Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heko serikali ya Sudan na waasi kwa kutia saini makubaliano ya amani- UN

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Pakistani wakizungumza na wananchi wa Darfur Kaskazini nchini Sudan.
UNAMID
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Pakistani wakizungumza na wananchi wa Darfur Kaskazini nchini Sudan.

Heko serikali ya Sudan na waasi kwa kutia saini makubaliano ya amani- UN

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres amesema kitendo cha serikali ya mpito na waasi nchini Sudan kutia saini mkataba wa amani kinaashiria mwanzo wa zama mpya kwa wananchi wa taifa hilo.
 

Mkataba huo wa amani, ukipatiwa jina la Mkataba wa amani wa Juba, umetiwa saini leo kwa lengo la kutatua mzozo wa wenyewe kwa wenyewe ambao umesababisha mamia ya maelfu ya watu kupoteza maisha huku mamilioni wakiwa wakimbizi ndani na nje ya nchi yao.

Kupitia ujumbe wake wa video, Bwana Guterres amesema hatua ya leo ni ya kihistoria na ni mwelekeo wa kupata amani endelevu na maendeleo jumuishi.

“Napongeza pande zilizotia saini mkataba huo kwa kushirikiana kwa lengo moja la amani, licha ya changamoto zitokanazo na janga la Corona au COVID-19,” amesema Katibu Mkuu Guterres.

Halikadhalika amepongeza serikali ya Sudan Kusini kwa dhima yake ya kuratibu na kuwezesha mashauriano hayo wakati huu wenye changamoto nyingi.

“Sherehe ya leo ina maana zaidi kwa wnanachi wa Darfur kwa kuwapatia matumaini mapya na mustakabali wenye ustawi na amani zaidi. Umoja wa Mataifa umekuwa unajivunia kusaidia mwelekeo wa mazungumzo wa Darfur kupitia ujumbe wake wa pamoja na Muungano wa Afrika, huko Darfur, UNAMID,” amesema Guterres.

Guterres amesema jambo muhimu sasa ni mkataba huo utafsiriwe katika vitendo ili ulete maisha bora kwa wananchi, “na tunavyoangalia mbele, tunafahamu kuwa kufanikisha amani jumuishi, ya dhati nchini kote lazima pande zote ziwe kwenye meza ya mazungumzo.

Wanawake waliotawanywa kutoka katika eneo la Jebel Marra Darfur wakiwa wamesimama pembezoni mwa makazi ya muda katika eneo la Tawilla, Darfur Kaskazini.
OCHA/Amy Martin
Wanawake waliotawanywa kutoka katika eneo la Jebel Marra Darfur wakiwa wamesimama pembezoni mwa makazi ya muda katika eneo la Tawilla, Darfur Kaskazini.

Ametoa wito kwa chama cha Sudan People Liberation Movement-Kaskazini kinachoongozwa na Abdelaziz Al-Hilu kushiriki kikamilifu kwenye mashauriano, kwa kukubali fursa ya sasa ya kutiwa saini kwa hivi karibuni kwa makubaliano ya amani sambamba na Waziri Mkuu Hamdok mjini  Addis Ababa nchini Ethiopia.

Halikadhalika ametoa wito kwa kundi la Sudan Liberation Army la kwake  Abdul Wahid Al-Nur kujiunga mara moja na mchakato wa amani.

Amekumbusha kuwa ili mkataba huo utekelezwe kwa mafanikio, kinachohitajika ni azma ya dhati na ushirikiano wa pande zote kwa ajili ya ustawi wa wananchi wa Sudan.
Amesema kuwa Umoja wa Mataifa kwa upande wake uko tayari kusaidia safari hii ya kihistoria kuelekea kwenye amani.

Kutiwa saini hii leo kwenye mji mkuu wa Sudan Kusni, Juba, kunakuja baada ya mwaka mzima wa mazungumzo ya amani na kumeshuhudiwa na wadhamini ambao ni Chad, Qatar, Misri, Muungano wa Afrika, Muungano wa Ulaya na Umoja wa Mataifa.