Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaongeza nguvu kujipanga dhidi ya COVID-19 katika kambi ya wakimbizi kanda ya Afrika Mashariki na pembe ya Afrika

Kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini Magharibi mwa Kenyal.
OCHA/Gabriella Waaijman
Kambi ya wakimbizi ya Kakuma Kaskazini Magharibi mwa Kenyal.

UNHCR yaongeza nguvu kujipanga dhidi ya COVID-19 katika kambi ya wakimbizi kanda ya Afrika Mashariki na pembe ya Afrika

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, kupitia msemaji wake Babar Baloch limesema linaongeza juhudi za kuongeza uwezo wa kuzuia, kutibu na kuzuia uwezekano wa kuenea kwa COVID-19 miongoni mwa jamii katika eneo la Afrika Mashariki, pembe ya afrika na maziwa makuu ambako ni moja ya maeneo yanayowahifadhi wakimbizi wengi zaidi duniani. 

Bwana Baloch akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hii leo amesema kuishi katika maeneo yenye msongamano wa watu bila maji safi na salama na pia vifaa vya kujisafi na hali ya kuishi katika hali mbaya na usalama mdogo, wakimbizi katika ukanda huo wako hatarini kukumbwa na virusi vya corona, katika kambi za wakimbizi na hata katika maeneo ya mijini.

“Kufuatia kuthibitishwa kwa mgonjwa wa kwanza wa COVID-19 nchini Sudan Kusini na Eritrea wiki iliyopita, nchi zote katika ukanda huo hivi sasa ziko katika mapambano dhidi ya mlipuko huo wa virusi. Ingawa hadi kufikia hivi sasa hakujakuwa na kisa kilichothibitishwa miongoni mwa wakimbizi, wasaka hifadhi na wakimbizi wa ndani katika ukanda, kujiandaa ni suala la muhimu sana.” Amesema Bwana Baloch.

Mlipuko wa virusi vya corona unakuja katika hali ya dharura ambayo tayari imeshakuwepo katika ukanda huo, ambako asilimia sitini ya wakimbizi wanakabiliwa na punguzo la mgao wa chakula kutokana na ukosefu wa ufadhili. 

Aidha mlipuko huo una matokeo mabaya kwa wakimbizi ambapo pamoja na kufungwa kwa mipaka, pia wakimbizi wamejikuta katika hali ya kutoweza kukuza kipato chao kwani wameshuhudia maeneo yao ya kazi na biashara yakifungwa. Wale wanaotegemea biashara za kuvuka mipaka wameathirika zaidi.

UNHCR inatoa wito kwa serikali kuhakikisha wakimbizi wanajumuishwa katika mipango ya dharura ya ulinzi wa jamii wakati ikifuatilia uwezekano wa kuwapatia wale walioko hatarini msaada wa fedha ili waweze kupata mahitaji yao ya msingi.” Amesema msemaji wa UNHCR.

Katika moja ya miradi ya kusaidia wakimbizi, UNHCR inasaidiana na serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali katika masomo kwa njia ya masafa na pia programu za kidijitali nchini Kenya, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda. 

Nchini Djibouti zaidi ya wakimbizi 4,500 na wasaka hifadhi walipatiwatiwa makazi mapya ili kupunguza msongamano na pia kuweka nafasi ya kutokaribiana katika vijiji vya Ali Addeh na Holl-holl. 

Huko Ethiopia, usambazaji wa maji na sabuni vimeongezwa na pia vituo vya kunawa mikono vinawekwa ikiwemo vituo 127 katika maeneo ya kijamii na zaidi ya vituo 14,700 katika kambi ya wakimbizi ya Gambella. 

Nchini Kenya, Somalia, Sudan, Tanzania na Uganda kote UNHCR imefanya juhudi za kupambana na virusi vya corona katika kambi za wakimbizi.

Nchi zote katika ukanda ambazo zimeweka hatua za kuzuia mizunguko n ahata kufunga mipaka ikiwemo kuweka zuio la kutembea, UNHCR inazisihi, miongoni mwazo zikiwa ni zile ambazo zimekuwa mwenyeji wa wakimbizi kwa miongo kadhaa, kuendelea kuwapatia ulinzi na hifadhi watu wanaokimbia vita na ukatili katika kipindi hiki cha changamoto. 

Ofisi ya UNHCR kanda ya Afrika Mashariki, pembe ya Afrika na maziwa makuu inahudumia nchi 11 ambazo ni Burundi, Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania na Uganda.