Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwezi mtukufu wagubikwa na mauaji na mashambulizi Mashariki ya Kati  

Kituo cha Qalandia kati ya Mashariki mwa Jerusalem na Ramallah ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan.
UN News/Shirin Yaseen
Kituo cha Qalandia kati ya Mashariki mwa Jerusalem na Ramallah ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan.

Mwezi mtukufu wagubikwa na mauaji na mashambulizi Mashariki ya Kati  

Amani na Usalama

Mratibu Maalum wa Umoja wa Mataifa huko Mashariki ya Kati Tor Wennesland, amelijulisha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hii leo kuwa eneo la Yerusalem Mashariki lililoko Ukingo wa Magharibi mwa mto Jordan ambalo linakaliwa na Israel liligubikwa na ghasia kubwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita sambamba na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya Israel.

Akihutubia Baraza la Usalama lililokutana leo jijini New York, Marekani kujadili amani Mashariki ya Kati ikiwemo hoja ya Palestina, Bwana Wennesland amesema, “raia kadhaa wameuawa na wengine wamejeruhiwa katika matukio hayo wakati kipindi hicho cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani huku wakristo nao na wayahudi wakiadhimisha sikukuu ya Pasaka.” 

Amesema alitumai kuwa kipindi hicho kitakuwa cha amani lakini hilo halikutokea. 

Vifo na Majeruhi 

Katika eneo linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan na Israel, wapalestina 23 wakiwemo wanawake 3 na watoto 4 waliuawa na jeshi la Israel wakati wa maandamano na wapalestina 541 walijeruhiwa. 

Waisrael 12 wakiwemo wanawake 2 na raia 3 wa kigeni waliuawa huku wengine 82 walijeruhiwa na wapalestina kwa kupigwa risasi, kuchomwa visu au kurushiwa mawe. “Kwa ujumla, wapalestina walitekeleza mashambulizi 144 dhidi ya raia wa Israel. 

Maeneo matakatifu 

Katika maeneo matakatifu huko Yerusalem, hali ya usalama imekuwa tulivu kidogo licha ya mapigano na kauli za chuki kati ya vikosi vya Palestina na vile vya Israeli. 

Huko Ukanda wa Gaza, urushaji wa makombora kutoka upande wa Palestina umedidimiza utulivu kiasi uliokuweko tangu mwezi Mei mwaka jana. 

“Baada ya miezi kadhaa bila shambulizi la maroketi, wanamgambo Gaza walirusha makombota Matano kuelekea Israel, ambapo moja lilitua kwenye mji wa Sderot nchini Israel. Katika kujibu mashambulizi, jeshi la Israel lilifanya mashambulizi kutoka angani dhidi ya kile inachodai kulenga maeneo ya wanamgambo wa Hamas huko  ukanda wa Gaza, na hakukuweko na majeruhi wowote walioripotiwa,” amesema mratibu huyo. 

Hakuna kihalalishacho mashambulizi dhidi ya raia 

“Hebu nieleweke, hakuna uhalalishaji wowote wa vitendo vya kigaidi au ghasia dhidi ya raia. Ghasia na uchochezi lazima vikome mara moja na vilaaniwe na pande zote,” amesema Bwana Wennesland huku akisisitiza kuwa viongozi wa kisiasa, kidini na kijmaii katika pande zote lazima watekeleze wajibu waoe wa kupungua ghasia, wasimamie  hali inavyopaswa kuwa katika maeneo matakatifu na kuhakikisha yanaheshimiwa na pande zote. 

Kwa Bwana Wennesland, ghasia na kuongezeka kwa mvutano katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita, ni dhihirisho lingine ya kwamba juhudi za kusimamia mizozo si mbadala wa maendeleo halisi ya kutatua mzozo husika. 

Amesema jamii ya kimataifa lazima ifanya kazi kupunguza mvutano na kusongesha utulivu na wakati huo huo juhudi za pamoja zinahitajika kutatua vichocheo vya mzozo. 

Mathalani anachoamini ni kwamba kupunguza ghasia na kusitisha shughuli za ujenzi wa makazi ya walowezi kwenye maeneo ya wapalestina sambamba na kuimarisha uwezo wa kipato wa mamlaka ya Palestina na taasisi zake ni mambo muhimu. 

Kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali Mashariki ya Kati ikiwemo suala la Palestina.
UN Photo/Mark Garten
Kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali Mashariki ya Kati ikiwemo suala la Palestina.

Kauli ya Palestina barazani 

Akihutubia Baraza, Mwakilishi wa Kudumu wa Palestina ambayo ina hadhi ya utazamaji  kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Riyad Mansour, amesema “Israel inaamini kuwa jamii ya kimataifa itasahau kuwa Yerusalem Mashariki inakaliwa na imemegwa kinyume cha sheria kwa mujibu wa Chata ya  Umoja wa Mataifa.” 

Kwa mujibu wa Balozi Mansour, Israel haina haki ya madai au mamlaka dhidi ya eneo lolote lnialokaliwa la Palestina ikiwemo Yerusalem Mashariki. 

Israel yageukia Iran  

Mwakilishi wa Kudumu wa Israel kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Gilad Erdan, akijibu hoja akalieleza Baraza la Usalama kuwa “Iran ambayo ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa inatishia kutokomeza taifa la Israel na itakuwa na madini ya kutosha ya Uranium ili kutengeneza bomu la nyuklia katika wiki chache.” 

Amehoji inawezekana vipi kwa chombo kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambacho kimakasimiwa jukumu la usalama duniani hakiwezi kuamua kwa kura nyingi juu ya mjadala wa Mashariki ya Kati kuhusu tishio la nyuklia kutoka Iran. 

“Je kuzuia waislamu wenye msimamo mkali kupata silaha za maangamizi si kipaumbele cha juu cha Baraza hili?” amehoji Balozi Erdan. 

Balozi Erdan pia ameomba wajumbe wa Baraza kufikiria jinsi ambavyo Mashariki ya Kati itaonekana iwapo washirika wa mbali wa Iran wanaweza kutekeleza mambo yao kwa kisingizio cha nyuklia.