Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNODC na wadau waanzisha kituo cha ushauri nasaha katika gereza la Langata Kenya

Bamba la kumbukumbu kwenye ukuta wa kituo cha ushauri nasaha katika jela ya Langata nchini Kenya.
UN News/Thelma Mwadzaya
Bamba la kumbukumbu kwenye ukuta wa kituo cha ushauri nasaha katika jela ya Langata nchini Kenya.

UNODC na wadau waanzisha kituo cha ushauri nasaha katika gereza la Langata Kenya

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Kwa mara ya kwanza katika historia ya magereza nchini Kenya, jela kuu ya wanawake ya Langata imepata kituo kipya cha kuwapa maafisa wake ushauri nasaha.Utafiti umebaini kuwa maafisa wa magereza wanakabiliana na hali ngumu kiakili kwasababu ya majukumu yao. 

Matatizo ya kiakili yanayowatatiza ni msongo wa mawazo, mfadhaiko wa kiakili na madhara ya mihadarati. 

Kituo hicho kipya kimejengwa kwa ufadhili wa serikali ya Canada na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupambana na mihadarati na uhalifu UNODC

Ushauri nasaha ni muhumi kuwawezesha maafisa hao kupambana na mahitaji ya kazi.Gereza la Langata lina sehemu tatu ambazo ni jela kuu ya waliohukumiwa mauaji na wizi wa mabavu, kituo cha marekebisho ya tabia na rumande. 

Wafungwa wa jela ya Langata wakiwatumbuiza wageni kwenye uzinduzi wa kituo cha ushauri nasaha kwa maafisa wa magereza.
UN News/Thelma Mwadzaya
Wafungwa wa jela ya Langata wakiwatumbuiza wageni kwenye uzinduzi wa kituo cha ushauri nasaha kwa maafisa wa magereza.

Idadi kubwa ya wafungwa ni changamoto 

Maisha katika jela yoyote ile sio rahisi kwa wafungwa na wasimamizi wao.Hii ni kwasababu mawazo na ratiba kali za jela huwasukuma baadhi kupata matatizo ya akili.  

Nchini Kenya gereza la Langata ndicho kituo kikubwa zaidi cha wafungwa wanawake waliohukumiwa kwa makosa mazito kama mauaji na wizi wa mabavu. 

Takriban maafisa elfu 22 wanahudumu kwenye magereza nchini. Na idadi ya wafungwa ni zaidi ya maradufu ile ya maafisa. 

Hali hiyo inawaweka maafisa wa magereza katika mtihani ngumu kiakili kwani wanaowasimamia ni wahalifu wa madaraja mbalimbali. 

Ili kuwashika mkono maafisa wa magereza,serikali ya Canada na Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na mihadarati na Uhalifu, UNODC,wamezindua kituo cha kwanza na cha kipekee cha kutoa ushauri nasaha ndani ya magereza ya wanawake ya Langata. 

Charity Kagwi Ndungu ni mwakilishi wa UNODC na anasisitiza kuwa dhamira ni kuibadili tabia kwani,“Kazi yetu ni kusaidia marekebisho ya adhabu, na marekebisho ya mfumo wa adhabu.Na marekebisho lazma yaangalie yule anayefanya kazi huko na mfungwa.Marekebisho yanaangalia ujumla ndio yasaidie watu wasifurike kwenye magereza yetu.Hayo, siyo matumizi bora ya rasilimali watu, hawa watu wanahitajika kutoka waende kufanya kazi ili tujenge taifa.” 

Kituo kipya cha ushauri nasaha kilichozinduliwa na UNODC na Serikali ya Canada.
UN News/Thelma Mwadzaya
Kituo kipya cha ushauri nasaha kilichozinduliwa na UNODC na Serikali ya Canada.

Mchango mkubwa wa ushauri nasaha 

Utafiti umebaini kuwa ushauri nasaha una mchango muhimu katika kupunguza msongo wa mawazo na kuepusha uhalifu wa kikatili uliokithiri. 

Imebainika kuwa maafisa wa magereza wanakabiliana na hali ngumu ukizingatia kuwa wafungwa wanaweza kuwa na misimamo mikali, tabia zisizoridhisha na pia machungu kwa kunyimwa uhuru wao.  

Mchango wa ushauri nasaha katika usimamizi mujarab wa idara ya magereza ni mkubwa kama anavyoelezea Dkt. Judith Pete kutoka Chuo Kikuu cha Tangaza kinachotoa huduma hiyo pasi na malipo. 

Chuo Kikuu cha Tangaza cha Kanisa Katoliki ni mmoja ya washirika wa magereza wanaotoa ushauri nasaha pasina malipo. 

Dkt Judith Pete ni Mshauri nasaha na mhadhiri, katika Chuo kikuu cha Tangaza na anaelezea kuwa,”“Kuna changamoto sana katika maafisa ambao wanafanya kazi katika gereza.Tunaona mara nyingi wengi wao wanajiua , hawana raha hata ukiongea nao akili haipo mlipo.Lakini ni jukumu letu sisi kama walimu tuone ya kwamba tunajaribu kupunguza changamoto hizo kwa hao maafisa”. 

Kulingana na tathmini ya magereza,maafisa 40 pekee mpaka sasa wamepokea huduma za ushauri nasaha katika jela ya wanawake ya Langata. 

Ili kufanikisha mradi huu, washauri nasaha binafsi kutoka mashirika ya kijamii hujitolea kutoa huduma ya ushauri nasaha. 

Soony Wendy ni mshauri nasaha kutoka Shirika la Coalition Action For Preventing Mental Health anafafanua kuwa,”Wale ambao wanawasaida, hawa maaskari wamekuwa wakiachwa nyuma.Kwahiyo hili ni jambo kubwa sana na nimefurahia kwasababu hao pia wataweza kupata usaidizi na kuwasaidia wafungwa.Wakati unapata kujijua na kuelewa jinsi afya yako ya akili unaweza kuitunza na kuilinda,tunaweza kuzuwia watu wengi kuja hapa na pia kuzuwia askari wengi kuwa na haya magonjwa ya akili ambayo wanayapata huku ndani.” 

Wawakilishi wa UNODC,Serikali ya Canada na viongozi wa magereza wakisikiliza hotuba kwenye uzinduzi wa kituo kipya cha ushauri nasaha jela ya Langata.
UN News/Thelma Mwadzaya
Wawakilishi wa UNODC,Serikali ya Canada na viongozi wa magereza wakisikiliza hotuba kwenye uzinduzi wa kituo kipya cha ushauri nasaha jela ya Langata.

Mradi wa haki wa PLEAD 

Ofisi ya Umoja wa Mataifa la kupambana na mihadarati na Uhalifu, UNODC na Idara ya mahakama mapema mwaka huu waliafikiana kuimarisha miradi inayowalenga zaidi masikini na wasiojiweza katika jamii nchini Kenya. 

Kuanzia Machi mwaka huu, mradi wa kuleta mabadiliko na haki,PLEAD wa ofisi ya UNODC, utaingia awamu yake ya pili. 

Magereza ya wanawake ya Langata ilipokea ufadhili kwa ujenzi wa jengo maalum la kuwahifadhi wafungwa waliohukumiwa kwa ugaidi. 

Jengo hilo linawawezesha maafisa wasimamizi wa magereza kuwatenga wahalifu wanaosadikika kuwa hatari zaidi kuliko wengine na kuepusha itikadi kali kusambaa gerezani.Juhudi hizo zilifanikishwa na serikali ya Uingereza na ofisi ya UNODC.Kulingana na ripoti ya mkakati wa taifa wa kupambana na uhalifu na ukatili uliokithiri, KNSCVE, waliohukumiwa kwa makosa hayo na kufungwa huwalenga wenzawao wanyonge na kutumia hata dini kujiunga na kuwa wafuasi wao. 

Itikadi kali ndani ya magereza 

Ripoti hiyo inasema wafungwa hao walio na itikadi kali wanaweza kufanikiwa kwani wanaaminika ndani ya jela.Jee vipi ambavyo ofisi ya UNODC inachangia katika vita dhidi ya itikadi kali?.  

Charity Kagwi Ndungu ni mwakilishi wa UNODC na anaafiki kuwa udongo upatiliwe uli maji kwasababu,” Hawa maofisa, wakipata huo ushauri nasaha wataweza kuelewa, kinachowafanyikia wafungwa.Lazma uangalie kuwa sio tunawafunga tunawaadhibu, hapana. Tunajaribu kuwarekebisha na kuwarudisha kwenye laini tunayoitaka kama wakenya.Mtoto ama baba akiingia kwenye kitu kama misimamo mikali,huyo ni mtu ambaye yuko hatarini, ana shinda na ndio ameingia hapo.Lakini tukimleta hapa gerezani hatujawezesha hawa maafisa kuwaongelesha, kuwarekebisha kuwaonyesha wamekubalika na Kenya.” 

Jela ya Langata ya wanawake ndio ya kwanza kupokea kituo hiki cha kipekee cha kutoa ushauri nasaha kwa maafisa wa magereza wanaotatizwa na msongo wa mawazo. 

 

Taarifa hii imeandaliwa na Thelma Mwadzaya, mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa nchini Kenya