Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yashtushwa na vifo vya wasaka hifadhi Malaysia

Mkimbizi wa kabila la rohingya akiwa jimboni Aceh, Indonesia
© UNHCR/Jiro Ose
Mkimbizi wa kabila la rohingya akiwa jimboni Aceh, Indonesia

UNHCR yashtushwa na vifo vya wasaka hifadhi Malaysia

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, limeeleza kushtushwa kwake na ripoti ya vifo vya wasaka hifadhi 6 vilivyotokea wakati wakijaribu kutoroka kutoka kituo cha muda cha uhamiaji kwenye jimbo la Penang, kaskazini mwa Malaysia.

 

UNHCR kupitia taarifa yake iliyotolewa leo, inasema miongoni mwa waliokufa katika tukio hilo la jana Jumatano ni watoto wawili, na shirika hilo limetuma salamu za rambirambi kwa familia za watu hao.

Hofu ya UNHCR pia ni kuhusu tukio hilo katika kituo hicho ambako zaidi ya watu 500 waliokuwa wakishikiliwa, wengi wao wakiwa wakimbizi wa kabila la Rohingya kutoka Myanmar, walitoroka kufuatia maandamano katika kituo hicho.

UNHCR inasema kwa sasa haina taarifa zozote za kina kuhusu tukio hilo au watu waliohusika kwa kuwa “tangu mwezi Agosti mwaka 2019 hatujapokea idhini kutoka mamlaka za uhamiaji ili kuweza kutathmini hali ya vituo vya kushikilia wasaka hifadhi. Hali hii, kwa bahati mbaya inazuia UNHCR kukutana na wanaoshikiliwa korokoroni na kubaini wale wanaohitaji hifadhi ya kimataifa na kuchagiza pia kuachiliwa kwao huru,” imesema taarifa hiyo.

Halikadhalika, UNHCR inasema hofu nyingine ni mustakabali wa waliosalia kwenye kituo hicho kiitwacho Sg Bakap, pamoja na vituo vingine vya aina hiyo nchini Malaysia, ikisema watu wanaoshikiliwa ambao wako hatarini wanahitaji msaada wa UNHCR.

Taarifa hiyo imesema UNHCR na mashirika ya kiraia, yako tayari kusaidia serikali ya Malaysia kuandaa maeneo mbadala ya kushikilia wasaka hifadhi hususan makundi yaliyo hatarini kama vile watoto na wazee na kusaidia pia kutathmini mahitaji ya wale wanaotakiwa kupata hifadhi ya kimataifa.