Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna kinachohalalisha mashambulizi dhidi ya raia katika machafuko ya sasa kati ya Israel na Palestina:Mladenov

Mtoto wa umri wa miaka 12 akipita pembezoni mwa nyumba iliyobomolewa na mashambulizi kutoka angani yaliyofanywa na Israeli katika jiji la Rafah, kusini mwa Gaza .
UNICEF/Eyad El Baba

Amani na Usalama

Machafuko makubwa yanayoendelea hivi sasa baina ya kundi la Kipalestina la Islamic Jihad na Israel yanatia wasiwasi mkubwa kufuatia mauaji ya kupanga ya kiongozi mmoja wa kundi hilo ndani ya Gaza Jana Jumanne.

Onyo hilo limetolewa leo na mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati Nickolay Mladenov .

Na kuongeza kuwa “Uvurumushaji wa maroketi na makombora katika vituo vya makazi ya raia ni suala lisilokubalika asiliani na ni lazima hali hiyo ikome mara moja. Hakutakuwa na sababu yoyote ya kuhalalisha mashambulizi ya aina yoyote dhidi ya raia.”

Bwana Mladenov amesema kuendelea kwa machafuko ni hatari kubwa na hilo ni jaribio lingine la kutaka kuvuruga juhudi za kuboresha hali ya kiuchumi na kijamii katika eneo la Gaza na kuzua vita nyingine mbaya.

Amesisitiza kuwa hivi sasa Umoja wa Mataifa unafanya kila uwezalo haraka ili kuzuia kuendelea kwa machafuko hayo ambayo yanawabebesha gharama kubwa ya maisha yao raia wasio na hatia.

Kwa mujibu wa duru za habari takriban Wapalestina 23 wameuawa hadi sasa na wengine wengi kujeruhiwa huku kwa upande wa Israel watu wapatao 50 wamejeruhiwa na idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka.