UNAMID yakabidhi kambi ya Khor Abeche Darfur kwa serikali ya Sudan 

19 Februari 2021

Hatimaye kambi ya Khor Abeche iliyokuwa inatumiwa na walinda amani ujumbe wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika jimboni Darfur, UNAMID imekabidhiwa rasmi kwa serikali ya Sudan kufuatia kukamilika kwa majukumu ya ulinzi wa aman jimboni humo. 

Kambini Khor Abeche, jimboni Darfur nchini Sudan, bendera za Umoja wa Mataifa, Muungano wa Afrika na ile ya Tanzania , zilishushwa kuashiria kutamatishwa kwa shughuli zao, huku ile ya Sudan ikipandishwa kuashiria sasa eneo hili liko chini ya Sudan baada ya UNAMID kufunga virago na jukumu la ulinzi kusalia kwa serikali. 

Bendera zilikabidhiwa kwa Houston Ferguson  ambaye ni mkurugenzi wa utawala wa UNAMID. UNAMID imekuwepo Darfur tangu mwezi Oktoba mwaka 2007 na azimio la Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa la mwaka jana lilitamatisha rasmi shughuli za ujumbe huo tarehe 31 Desemba 2020. 

Shughuli ya kukabidhi bendera ilitanguliwa na ziara ya Bwana Ferguson katika kijiji cha Khor Abeche akiwa ameambatana na watendaji kutoka wa UNAMID na kuonesha kuridhishwa na hali ya usalama na utulivu katika eneo hilo. 

Akizungumza na wakazi wa Khor Abeche na viongozi wao  kupitia mkalimani, Bwana Ferguson amesisitiza kuwa UNAMID inaondoka eneo hilo, na hivyo wakazi wa Khor Abeche wailinde amani iliyopo. 

Bwana Ferguson amesema, “hii ni siku ya furaha sana kwa UNAMID na Umoja wa Mataifa. Tunaondoka na tunajivunia sana kile tulichofanikisha hapa Khor Abache. Ni wakati wa kurejea nyumbani na wakati wa wenyeji kutumia vyema kile tulichoacha hapa. Natamani kuwa mwanafunzi wa kwanza kuandikishwa katika kituo cha Ufundi Stadi ingawa mimi ni mwanafunzi wa kujifunza pole pole. Nashukuru pia kwa walinda amani wa Tanzania ambao wamejenga uhusiano mzuri na wa kipekee na wenyeji wa hapa.” 

Luteni Kanali Khalfani Rashidi Kayage, kamanda wa kikosi cha TANZBATT - 13 Luteni Kanali Khalfani Rashidi Kayage amewashukuru wakazi wa Khor Abeche,  viongozi wa serikali ya Sudan na uongozi wa UNAMID kwa kutoa ushirikiano kwa kipindi chote walinda amani kutoka Tanzania walipokuwa wanatekeleza majukumu ya ulinzi wa amani katika eneo hilo.
Luteni Kanali Kayage akizungumzia kufunga kambi amesema, “leo ni siku moja muhimu sana ambayo tumeshiriki ufungaji wa Team site ya Khor Abeche ambayo tulikuwa tukitekeleza majukumu yetu hapa tangu TANZBATT - 1 hadi sasa TANZBATT - 13. Tunashukuru tumeweza kutimiza jukumu letu la kuhakikisha kwamba tumeweza kuilinda kambi hii na ikaweza kukabidhiwa kwa salama na amani kwa serikali ya Sudan. Sasa hivi tunajiandaa kuondoka maeneo haya kuelekea MINAWASHI ambako nayo tunategemea itafungwa tarehe 25 mwezi huu. Sisi tunajivunia kwamba tunaondoka tumejifunza mengi kutoka kwao, tutakuwa mabalozi wema kwao. Tunamuomba mwenyezi Mungu atutangulie safari yetu kuelekea MINAWASHI Team Site.” 

UNAMID yakabidhi kambi ya Khor Abeche Darfur kwa serikali ya Sudan
UNAMID
UNAMID yakabidhi kambi ya Khor Abeche Darfur kwa serikali ya Sudan

Msimamizi na mratibu wa ufungaji wa kambi ya Khor Abeche ni Alex Mutuli hakuficha hisia zake akisema  “tumekuwa tukishirikiana na Luteni Kanali Kayage kamanda wa TANZBATT_13, ametusaidia sana kuhakikisha kambi ina amani na wale wenye mrengo wa kupigana nasi ili kuzuia amani tunawatuliza, viongozi wa ngazi zote tumewekuwa tunashirikiana kila siku. Luteni Kanali Kayage amefanya kazi kubwa na ameweza kutimiza kwamba kuna amani, tunaondoka huku kuna amani na wanatakiwa washikilie hapo kwa kuwa ikizoroteka wameumia.” 

Vijana wa kijiji cha Khor Abeche walikuwa na mwakilishi wao katika hafla hii ambaye ni Ali Ahmed Ali. 

Bwana Ali amesema "leo ni siku ya mwisho ya kufunga kambi ya Khor Abeche. Hii Team site ilikuwa chini ya uangalizi kuanzia TANZBATT - 1 hadi sasa TANZBATT_13. Kile walichofanya kwa jamii ya Khor Abeche na wakazi wote ambapo kwa kiswahili wanasema kijijini, kijiji cha kalaka, kijiji cha Nigeha, kijiji cha Karbab, Tirban, Khor abeche, watanzania walijenga madrasa katika kijiji cha Khor Abeche na pia walijenga shule katika kijiji cha Kalaka. TANZBATT 13 wamesaidia vitu vingi, nashukuru sana TANZBATT- 13 kwa walichofanya Khor Abeche na vyote walivyofanya ni kwa ajili ya raia wote wa Sudan na Serikali ya Sudan  hivyo  nawashukuru sana Watanzania"  

Wahenga walinena mwenda kwao si mtoro na ndivyo ilivyo kwa Koplo Mashauri Labani Rugina, mlinda wa TANZBATT  13 ambaye anaeleza ushiriki wake katika jukumu walilokamilisha. 

"Nimefurahi sana na nimepata heshima kubwa kuiwakilisha nchi yangu katika nchi ya Sudan nikiwa kama mlinda amani na nimejifunza mambo mengi katika utendaji kivita, lakini pia nimejifunza mambo mengi katika utendaji wa kiutawal. Kwa hiyo nimekuwa na uzoefu mkubwa  na majukumu yaliyokuwepo mengi ni ya utendaji kivita kwa sababu huku kazi yetu kubwa ni kuwalinda raia wananchi pamoja na kulinda mali za UN. Nimeshiriki katika mambo ya kiutawala, pia nimeshiriki katika doria ndefu na doria fupi ambazo tulizifanya na kufanikiwa kwa kiwango kikubwa.” 

Halikadhalika amezungumzia yale muhimu waliyofanya ikiwemo kulipia karo wanafunzi wa shule sambamba na kujenga madrasa. 

Kambi ya Khor Abeche ni kambi iliyokuwa makao makuu ya kikosi cha walinda amani kutoka Tanzania kuanzia TANZBATT - 1 hadi sasa TANZBATT - 13. 

Kutoka hapa Khor Abeche, Darfur nchini Sudan, mimi ni Koplo Japhet Chaula afisa Habari TANZBATT_13 .

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter