Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nyuki wameboresha maisha yangu na jamii yangu – Katobagula wa Kigoma, Tanzania 

Hija Katobagula ni mmoja kati ya wanufaika wa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa tija yaliyotolewa na wataalamu kutoka shirika la kimataifa la chakula na kilimo FAO.
UN NEWS/ John Kabambala
Hija Katobagula ni mmoja kati ya wanufaika wa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa tija yaliyotolewa na wataalamu kutoka shirika la kimataifa la chakula na kilimo FAO.

Nyuki wameboresha maisha yangu na jamii yangu – Katobagula wa Kigoma, Tanzania 

Ukuaji wa Kiuchumi

Leo ni Siku ya Nyuki Duniani, ambapo maadhimisho ya mwaka huu, shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO limekuwa na matukio mbalimbali japo kwa njia ya mtandao kupitia kaulimbiu ‘Nyuki wanavyoshirikiana: Tusherehekee aina mbalimbali za nyuki na mifumo ya ufugaji nyuki’. 

Ufugaji nyuki ni shughuli iliyoenea na ya kimataifa, huku mamilioni ya wafugaji nyuki wakitegemea nyuki kwa riziki na ustawi wao. Pamoja na kuwa wachavushaji wa porini, nyuki wana jukumu kubwa katika kudumisha bayonuai, kuhakikisha uhai na uzazi wa mimea mingi, kusaidia vizazi vya misitu, kukuza uendelevu na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuboresha wingi na ubora wa mazao ya kilimo. 

Nchini Tanzania, takribani miaka mitano iliyopita mashirika manne ya Umoja wa Mataifa likiwemo la Chakula na Kilimo FAO, la Mpango wa Chakula Duniani WFP, la maendeleo ya mitaji UNCDF na Kituo cha Biashara cha kimataifa ITC yalishirikiana kutekeleza mradi wa pamoja Mkoani Kigoma ujulikanao kama KJP na matunda ya mradi huo yanaendelea kuonekana.  

Hija Katobagula ni mmoja kati ya wanufaika wa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa tija yaliyotolewa na wataalamu kutoka shirika la kimataifa la chakula na kilimo FAO,
UN News/John Kabambala
Hija Katobagula ni mmoja kati ya wanufaika wa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa tija yaliyotolewa na wataalamu kutoka shirika la kimataifa la chakula na kilimo FAO,

Takribani umbali wa kilometa 18 hivi kutoka Kibondo mjini hadi katikati ya shamba lenye ukubwa wa zaidi ya heka elfu moja lililopo katika halmashauri ya Wilaya ya Kibondo Mkoani Kigoma mfugaji nyuki Hija Katobagula ni mmoja kati ya wanufaika wa mafunzo ya ufugaji nyuki kwa tija yaliyotolewa na wataalamu kutoka shirika la kimataifa la chakula na kilimo FAO, anasema kwa miaka mingi alikuwa sio Rafiki wa nyuki kwa sababu ya kumbukumbu ya namna alivyong’atwa na yuki alipokuwa mdogo lakini sasa amekuwa mtaalamu na anaona faida ya nyuki. 

“Katika ufugaji wa nyuki, kalenda ni kitu muhimu sana kwa sababu ukijua ni muda gani uweke mizinga, ni muda gani uende ukakague, tabia na maendeleo ya nyuki walioko kwenye mzinga wako, ni muda gani unatakiwa uende kuvuna, ni muda gani unatakiwa uende kuangalia soko. Na uvunaji ambao una tija. Kutokana na ambacho tumejifunza, ukiivuna vibaya inaleta madhara, inakuwa imeathirika ubora wake.” Anaeleza kitaalamu Bwana Katobagula.  

Ni hatua gani alizichukua baada ya kupata mafunzo hayo kutoka FAO? Anaeleza akisema kwamba baada ya kupata yale mafunzo ya FAO na kuelewa vizuri tasnia nzima ya nyuki, alihamasika akarundi nyumbani akachagua eneo la msitu mmojawapo akavuna mbao kwa ajili ya kutengeneza mizinga na bahati ni kuwa yale mafunzo yalikuwa yamehusisha mafundi wa mbao ambao walipewa mafunzo ya kutengeneza mizinga ya kisasa na hao ndio aliowatumia.   

“Mpaka sasa tuna mizinga 770 ambayo yote ni ya kisasa. Lakini pia katika yale mafunzo, tulijifunza pia ufugaji wa nyuki kwa kutumia nyumba ya nyuki ambapo tunatega nje mizinga kupata nyuki halafu tunawaweka katika hiyo nyumba wanaishi kwa raha mstarehe na kuzalisha vizuri.” 

Na je katika awamu ya kwanza baada ya kurengeneza mizinga na kuiweka kwenye maeneo husika, walipata mavuno kiasi gani? Bwana Katobagula anasema kwa kuanzia wamepata kilo mia sita za asali ambazo ni kiasi kidogo lakini kimewaletea fedha ambacho kimewasaidia angalau katika shughuli zingine za kilimo.   

Kuhusu faida nyingine ambazo wanazipata zaidi ya asali, Bwana Katobagula anasema, “kipindi cha nyuma, mti mmoja wa maembe tulikuwa tunaweza kupata maembe 50 mpaka 70 lakii sasa hivi mti mmoja unatoa maembe mpaka 150 na baada ya kufuatilia kiundani tumegundua uchavushaji wa mdudu nyuki, umeongeza kuchavusha yale maua na kutengeneza maua yaliyo bora.” 

Je jamii iliyomzunguka nayo imenufaikaje na elimu aliyoipata kutoka kwa mashirika ya Umoja wa Mataifa? Anasema baadhi ya wakazi majirani wa eneo la ufugaji nyuki wamemtembelea na kuja kupata ujuzi wa ufugaji nyuki.  

“Tumewafundisha, wameona kwa vitendo, mzinga unavyotengenezwa, unavyowekwa, na uzalishaji pia. Lakini pia jamii inayotuzunguka kupitia huyu mdudu nyuki ambaye anaenda kutafuta chakula huko kwenye misitu na mashamba yao, imesaidia kuongeza uchavushaji kwa maana ya mazao ya mahindi, maharagwe na matunda na mazao mengine yoyote ambayo yanatoa maua na hivyo kuongeza tija katika mazao yao.” Anahitimisha Bwana Katobagula.  

Kwa kuadhimisha Siku ya Nyuki Duniani kila mwaka, FAO inasema tunaweza kuongeza ufahamu kuhusu jukumu muhimu la nyuki na wadudu wachavushaji wengine katika kuwaweka watu na sayari wakiwa na afya, na kuhusu changamoto nyingi wanazokabiliana nazo leo.  

Ulimwengu umekuwa ukiadhimisha siku hii tangu mwaka 2018 ambapo juhudi za Serikali ya Slovenia kwa msaada wa Apimondia zilisababisha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutangaza Mei 20 kuwa Siku ya Nyuki Duniani. 

Tarehe ya madhimisho haya ya Siku ya Nyuki Duniani ilichaguliwa kwani ndiyo siku ambayo Anton Janša, mwanzilishi wa ufugaji wa kisasa wa nyuki, alizaliwa. Janša alitoka katika familia ya wafugaji nyuki huko Slovenia, ambapo ufugaji nyuki ni shughuli muhimu ya kilimo yenye utamaduni wa muda mrefu.