Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Colombo, Mji Mkuu wa Sri Lanka

Hali mbaya ya kiuchumi Sri Lanka: Bachelet anahimiza mazungumzo ili vurugu zisiongezeka

Unsplash/Jalitha Hewage
Colombo, Mji Mkuu wa Sri Lanka

Hali mbaya ya kiuchumi Sri Lanka: Bachelet anahimiza mazungumzo ili vurugu zisiongezeka

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu Michelle Bachelet ametoa wito kwa mamlaka nchini Sri Lanka kuzuia ghasia zaidi na kushiriki mazungumzo ya kushughulikia malalamiko ya wananchi kufuatia mzozo mkubwa wa kiuchumi nchini humo.

Taarifa kutoka Geneva Uswisi imemnukuu Bachelet akieleza kusikitishwa na kuongezeka kwa ghasia nchini humo baada ya wafuasi wa Waziri Mkuu kuwashambulia watu waliokuwa wanaandamana kwa amani huko Colombo tarehe 9 Mei 2022 na ghasia zilizofuata za umati dhidi ya wanachama wa chama tawala.

Watu 7 wamekufa wakati wa matukio hayo ikiwa ni pamoja na Mbunge na viongozi wawili wa eneo hilo, zaidi ya 250 walijeruhiwa, na mali za wengine kuharibiwa kwa kuchomwa moto nchini kote.

“Nalaani vurugu zote na natoa wito kwa mamlaka kuchunguza kwa uhuru, kwa kina na kwa uwazi mashambulizi yote ambayo yametokea. Ni muhimu kuhakikisha kwamba wale wanaopatikana na hatia, ikiwa ni pamoja na wale wanaochochea au kuandaa vurugu, wanachukuliwa hatua.”

Serikali zuieni vurugu

Kamishna huyo wa umoja wa Mataifa ameitaka mamlaka nchini Sri Lanka kuhakikisha wanadhibiti kutokea tena kwa vurugu na kulinda wanaofanya maandamano ya amani. 

“Mamlaka ikiwemo maafisa wa kijeshi wanaopewa jukumu la kusaidia vikosi vya usalama, wanapaswa kujizuia wakati wakitekeleza majaukumu yao ya kipolisi na kuhakikisha hatua zinazochukuliwa katika muktadha wa hali ya hatari zinazingatia kanuni za kimataifa za haki za binadamu na hazitumiwi kuzuia upinzani au kuzuia maandamano ya amani,” alisisitiza Bachelet.

Rafu zikiwa tupu kwenye maduka makubwa huko Colombo, Sri Lanka. (Maktaba)
© ADB/M.A. Pushpa Kumara
Rafu zikiwa tupu kwenye maduka makubwa huko Colombo, Sri Lanka. (Maktaba)

Jumuisheni makundi yote kwenye mazungumzo

Serikali ina wajibu wa kuhakikisha haki ya kuishi na kufanya bidii ili kulinda maisha ya watu dhidi ya unyanyasaji unaofanywa na watu binafsi au taasisi.

Mgogoro mkubwa wa kiuchumi umefanya maisha ya kila siku kuwa magumu kwa watu wengi wa Sri Lanka. Bachelet amehimiza mazungumzo ya kitaifa na mageuzi ya kina ya kimuundo ambayo yatawaleta pamoja watu wa makabila na dini mbalimbali ili kudai uwazi zaidi, uwajibikaji na ushiriki katika maisha ya kidemokrasia.

“Ninaiomba Serikali ya Sri Lanka kushiriki katika mazungumzo ya kina na sehemu zote za jamii ili kutafuta njia ya kusonga mbele na kushughulikia changamoto za kijamii na kiuchumi ambazo watu, haswa makundi yaliyo hatarini na yaliyotengwa, wanakabiliana nayo. Natoa wito kwa Serikali kushughulikia masuala ya msingi ya kisiasa na kimfumo ambayo kwa muda mrefu yameendeleza ubaguzi na kudhoofisha haki za binadamu.”

Bachelet alisema Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa itaendelea kuangalia kwa karibu na kutoa taarifa kuhusu hali ilivyo nchini humo huku akionesha matumaini kwamba Sri Lanka itapata suluhisho la amani kwa mzozo uliopo ili kupunguza mateso ya watu, kuimarisha demokrasia na haki za binadamu, na kuzuia ghasia zaidi.