UNICEF yahakikisha watoto DRC wanasoma licha ya changamoto
UNICEF yahakikisha watoto DRC wanasoma licha ya changamoto
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF linajitahidi kwa kadri ya uwezo wake kuhakiisha watoto walioko kwenye kituo cha makazi ya muda cha Rhoe kwenye jimbo la Ituri nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC wanaendelea kupata haki yao ya msingi ya elimu licha ya mazingira wanamoishi.
Wimbo wa matumaini katikati ya mazingira magumu!
Ni wanafunzi wa shule ya msingi iliyoko Rhoe, kituo cha muda cha makazi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ambako walikimbilia wakazi wa Ituri kufuatia mashambulizi kwenye eneo lao. Kituo kinahifadhi takribani wakimbizi 74,000 miongoni mwao 35,000 ni watoto, kwa mujibu wa UNICEF.
Darasa linaendelea na kipindi ni hesabu, wanafunzi wakipata elimu kuhusu kujumlisha na kutoa.
Baada ya ufafanuzi na wanafunzi kupata jibu anawaambia jipigieni makofi wenyewe!
Miongoni mwa wanafunzi hawa ni Bulkwa ambaye jina lake halisi limehifadhiwa kwa usalama wake.
Ana umri wa miaka 14 na amekumbwa na kiwewe baada ya kushuhudia mwenzake akiuawa na waasi wakati wakikimbia mashambulizi.
“Tulikuwa kwenye makazi ya wakimbizi ya Drodro, mapigano yalipoanza. Nilikuwa nacheza na marafaiki zangu na sikufahamu wazazi walishakimbia. Tulikimbia na rafiki yangu lakini yeye bahati mbaya aliuawa kwa panga kwa sababu alikimbia taratibu.”
Baada ya kufikia Rhoe, alipokelewa na familia moja iliyomlea hadi taasisi ya AJEDEC inayopatiwa ufadhili ya UNICEF katika ilipomkutanisha na mama yake mzazi.
Sasa Bulkwa anasoma na anasema, “shuleni tunacheza soka. Pia tunafundishwa kuheshimu wazazi, tusiibe na tusitukane watu. Tunafundishwa pia kupenda majiran izetu. Baada ya masomo yangu ndoto yangu ni kuwa daktari ili nitibu wazazi wangu na jamii yangu.”