Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Programu za mlo shuleni ni daraja la ndoto za elimu kwa watoto masikini :WFP

Shukrani kwa mpango wa canteen wa shule wa WFP, maelfu ya watoto katika eneo la Matam kaskazini mwa Senegal wanapokea chakula cha moto kila siku. Mpango huu umechangia pakubwa katika kuwarudisha watoto shuleni
ONU Senegal
Shukrani kwa mpango wa canteen wa shule wa WFP, maelfu ya watoto katika eneo la Matam kaskazini mwa Senegal wanapokea chakula cha moto kila siku. Mpango huu umechangia pakubwa katika kuwarudisha watoto shuleni

Programu za mlo shuleni ni daraja la ndoto za elimu kwa watoto masikini :WFP

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP linasema afya bora na lishe bora vinaruhusu watoto kujifunza na kufanya vyema katika masomo yao na hivyo kupanua wigo wa fursa zao za kielimu.

Kwa mujibu wa WFP lishe duni na kukosa mlo ni sababu kubwa ya watoto wengi kutohudhuria masomo hasa katika nchi masikini ikiwemo barani Afrika na ndio maana mwezi uliopita wa Machi ilizindua kampeni kabambe ya kuchagiza programu za mlo mashuleni. 

Kampeni hiyo pamoja na kusaidia watoto wote wenye uhitaji imewawezesha watoto wa kike kusalia shuleni badala ya wazazi wao kuwaozesha mapema kutokana na ugumu wa maisha, hali ambayo inakatiza ndoto zao za elimu na kuchangia katika mimba za utotoni. 

WFP imeongeza kuwa programu za mlo shuleni hutumika kama motisha kwa familia kuandikisha na kuwaweka watoto wao shuleni. 

Lakini pia programu hiyo inawapunguzia wazazi mzigo wa kupanga bajeti ya chakula cha mchana, huwaongezea mapato na kusaidia kupunguza umaskini. 

Kwa mujibu wa WFP milo ya shuleni inawakilisha asilimia 10 ya mapato ya kaya maskini na zilizo hatarini, na hiyo ni akiba kubwa kwa familia zilizo na mtoto zaidi ya mmoja. 

Katika kunufaisha watoto na familia zao, WFP inasema mlo shuleni na afya husaidia kujenga kile kinachojulikana kama ‘mtaji wa kibinadamu’ ambao unajumuisha afya ya watu, ujuzi, elimu, uzoefu na mazoea. 

WFP inasema thamani ya programu za mlo shuleni ni kubwa zaidi ya mlo mmoja. Na kupitia shirika hilo sasa programu za mlo shuleni zinawafikia watoto wa shule milioni 15 katika nchi 61.  

Juhudi hizo humpa kila mtoto matumaini ya kujifunza na motisha wa kusalia shuleni huku zikizalisha kipato kwa wakulima wadogo kupitia vyakula vinavyonunuliwa na WFP ndani ya nchi kwa ajili ya kulisha Watoto hao.