Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yapaza sauti kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu ya Marekani kuhusu utoaji mimba

Watetezi wa haki ya utoaji mimba wakiandamana mjini Washington D.C mwezi Oktoba mwaka 2021
© Unsplash/Gayatri Malhotra
Watetezi wa haki ya utoaji mimba wakiandamana mjini Washington D.C mwezi Oktoba mwaka 2021

Mashirika ya UN yapaza sauti kufuatia uamuzi wa Mahakama Kuu ya Marekani kuhusu utoaji mimba

Afya

Iwe utoaji wa mimba ni halali kisheria au si halali kisheria, bado hufanyika mara kwa mara, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu na afya ya uzazi duniani, UNFPA hii leo kupitia taarifa iliyotolewa jijini New York, Marekani.

Taarifa hiyo imetolewa wakati Mahakama Kuu ya Marekani imetupilia mbali hoja ya haki kikatiba ya utoaji wa mimba na kuacha suala hilo mikononi mwa majimbo.

UNFPA kupitia taarifa yake, inanukuu Ripoti ya mwaka huu ya hali ya idadi ya watu duniani ambayo ilifichua ya kwamba takribani nusu ya mimba au  ujauzito wote unaobebwa na wanawake na wasichana duniani haikuwa imepangwa na zaidi ya yote huishia kutolewa.

Tweet URL

“Takwimu zinaonesha kuwa kuzuia utoaji mimba hakuzuii watu kusaka huduma ya utoaji wa mimba, na zaidi ni kwamba utoaji huo hufanyika katika mazingira hatarishi,” imesema UNFPA.
Asilimia 45 ya utoaji mimba duniani kote si silama

Takwimu zinatisha! Kwa kuwa asilimia 45 ya mimba zinazotolewa, hufanyika kwa njia isiyo salama na hivyo kufanya kuwa sababu kubwa inayoongoza ya vifo vya wajawazito.

Kinachotisha zaidi, ni kwamba takribani nusu ya mimba zote zinazotolewa kwa njia zisizo salama hufanyika katika nchi zinazoendelea, “na UNFPA inahofu kuwa kutakuwepo na utoaji mimba zaidi usio salama iwapo huduma ya utoaji mimba kwa njia salama hazitakuweko.”

UNFPA inasema uamuzi wa kupindua mafanikio yaliyopatikana una madhara mapana kwa haki na uwezo wa wanawake na barubaru kokote duniani.

Programu ya mwaka 1994 inatekelezwa na kila nchi

Shirika hilo linafafanua kuwa Programu ya utekelezaji iliyopitishwa wakati wa mkutano wa kimataifa wa Idadi ya watu na maendeleo mwaka 1994 na kutiwa saini na mataifa 179 ikiwemo Marekani inatambua ni kwa kiasi gani kuna hatari kubwa katika utoaji mimba usio salama na inasihi mataifa yote kutoa huduma kwa wanawake baada ya utoaji mimba bila kujali inakubalika kisheria au la.

Ukosefu wa taarifa au uelewa kuhusu ngono na afya ya uzazi umechangia msichana wa miaka 18 kupata mimba isiyo tarajiwa huko Timor Leste
© UNFPA/Ruth Carr
Ukosefu wa taarifa au uelewa kuhusu ngono na afya ya uzazi umechangia msichana wa miaka 18 kupata mimba isiyo tarajiwa huko Timor Leste

Halikadhalika program hiyo inataka watu wawe na fursa ya kupata taarifa bora na sahihi kuhusu afya yao ya uzazi na njia za uzazi wa mpango.

UN Women nayo yakazia kauli ya UNFPA

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la kushughulikia masualaya wanawake, UN Women limesema haki ya afya ya uzazi kwa wanawake ni haki ya binadamu.

Taarifa ya shirika hilo iliyotolewa leo jijini New York, Marekani inasema haki za afya ya  uzazi ni sehemu ya haki za wanawake suala ambalo linakaziwa na mikataba ya kimataifa na kuakisiwa katika sheria za nchi mbalimbali duniani.
 
Shirika hilo linasema, “pindi utoaji mimba salama na unaofanyika kisheria unapokumbwa na vikwazo, wanawake wanalazimika kusaka utoaji mimba  usio salama na mara nyingi huwa na madhara makubwa kiafya hasa kwa wanawake masikini na walio pembezoni.”

“UN Women inasalia na azma yake ya kuhakikisha haki za wanawake na wasichana zinazingatiwa na kufurahiwa duniani kote na tutaendelea kushirikiana na wadau wetu kwa kutumia ushahidi mahsusi ili haki hizi zifurahiwe duniani kote,” imesema UN Women kupitia taarifa iliyotolewa leo baada ya uamuzi kutoka Mahakama Kuu ya Marekani wa kupindua suala la utoaji mimba kuwa haki ya kikatiba, na jukumu kuachiwa serikali za majimbo.