Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Robo ya watu wote nchini Ukraine wanahitaji msaada:UN 

Jumba la ghorofa lililoharibiwa kufuatiwa mashambulizi wilaya ya Obolon, Kyiv, Ukraine.
© UNDP/Oleksandr Ratushniak
Jumba la ghorofa lililoharibiwa kufuatiwa mashambulizi wilaya ya Obolon, Kyiv, Ukraine.

Robo ya watu wote nchini Ukraine wanahitaji msaada:UN 

Amani na Usalama

Katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, Ukraine imeshuhudia "mateso, madhila na uharibifu kwa kiwango kikubwa", amesema mratibu wa Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro wa Ukraine akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Lviv Msagharibi mwa Ukraine, na kumuunga mkono Katibu Mkuu kwa kusema, "lazima tukomeshe umwagaji damu na Uharibifu  nchini humo". 

Mratibu huyo Amin Awad ameongeza kuwa "Takriban watu milioni 15.7 nchini Ukraine sasa wanahitaji msaada wa dharura wa kibinadamu na ulinzi wakati zaidi ya watu milioni tano wamekimbia Ukraine na kwenda kutafuta usalama katika nchi nyingine na wengine milioni 7.1 wamekimbia makazi yao na kuwa wakimbizi  nchini kote. Hii inawakilisha zaidi ya asilimia 25 ya wakazi wote wa Ukraine". 

Uharibifu katika jengo la makazi Bucha, Kyiv, Ukraine.
© Said Ismagilov
Uharibifu katika jengo la makazi Bucha, Kyiv, Ukraine.

Uharibifu wa usioelezeka 

Tangu vita kuanza, miundombinu ya kiraia imepata pigo kubwa kutokana na kusambaratishwa kwa vituo vya afya zaidi ya 136 na wastani wa shule 22 kwa siku vikishambuliwa. 

Zaidi ya hayo, mifumo ya maji iliyoharibiwa imeacha watu milioni sita bila upatikanaji wa mara kwa mara wa huduma hiyo muhimu. 

"Ulimwengu unashtushwa na kile kinachotokea Ukraine," amesema bwana Awad akiita ni hali ya kusikitisha jinsi wanavyotendewa wafungwa wa vita na kwamba hatima ya raia huko Mariupol bado haijulikani. 

Wakati huo huo, watu wanaoishi katika mji unaokaliwa wa Kherson wana uhaba mkubwa wa chakula na madawa, mji wa Mykolaiv umekuwa bila maji kwa siku saba na uharibifu wa vituo vya mijini na miundombinu ya kiraia katika maeneo ya oblasts na hasa katika mji wa Donetska, Luhanska, Khakvska, Kyivska na Chernivska umetatiza huduma muhimu kwa mamilioni ya watu , ikiwa ni pamoja na maji na huduma za afya. 

Maelezo ya mashuhuda 

Mratibu huyo wa Umoja wa Mataifa ameelezea uharibifu alioushuhudia. 

"Nimekutana na watu ambao walilazimika kubeba miili ya wanafamilia wao na majirani zao kutoka mitaa ya Bucha na Irpin ili kuzikwa kwenye bustani au makaburi ya pamoja. Siwezi hata kuanza kufikiria mateso yao makubwa”. 

Amekumbusha kwamba kushambulia watu wasio wapiganaji au miundombinu ya kiraia ni "ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu," akitaka kukomesha mashambulizi hayo na kuhakikisha raia wanalindwa na kuruhusiwa kukimbia kwa usalama. 

Mpakani Ukraine na Moldova wakimbizi wakiwa wamepanga foleni.
© UNICEF/Vincent Tremeau
Mpakani Ukraine na Moldova wakimbizi wakiwa wamepanga foleni.

Wahudumu wa kibinadamu na watu wanaorejea 

Wakati huo huo, wasaidizi wa kibinadamu wanakabiliwa na changamoto kubwa ambazo mara nyingi huwazuia kupeleka msaada katika maeneo ambayo watu wanahitaji zaidi. 

"Ninaomba ufikishaji salama na usiozuiliwa wa usaidizi wa kibinadamu,” ametoa wito afisa huyo wa Umoja wa Mataifa. 

Bwana Awad pia amesema takribani zaidi ya watu milioni 12 ambao wametawanhywa na machafuko ya Ukraine sasa wanarejea nyumbani. 

"Kama Umoja wa Mataifa, na pamoja na washirika wetu wa kibinadamu na wa maendeleo, lazima tuwe tayari kuunga mkono suluhisho lao la kudumu tangu mwanzo". 

Amesisitiza wito wa Katibu Mkuu wa kusitishwa  kwa mashambulizi kwa ajili ya masuala ya kibinadamu na haja ya kuweka kando migawanyiko na kuzingatia maslahi ya kkuungana ili kumaliza vita hivi visivyo na maana. 

Msaada mpya wa fedha 

Mratibu wa misaada ya kibinadamu kwa Ukraine, Osnat Lubrani, amevifahamisha vyombo vya habari kwamba ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA, imetoa kwa mashirika ya misaada dola milioni 50 zaidi  mbali na dola milioni 158 ambazo tayari zimetolewa kwa ajili ya shughuli za kuokoa maisha. 

Hii inajumuisha karibu dola milioni 98 kutoka kwa hazina ya masuala ya kibinadamu ya Ukraine (UHF), ukiwa ni mgao mkubwa zaidi tangu hazina hiyo ilipoanzishwa mwaka wa 2019, na dola zingine milioni $60 zimetoka kwenye mfuko wa dharitra wa Umoja wa Mataifa (CERF). 

Huku kukiwa na madai yanayoongezeka ya ubakaji, alisema kuwa sehemu ya fedha hizo zitaelekezwa kuzuia aina yoyote ya unyanyasaji wa kijinsia na kusaidia manusura. 

"Shukrani kwa msaada uliotolewa kwa wakati na wafadhili wetu, fedha hizi zitaturuhusu kufikia mamilioni ya watu haswa katika mikoa iliyoathiriwa zaidi mashariki mwa nchi kwa msaada wanaohitaji ili kuweza kuishi na kukabili labda moja ya changamoto kubwa ya maisha yao,” ameongeza Bi Lubrani. 

Watu wanaokimbia mashambulizi wanapita Lyiv, magharibi mwa Ukraine kuelekea Poland.
© UNICEF/Siegfried Modola
Watu wanaokimbia mashambulizi wanapita Lyiv, magharibi mwa Ukraine kuelekea Poland.

Changamoto ni nyingi 

Licha ya juhudi hizi muhimu na usaidizi wa thamani kubwa, mengi zaidi yanahitajika ili kukidhi mahitaji yanayokua na kuongezeka kila uchao ya Waukraine. 

"Inashangaza jinsi jumuiya ya kibinadamu hapa ilivyoweza, katika wiki chache, kupanua wigo wa msaada kutoka kutoa msaada katika maeneo mawili ya mashariki mwa Ukraine hadi sasa kufanya kazi katika majimbo yot 24," amekiri Bi. Lubnrani. 

"Hata hivyo, bado hatujaweza au tumezuiwa kufika maeneo ambayo watu wanahitaji zaidi msaada, ikiwa ni pamoja na Mariupol na Kherson".