Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tai Tanzania, taasisi inayotambuliwa na mashirika ya UN kwa kuleta mabadiliko chanya Tanzania

Mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi wa Tai (Tai Tanzania na Tai Plus)
Ian Tarimo/Tai Tanzania
Mwanzilishi mwenza na Mkurugenzi wa Tai (Tai Tanzania na Tai Plus)

Tai Tanzania, taasisi inayotambuliwa na mashirika ya UN kwa kuleta mabadiliko chanya Tanzania

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Taasisi hiyo inayofahamika kwa jina la Tai, katika miaka ya hivi karibuni imefanikiwa kuungwa mkono na mashirika ya Umoja wa Mataifa lilikwemo la kuhudumia watoto, UNICEF, na pia shirika la idadi ya watu na afya ya uzazi, UNFPA ambapo mradi na UNICEF ulihusu usafi wakati wa hedhi na wa UNFPA ukiangazia unyanyasaji wa kijinsia na ndoa za utotoni. 

Ian Tarimo ni kijana anayeongoza taasisi hiyo inayotumia masimulizi, michoro, teknolojia ya video na vyombo vya habari kuhamasisha masuala mbalimbali katika jamii. 

Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Tai Tanzania akiwa amevaa shati la kitenge na akijizungushia kipande cha shuka la kimaasai shingoni na ambacho kina bendera ya Tanzania ili kuidhibiti baridi ya New York na pengine kuonesha uzalendo wake kwa nchi yake, akiwa amesimama nje ya makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, anaanza kwa kuieleza UN News Kiswahili namna yeye na wenzake walivyoanza harakati zao na namna walivyoamua kuanza kutumia teknolojia ya katuni. Katuni za 3D au kama anavyoziita yeye, Katuni chapa tatu au 3D Animation films. 

Ian anasema katika miaka mitatu ya kwanza walikuwa wanatumia mbinu za kawaida za kukwenda kwenye jamii na kuzungumza, "lakini vijana walikuwa hawatusikilizi kama tulivyokuwa tunategemea." Ian anaeleza akiongeza kwamba hapo ndipo waligundua kwamba wakitumia ubunifu wataweza kuwafanya watoto wapende kinachofanyika na kwa kufanya hivyo ndivyo watabadilisha mitazamo yao. Hapo ndipo walipoanza kutumia hizo katuni chapa tatu, "ambazo zilikuwa zinatona na hadithi za watoto wenyewe katika mazingira yao. Kwa sababu tulichogundua suluhisho ambalo ni la muda mrefu halitakiwi litoke upande mmoja. Siyo serikali peke yake, wala sio wazazi peke yake ila ni kila mtu atimize wajibu wake." 

Kuhusu ni kwa kiasi gani Tai Tanzania imeifikia jamii, Ian anaonesha ni kwa kiasi kikubwa kwa kuchagua angalau kuzungumzia mwaka mmoja tu uliopita yaani 2021 akisema kwa mfano kwa mwaka jana, wamefika katika shule 80 ambazo ziko katika wilaya 7 zikiwemo Ngorongoro, Sengerema, Pemba, Morogoro, Kasulu na kwingine na kwamba wanajaribu kwenda sehemu ambazo hazifikiki. 

Maudhui katika Katuni Chapa Tatu 

Kuhusu Maudhui wanayoyatengeneza Tai Tanzania, Tarimo anasema kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania na Afrika kwa ujumlasio kila mmoja ana uwezo wa kuwa na simu janja au akaweza kutumia kompyuta na si kila mtu ana intaneti na umeme kwa hivyo wanachokifanya ni kutengeneza maudhui katika mfumo wa Katuni Chapa Tatu kisha wanaweka kwenye televisheni, kwenye mitandao ya kijamii lakini maudhui yale yale yanatengenezwa kwa njia ya michezo ya maigizo ya redioni na wanafanya kazi na redio za kijamii ambazo zinazifikia jamii mbalimbali huko ziliko akitolea mfano Loliondo FM. Pia kwa wale ambao wanakosa furs aya vyote hivyo, Tai inaandaa michoro ambayo inasambazwa katika shule ili kupeleka ujumbe huo huo. 

Tuzo 

Ian Tarimo anajivunia taasisi yake kuwa na tuzo nne hadi sasa ambapo mwaka jana 2021 walipata tuzo ya filamu bora ya katuni, tuzo ambayo ilitolewa na serikali ya Tanzania. Filamu hiyo ilikuwa inahusu mtoto msichana mwenye ualbino ambaye pamoja na changamoto mbalimbali alizozipitia, aliweza kupambana na kuifikia ndoto yake. 

« Mwaka huu kupitia Kwetu Internationa Film Festival, Tai Tanzania imetunukiwa tuzo ya Filamu Bora Afrika Mashariki kutokana na filamu inayohusu jinsi watoto na jamii nzima wanavyoweza kupambana na malaria. » Ian anaeleza akiongeza kuwa walipata tuzo nyingine kutoka UKAID inayohusu jinsi ya kujikinga na Covid-19 na tuzo nyingine kutoka Watoto International Film Festival. 

Kijana huyo akionesha kuwa bado wana mipango mingi ya kuleta mabadiliko chanya katika jamii ili kufanikisha malengo endelevu, SDGs, anasema kuna miradi mingi wataifanya katika siku za usoni ikiwemo kutoa nafasi ya mtandao wao kutumika kutoa taarifa za unyanyasaji wa watoto na manyanyaso ya kijinsia pamoja na masuala mengine muhimu kwa jamii.