Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR: Mzozo wa Ukraine na mingineyo imepelekea watu milioni moja kukimbia makwao

Mwanamke kutoka Kramatorsk, eneo la Donetsk Ukraine Mashariki akichagua mavazi ya joto kwa ajili ya familia yake katika makazi ya muda Mukachevo, Magharibi Ukraine.o
© UNHCR/Igor Karpenko
Mwanamke kutoka Kramatorsk, eneo la Donetsk Ukraine Mashariki akichagua mavazi ya joto kwa ajili ya familia yake katika makazi ya muda Mukachevo, Magharibi Ukraine.o

UNHCR: Mzozo wa Ukraine na mingineyo imepelekea watu milioni moja kukimbia makwao

Wahamiaji na Wakimbizi

Idadi ya watu waliolazimika kukimbia migogoro, ghasia, ukiukwaji wa haki za binadamu na mateso sasa imevuka hatua ya kushangaza ya watu milioni 100 kwa mara ya kwanza kwenye rekodi, iliyochochewa na vita vya Ukraine na migogoro mingine inayosababisha maafa limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR

Kamishna Mkuu wa UNHCR Filippo Grandi akizungumzia takwimu hizo amesema, "Milioni mia moja ni takwimu ya kushangaza - ya kushtua na ya kutisha kwa kipimo sawa. Ni rekodi ambayo haikupaswa kuwekwa kamwe,” Ameongeza kwamba, "Hii lazima iwe kama mwito wa kusuluhisha na kuzuia mizozo haribifu, kukomesha mateso, na kushughulikia sababu zinazowalazimisha watu wasio na hatia kukimbia makazi yao."

Kwa mujibu wa takwimu mpya kutoka kwa UNHCR, idadi ya watu waliolazimika kukimbia makazi yao kote ulimwenguni iliongezeka hadi milioni 90 kufikia mwisho wa mwaka 2021, ikichochewa na mawimbi mapya ya ghasia au migogoro ya muda mrefu katika nchi zikiwemo Ethiopia, Burkina Faso, Myanmar, Nigeria. Afghanistan na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.  Halikadhalika, vita ya Ukraine imefurusha watu milioni 8 ndani ya nchi mwaka huu, na zaidi ya wakimbizi milioni 6 kutoka Ukraine wamesajiliwa.

Idadi ikiwa ni zaidi ya asilimia 1 ya idadi ya watu duniani, takwmu za jumla ni sawa na nchi ya 14 yenye watu wengi zaidi duniani. Inajumuisha wakimbizi na wasaka hifadhi pamoja na wakimbizi wa ndani milioni 53.2 waliokimbia makazi yao ndani ya mipaka yao kutokana na migogoro, kulingana na ripoti ya hivi majuzi kutoka Kituo cha Ufuatiliaji wa Wahamaji wa Ndani (IDMC).

Bwana Grandi amesema, "mwitikio wa kimataifa kwa watu wanaokimbia vita nchini Ukraine umekuwa mzuri," "Huruma iko hai na tunahitaji uhamasishaji sawa kwa majanga yote ulimwenguni. Lakini hatimaye, misaada ya kibinadamu ni kama dawa ya kupunguza makali lakini, si tiba. Ili kubadili mwelekeo huu, jibu pekee ni amani na utulivu ili watu wasio na hatia wasilazimishwe kuchagua kati ya hatari kubwa nyumbani au kukimbia kupitia safari hatarishi.”

UNHCR itatoa Ripoti yake ya kila mwaka ya Mwelekeo kimataifa tarehe 16 Juni, ikieleza takwimu  kamili za kimataifa, kikanda na kitaifa kuhusu watu waliolazimika kuhama makazi yao kwa mwaka wa 2021, pamoja na takwimu zaidi za hadi Aprili 2022, na maelezo kuhusu marejesho na masuluhisho.