Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sanaa ya kufikirika yachangia ufanikishaji wa SDG

Harrieth C. Kwetkia kutoka Tanzania akichora moja ya kazi zake za sanaa za kufikirika.
UNIC/ Tanzania
Harrieth C. Kwetkia kutoka Tanzania akichora moja ya kazi zake za sanaa za kufikirika.

Sanaa ya kufikirika yachangia ufanikishaji wa SDG

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Nchini Tanzania kijana Harrieth C. Kwetukia ametumia kipaji chake cha uchoraji wa kufikirika ili kuchangia katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, SDGs ya Umoja wa Mataifa, SDGs au Ajenda 2030.

Kijana huyo licha ya kuwa mwajiriwa kwenye kampuni, hutumia muda wake wa kando kuchora picha hizo ambazo pamoja na kumwezesha kutimiza ari yake ya kusongesha kipaji hicho na kufundisha wengine, hujipatia pia kipato na hivyo kufanikisha lengo namba 1 la SDGs, kutokomeza umaskini.

Akiwa ni mkazi wa Dar es salaam, mji mkuu wa kibiashara wa Tanzania, Bi. Kwetukia amezungumza na Maria Kabora wa kituo cha habari cha Umoja wa Mataifa,  UNIC, Dar es salaam na kusema kuwa anatumia sanaa hiyo kuleta mabadiliko chanya kweney jamii yake tangu aanze mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 23.

Pamoja na lengo namba 1 la kutokomeza umaskini, Bi. Kwetukia anashiriki kutekeleza lengo namba 8 la ajira zenye staha na ukuaji wa uchumi.

“Mara nyingi picha ninazochora zina maana tofauti tofauti” amesema Bi. Kwetukia akizungumza na UNIC Dar es salaam.

Kazi ya sanaa ya mchoro wa kufikirika kutoka kwa kijana mtanzania, Harrieth C. Kwetukia.
UNIC Dar es salaam
Kazi ya sanaa ya mchoro wa kufikirika kutoka kwa kijana mtanzania, Harrieth C. Kwetukia.

Akionesha picha moja aliyochora, anasema “nimechora picha hii ikionesha msitu huku jua likizama. Hii ni zawadi kwa rafiki yangu, nikimshukuru kwa yeye kuweko kipindi ambacho katika maisha yangu niliona kama msitu mnene, hivyo yeye alikuwa kama jua kunifariji, kuniliwaza na kunipa tumaini kuwa maisha yanaendelea”. 

Alipata wapi mafunzo ya uchoraji?

Alijifunza shuleni, halikadhalika mtandaoni. Anasema haikuwa rahisi kwani aliwekeza muda wake mwingi kujifunza na kuwa tofauti na wengine ili kazi yake ivutie wateja siyo tu Tanzania bali hata nchi mbalimbali duniani.

Sanaa ya kufikirika na sanaa dhahiri
Akifafanua kuhusu tofauti wake, Bi.Kwetukia anasema ni uchoraji wa sanaa ya kufikirika.

“Utofauti wangu ni kwamba nafanya sanaa ya kufikirika ilhali watu wengi hufanya sanaa ya uhalisia kwamba mtu atachora mnyama kama vile nyani au simba ambaye anaonekana dhahiri. Na kama ni  binadamu basi atachora binadamu anayeonekana lakini mimi nafanya sanaa za kufikirika ambayo muda mwingine ni rangi tu na watu wakijihusisha na kazi yangu wanajua namaanisha nini,” amesema Bi. Kwetukia. 

Ujumbe kwa vijana wa kike

Kupitia kazi yake amekuwa chachu kwa vijana na watoto wanaomzunguka kwa kuwa ameweza kuwaonesha kuwa wanaweza.

“Nawaeleza wasichana na watoto wa kike kuwa hii kazi inaweza kufanywa na wanawake pia. Wasichana wadogo wanaoingia katika tasnia hii wana uwezo huo, hivyo nimewashawishi na kuwashauri jinsi gani ya kufanyakazi hii,” amesema Bi .Kwetukia.

Manufaa apatayo

Manufaa aonayo ni pamoja na kuwa rafiki wa dunia, “kwa kutumia Sanaa yangu kuelimisha wananchi juu ya kuhifadhi mazingira. Natumia Sanaa kuelezea vitu hatarishi kwa mazingira.”

Halikadhalika anasema amepanuka kiaikili kutokana na watu anaokutana nao na kushirikiana nao katika kuelimisha jamii kuhusu mwelekeo wa dunia kiuchoraji.

“Tatu ni kipato, kupitia kazi hii nauza nah ii imekuwa ni mchango mkubwa na zaidi ya yote ni kukutana na watu kutoka mataifa mengine.”

Penye manufaa hapakosi changamoto

Bi. Kwetukia anasema changamoto ni nyingi lakini amechagua kusonga mbele na ana imani atafika malengo lakini pia hafikiri kuacha kufanya sanaa ya uchoraji kwani anajiona kuendelea kuifanya hata kama anajishughulisha na kazi yake ya kitaaluma.