaoambatana na wahamiaji watu wazima, wakimbizi, wasaka hifadhi ambao wanashikiliwa katika maeneo katili nchiin Libya.

Tume hiyo itawasilisha mbele ya Baraza la Haki za Binadamu ripoti hii ya tatu Jumatano wiki hii ya tarehe 6 mwezi Julai.