Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Buriani Yury Fedotov tutaenzi mchango wako :Guterres

Yury Fedotov aliyewahi kuwa mkuu wa UNODC akihojiwa na UN News enzi za uhai wake sasa amefariki dunia
UN News/Liz Scaffidi
Yury Fedotov aliyewahi kuwa mkuu wa UNODC akihojiwa na UN News enzi za uhai wake sasa amefariki dunia

Buriani Yury Fedotov tutaenzi mchango wako :Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema ameshtushwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha Yury Fedotov ambaye kwa muongo mmoja alihudumu kama mkurugenzi mkuu wa ofisi ya umoja wa Mataifa inayohusika na madawa na uhalifu UNODC.

Kupitia taarifa iliyoptolewa leo na msemaji wake kwa waandishi wa Habari mjini New York Marekani Antonio Guterres amesema wakati wa uhai wake kwa muda wote alipoiongoza ofisi ya UNODC bwana Fedotov alidhihirisha ujuzi wake na umakini katika kuzisaidia nchi wanachama kumaliza tofauti zao na kushirikiana katika mchakato wa moja ya masuala magumu nan yeti katika ajenda za kimataifa. Katibu Mkuu ameongeza kuwa mtazamo na mchango wake kama mshiriki kwenye kundio la utawala wa ngazi ya juu wa umoja wa Mataifa ulithaminiwa sana. Ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Fedotov na wapendwa wake wote huku akisema kuwa mchago wake, dhamira yake na kujitolea kwake kwenye Umoja wa Mataifa kuliteta mabadiliko na tija na daima mchango huo utaenziwa na kukumbukwa.