Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR imetoa ombi la dola bilioni 1.85 kwa ajili ya wakimbizi wa Ukraine

Kijiji cha Novoselivka karibu na Chernihiv na Ukraine kimeshambuliwa kufuatia mzozo na Uruisi.
UNDP Ukraine/Oleksandr Ratushnia
Kijiji cha Novoselivka karibu na Chernihiv na Ukraine kimeshambuliwa kufuatia mzozo na Uruisi.

UNHCR imetoa ombi la dola bilioni 1.85 kwa ajili ya wakimbizi wa Ukraine

Wahamiaji na Wakimbizi

Katika kukabiliana na janga la wakimbizi wa Ukraine linaloongezeka kila uchao, UNHCR, Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, na washirika wa misaada ya kibinadamu wanaomba msaada wa kifedha zaidi ili kuwasaidia wakimbizi hao na nchi jirani zinazowahifadhi kwa ukarimu.

Likizindua mpango mpya wa Kikanda wa kukabiliana na changamoto ya wakimbizi (RRRP) kwa ajili ya hali inayoendelea nchini Ukraine, shirika la UNHCR na washirika wanasaka dola za bilioni 1.85 ili kuweza kusaidia wakimbizi milioni 8.3 wanaotarajiwa katika nchi jirani, ambazo ni Hungary, Jamhuri ya Moldova, Poland, Romania na Slovakia, pamoja na nchi nyingine katika kanda hiyo, ikiwemo Belarus, Bulgaria na Jamhuri ya Czech.

Ombi hilo la fedha limezinduliwa wakati kunaendelea mapigano, uharibifu na na maelfu ya watu wakilazimika kutawanywa ndani ya Ukraine.

Kwa mujibu wa UNHCR hadi sasa, vita hivyo vimewatawanya zaidi ya watu milioni 12.7 katika kipindi cha miezi miwili pekee ambapo zaidi ya milioni 5 wamefungasha virago na kuwa wakimbizi nje ya mipaka ya taifa lao na wengine milioni 7.7 wamesalia kuwa wakimbizi ndani ya nchi.

Takriban watu milioni 13 zaidi pia wanakadiriwa kukwama katika maeneo yaliyoathiriwa au hawawezi kuondoka kwa sababu ya hatari za usalama.