Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Azimio lapitishwa kuchochea kasi ya kusaidia wakimbizi wa CAR 

Wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wanarejea nyumbani kutoka kambi jimbo la  Ubangi nchini DRC.
© UNHCR/Alexis Huguet
Wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati wanarejea nyumbani kutoka kambi jimbo la Ubangi nchini DRC.

Azimio lapitishwa kuchochea kasi ya kusaidia wakimbizi wa CAR 

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR na serikali za  mataifa ya Afrika ya Kati wamepitisha azimio jipya linalotoa wito wa kuchukuliwa hatua zaidi kusaidia wakimbizi zaidi ya milioni 1.4 waliofurushwa kutokana na mzozo wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na UNHCR huko Yaounde, mji mkuu wa Cameroon, azimio hilo limetiwa saini mjini humo baada ya mkutano wa siku tatu wa ngazi ya  mawaziri,  mkutano uliohudhuriwa pia na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi. 

Akizungumza kwenye mkutano huo, Bwana Grandi amesema , “lengo la mkutano huo lilikuwa kusaka kasi mpya ya suluhu kwa wakimbizi kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati. Hii lazima itekelezwe kwa ushirikiano na serikali, jamii zinazotoa misaada, sekta ya biashara, wadau wa maendeleo, mashirika ya kiraia, sekta binafsi na wakimbizi wenyewe, hususan wanawake.” 

Wakimbizi wa CAR wako wapi? 

Tangu mwaka 2013, CAR imegubikwa na majanga mfululizo yakiathiri mataifa sita ambayo hadi leo yanahifadhi takribani wakimbizi 700,000. 

Cameroon imepokea idadi kubwa zaidi ambayo ni 345,000 ikifuatiwa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wakimbizi 212,000, Chad wakimbizi 119,000, Jamhuri ya Congo wakimbizi 29,000, Sudan inahifadhi wakimbizi 28,000 ilhali Sudan Kusini 2,500. 

Waziri Mkuu wa Cameroon Joseph Dion Ngute akizungumzia changamoto wanazombana nazo kuhifadhi wakimbizi amesema, “licha ya juhudi zinazochukuliwa na serikali, bado kiuchumi hali ni ngumu. Kuna umuhimu wa kuimarisha juhudi za kikanda kuainisha majawabu ya kimataifa na juhudi zetu ili tupate matokeo mazuri.” 

Kipi kitafanyika? 

Kupitia azimio hilo, UNHCR na mataifa hayo yanahohifadhi wakimbizi wa CAR wamekubaliana kwa msaada wa jamii ya kimataifa kuanzisha mfumo wa ushirikiano wa kikanda kuimarisha ulinzi na kusaka majawabu kwa raia waliokimbia CAR. 

Wakirejelea makubaliano ya amani ya mwaka 2019, ambayo wakimbizi na wasaka hifadhi walishiriki, pande husika kwenye azimio la sasa zimekubaliana kusaidia maridhiano yanayoendelea CAR sambamba na kuendelea kuwalinda wakimbizi na kusongesha ujumuishaji wa kiuchumi na kijamii wakati wakimbizi hao wanasubiri mazingira bora ya kuwawezesha kurejea nyumbani. 

Mazingira bora ni pamoja na kuondoa vikwazo vya kisheria kwenye fursa za kazi, mafunzo na kuweza kupata huduma za kijamii. 

Licha ya changamoto raia wa CAR wanarejea nyumbani 

Taarifa hiyo imesema licha ya changamoto, bado fursa za kurejea CAR ziko kwa kuwa, “zaidi ya wakimbizi 100,000 wamerejea nyumbani.” 

Kati ya 2017 na 2022, UNHCR imefanikisha kurejea nyumbani kwa hiari kutoka ugenini kwa wakimbizi 27,000 nchini CAR. Wakimbizi wengine wa ndani 27,000 nao wamerejea nyumbani. 

Sisi ni wawezeshaji maendeleo na si mzigo- Mkimbizi 

Kabla ya kushiriki kwenye mkutano huo, Kamishna Mkuu Grandi alikutana na wakimbizi wa ndani CAR huko Yaounde ambao wameshukuru hatua za kushughulikia changamoto zinazowakabili. 

Kiongozi wa kijamii wa wakimbizi hao alimweleza Bwana Grandi kuwa “wakimbizi tunataka tuonekane kama wawezeshaji wa maendeleo na si mzigo.”