Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO yasaidia wananchi wa Yemen kurejea kwenye ufugaji nyuki wa asili 

FAO ikisaidia wafugaji na mbinu za ufugaji nyuki.
©FAO/Jafaar Merie
FAO ikisaidia wafugaji na mbinu za ufugaji nyuki.

FAO yasaidia wananchi wa Yemen kurejea kwenye ufugaji nyuki wa asili 

Ukuaji wa Kiuchumi

Ikiwa leo ni Siku ya Nyuki Duniani na kaulimbiu ya mwaka huu ikisema, “Kama nyuki wanavyoshirikiana: Tusherehekee utofauti wa nyuki na ufugaji nyuki,” wafugaji wa nyuki nchini Yemen wanalishukuru Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO kwa kuwanyanyua tena baada ya kuwasaidia kurejea katika shughuli yao ya jadi ya ufugaji nyuki ambayo ni moja ya vyanzo vyao vya uchumi vilivyovurugwa na ukosefu wa amani nchini humo.

Hapa ni katika jimbo la Shabwah lililoko kusinimashariki mwa Yemen. Nyuki wanaonekana wakiingia na kutoka katika mzinga na wakati huohuo mwanaume mmoja anatoka katika nyumba yake tayari kwenda kulina asali.  

Asali ya Yemen inathaminiwa duniani kote na utamaduni wa nchi hiyo wa ufugaji nyuki umedumu kwa karne nyingi. Kuna hadi mashairi na nyimbo kadhaa duniani ambazo zimesifu ubora mwingi wa asali ya Yemen, lakini nyuki na wafugaji nyuki wa kienyeji wanatishiwa na changamoto zinazoongezeka kutokana na migogoro inayoendelea.  

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, zinasema takriban kaya laki moja (100,000) nchini Yemen zinategemea ufugaji nyuki kama chanzo kikuu ya mapato ya familia kuwawezesha kununua chakula, huduma za afya na mahitaji mengine ya lazima. 

Vita ilipozuka nchini humo na jimbo la Shabwah kugeuka uwanja wa vita, Salim Al-Diwali mwenye umri miaka 40 baba wa watoto saba akiwa ni mmoja wa wafugaji nyuki wengi, alipoteza mizinga yake ya nyuki na maisha kwake yalikuwa ni giza. 

(Nats) 

Bwana Al-Diwali anasema, “wakati wa vita, baadhi ya mizinga ya nyuki ilipigwa na mashambulizi ya anga, wafugaji wa nyuki waliacha mizinga yao katika maeneo yenye vita na ikaharibiwa kabisa.” 

Kwa kutambua umuhimu wa asali nchini Yemen, FAO ilipata ufadhili wa Benki ya Dunia na kuanzisha mradi wa miaka 3 uliotoa mafunzo na nyenzo za kilimo  na kuwawezesha wafuga nyuki mia saba kutoka majimbo 7 nchini humo ambao wamefanikiwa kuzalisha kila mmoja kilo 40 za asali kwa mwaka na hivyo kujipatia kipato cha uhakika kwa kuwa kilo moja wanauza kwa takriban dola 50 za kimarekani. 

Na sasa wafuganyuki kama Al-Diwali maisha yameanza kuwa na nuru kwa kuwa wana uhakika wa kuhudumia familia zao. 

(Nats) 

Anasema “Nyakati zangu za furaha ni pale ninapovuna asali nyingi, ninapoenda sokoni kuuza asali yangu, ninapopata pesa na kununua vitu kwa ajili ya watoto na familia yangu, na ninapokwenda sokoni kuuza asali yangu na kisha kuwa na akiba. Hizi ndizo nyakati za furaha zaidi kwa kuwa naona kwamba jitihada zangu zimezaa matunda.”