Mlo shuleni warejesha ari na matumaini kwa watoto Haiti baada ya tetemeko la ardhi

Maandalizi ya mlo wa mchana kwa wanafunzi 307 katika shule ya Dame Marie kusini-magharibi mwa Haiti
UN Haiti/Daniel Dickinson
Maandalizi ya mlo wa mchana kwa wanafunzi 307 katika shule ya Dame Marie kusini-magharibi mwa Haiti

Mlo shuleni warejesha ari na matumaini kwa watoto Haiti baada ya tetemeko la ardhi

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Haiti watoto wa familia ambazo ziliathiriwa vibaya na tetemeko kubwa la ardhi lililosambaratisha kwa kiasi kubwa eneo la kusini-magharibi mwa nchi hiyo mwezi Agosti mwaka huu sasa wanapata mgao wa bure wa chakula shuleni kama sehemu ya hatua ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP ya kusaidia jamii zilizo hatarini zaidi kujikwamua.

Saa 5 asubuhi katika shule ya wasichana ya Dame Marie, shule iliyoko rasi ya magaharibi mwa eneo la kusini mwa Haiti. Wapishi wawili wa kujitolea wamechelewa kidogo katika maandalizi ya mlo wa siku ya leo kwa wanafunzi 307.

Mlo wa leo ni maharagwe ambayo yanachukua muda mrefu kuliko kawaida kuiva. Viambato vingine vitakavyoongezwa ni pamoja na ngano kidogo, mafuta ya kula, vitunguu na pilipili.

Majani ya mgomba yametumika kufunika sufuria zilizopikia maharagwe na bulga, mlo wa shuleni kwa ajili ya watoto 300.
UN Haiti/Daniel Dickinson
Majani ya mgomba yametumika kufunika sufuria zilizopikia maharagwe na bulga, mlo wa shuleni kwa ajili ya watoto 300.

Hapa wanafunzi wote, wa kike na wa kiume licha ya jina kuitwa Shule ya Wasichana ya Dame Marie, wananufaika na mradi wa WFP wa mgao wa chakula shuleni wenye lengo la kuwapatia watoto walio hatarini zaidi angalau mlo mmoja kwa siku.

Mkuu wa shule Franesie Sylvestre anasema kwa watoto wengi “huu ni  mlo pekee watakaokula kwa siku ya leo.

Mji wa Dame Marie ulidhuriwa na tetemeko la ardhi lakini shule hii iliharibika kidogo tu kwa kupata nyufa kwenye kuta za majengo yake na lango kuu la kuingia liliporomoka.

Madhara ya tetemeko

Madhara makubwa ni kwa wazazi wa wanafunzi wa shule hii, wengi wao wamepoteza mashamba yao au wameshindwa kupanda mazao wakati wa msimu wa upanzi kutokana na tetemeko la ardhi.
“Hawawezi tena kulima mazao ya chakula,” anasema Mwalimu Mkuu Sylvestre, “kwa hiyo hawawezi kulisha vyema watoto wao. Ndio maana mpango wa mlo shuleni ni muhimu sana. Unawapatia watoto nguvu na ari ya kuendelea kusoma na kusaidia wazazi wao, jambo ambalo baadaye linakuwa jema kwa jamii.”

Mpango wa mlo shuleni ulikuwepo hata kabla ya tetemeko la ardhi tarehe 14 mwezi Agosti kupiga eneo la kusini-magharibi mwa Haiti, tetemeko ambalo lilisababisha zaidi ya watu 2,200 kufariki dunia na wengine 12,700 walijeruhiwa huku miundombinu ya msingi kama vile madaraja, barabara, hospitali na shule kusambaratishwa kabisa au kuharibika kiasi.

Mtoto ananawa mikono kabla ya kula mlo shuleni nchini Haiti
UN Haiti/Daniel Dickinson
Mtoto ananawa mikono kabla ya kula mlo shuleni nchini Haiti

Shule hii ni moja tu kati ya shule 1600 ambazo zinanufaika na mradi wa WFP wa kupatia wanafunzi mlo shuleni. Jumla ya wanafunzi 344,000 wanapata mlo kupitia mpango huu. Katika shule nyingi, mpango huu unajikita zaidi ya kuwapatia watoto mlo.

Mpango wenye mapana zaidi

Vituo vidogo vya kunawa mikono vimewekwa nje ya madarasa. Vituo hivi vimewekwa na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kuhakikisha watoto wanajifunza suala la usafi na kujisafi ikiwemo kunawa mikono kabla ya kula chakula.

UNICEF pia inasambaza vitabu vya kujifunza lugha ya kifaransa, hisabati na masomo mengine huku pia ikisambaza madawati ili wanafunzi wajisomee kwa faraja zaidi.

“Tumechukua mwelekeo mpana na wa jumla zaidi,” anasema  Afisa wa  WFP Maguelita Varin, “kwa sababu iwapo watoto hawatonawa mikono na kula chakula, wanaweza kuugua. Na iwapo hawana vitabu hawawezi kusoma hata kama wamekula vizuri.”

Mpango wa WFP wa mlo shuleni unatarajiwa kusambazwa zaidi ili kutoa milo itokanayo na mazao yaliyolimwa katika eneo ambako chakula kinapatiwa watoto 40,000 kwenye shule 190 zilizoko wilaya 3 za Haiti zilizoathiriwa na tetekemo la ardhi.

Shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani, ILO nalo linatarajia kusaidia kilimo miongoni mwa wakulima wa mashelisheli, zao ambalo hupatia jamii chakula chenye lishe. Inatarajiwa kuwa shelisheli litakuwa kiambato cha msingi kwenye mlo wa shule, kitendo ambacho kitasaidia pia uchumi wa jamii.

Watoto nchini Haiti wamepanga mstari kupata mlo wa bure unaotolewa na WFP
UN Haiti/Daniel Dickinson
Watoto nchini Haiti wamepanga mstari kupata mlo wa bure unaotolewa na WFP

“Hatua hii inasaidia kuendeleza uchumi wa jamii na unahamasisha wakulima wapande mazao zaidi.,” amesema Maguelita. “Hatimaye, itasaidia jamii kujikwamua kwa ubora zaidi na kujenga mnepo kwa majanga ya siku za usoni.”

Katika shule ya wasichana ya Dame Marie, chakula kimeiva, na wanafunzi wamejipanga mstari kunawa mikono kabla kujiunga na foleni ya kupokea chakula cha moto. Kwa wengi huu ni mlo wao wa kwanza wa siku na wengi wanaonekana wana najaa.

Baada ya kupatiwa mlo wanarejea kwenye madawati yao na kuanza kula maharagwe na bulga, wakiwa hawana kabisa muda wa mazungumzo huku walimu wakiwa na uhakika kuwa watashiba na kisha kuendelea kusikiliza vyema masomo yanayofuatia.