Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC na EU waleta tija kwenye mfumo mbadala wa sheria nchini Kenya

Mkutano wa kwanza wa mfumo mbadala wa sheria nchini Kenya, AJS uliondaliwa na UNODC na kufanyika mjini Nairobi, Kenya.
UN/ Thelma Mwadzaya
Mkutano wa kwanza wa mfumo mbadala wa sheria nchini Kenya, AJS uliondaliwa na UNODC na kufanyika mjini Nairobi, Kenya.

UNODC na EU waleta tija kwenye mfumo mbadala wa sheria nchini Kenya

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na kukabiliana na madawa ya kulevya na uhalifu UNODC imesema mfumo mbadala wa kutimiza na kusaka haki na sheria umeanza kuzaa matunda nchini Kenya. 

Mpango huo unaowaleta pamoja wazee wa jamii na viongozi wa kidini kwenye meza ya mazungumzo ili kusaka suluu, umefanikiwa kutatua kesi katika jamii pasi na kuzihusisha mahakama rasmi na vyombo vyengine vya sheria na usalama. 

Kongamano la kwanza la mwaka la mfumo huo wa sheria mbadala lililoandaliwa na UNODC limefanyika kwa siku mbili kwenye chuo kikuu cha Tangaza jijini Nairobi. 

Malengo ya mfumo huo ni kudumisha amani katika jamii. Kwa muda wa miaka 4 ofisi ya UNODC, kwa ufadhili wa Muungano wa  Ulaya EU imekuwa likisimamia mradi wa uwezeshaji na utoaji wa misaada ya kisheria nchini Kenya, ujulikanao kama PLEAD. 

Ushirikiano wa EU na UNODC 

Mpango wa PLEAD una mizizi yake kwenye dira ya mkakati wa Kenya wa maendeleo endeleo ya 2030 kwa kuunga mkono mageuzi yanayolenga kuibadili sekta ya haki katika masuala ya uhalifu. 

Mradi huo unaofadhiliwa na EU ndio mkubwa zaidi wa aina hiyo katika eneo lililo kusini mwa jangwa la Sahara. 

UNODC inasema baadhi ya malengo yake maalum kwa mwaka huu ni kuweza kupunguza idadi ya kesi zilizokwama mahakamani kwa asilimia 50% kadhalika idadi ya watu wanaozuiliwa jela kabla ya kesi zao kuamuliwa kwa asilimia 30% ili kuondoa msongamano magerezani. 

Kwa sasa mpango wa PLEAD unajikita katika kaunti 12 ila janga la COVID 19 liliivuruga mipango ya kuupanua wigo wa mradi huo ambao sasa uko katika mahakama 11. 

Mradi wa PLEAD unafanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali ili kufanikisha azma yao. 

Mohamed Jaffar ni mshauri katika ofisi ya UNODC na anasema kuwa  ,” Kwanza wazee wanafaa kuona kuwa katiba inawaruhusu kusaka mbinu za suluhu ya migogoro.Pili ni yapi kule mashinani wanayoyaona kuwa yanafanya kazi kupitia wazee.Sisi kama UNODC kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya ni kuweza kuwasukuma zaidi kusaka suluhu kwa njia mbadala isiwe kesi zote zinaishia mahakamani au gerezani.” 

Mrundiko wa kesi mahakamani 

Kwenye kongamano hilo la kwanza la mwaka la kuutambua mchango wa mpango mbadala wa sheria na haki, Jaji Mkuu wa Kenya Martha Koome ametoa wito kwa maafisa wa idara ya mahakama kuutumia mfumo huo zaidi ili kutatua kesi za mizozo.  

Naibu Jaji Mkuu wa Kenya Philomena Mwilu aliyewasilisha ujumbe huo anakiri kuwa ipo haja kwa watu wote kupewa haki,”Mwanamke yuko na haki sawa na mwanamume.Hakuna raha inaweza kuzidi ile raha ya kwamba idara ya mahakama ambayo inahakikisha kuwa sheria iliyotungwa na bunge la taifa inatimzwa kwa mujibu wa katiba.” 

Idara ya mahakama ya Kenya inazongwa na mrundiko wa kesi hali inayofanya mfumo mzima wa haki kusuasua.  

Kulingana na Jaji Joel Ngugi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya utekelezaji wa mfumo mbadala wa sheria katika idara ya mahakama, mpango huo umeleta tija kwa wakaazi wa vijiji hasa vya mashinani.  

Baadhi ya kesi zimekwama mahakamani kwa miaka kadhaa jambo linalowanyima haki wahusika hasa waliodhulumiwa. 

Wakitolea mfano wamesema Kaunti ya Kajiado imefanikiwa kutatua kesi 33 za mizozo ya ardhi katika muda wa miezi sita iliyopita wakati kesi za aina hiyo huchukua muda usiopungua miaka 3 kusuluhisha kwa njia rasmi za mahakamani. 

Mizozo ya maliasili 

Shirika la Umoja wa Mataifa la kilimo na chakula FAO limeshirikishwa kwenye mpango mzima wa haki na sheria mbadala ukizingatia kuwa mizozo ya ardhi huathiri shughuli za kilimo, ufugaji na mali asili. 

Husna Mubarak ni msimamizi wa masuala ya mali asili katika shirika la FAO na anafafanua kuwa, “ Pale mizozo ya ardhi inapokithiri inakuwa vigumu kulinda haki kadhalika mali asili au kutimiza shughuli za kilimo na ufugaji. Na hilo linakwamisha harakati za kuhakisha jamii inakuwa na lishe na afya bora.” 

Mkutano huo ulioanza jana umekunja jamvi leo huku pofisi ya UNODC ikisema kwa muda ambao umekuwa ukitumia mfumo huo wa haki mbadfala za kisheria umeleta tija kubwa nchini Kenya.