Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 300 wanakosa mlo shuleni sababu ya COVID-19:WFP

Mpango wa mlo shuleni kwa hisani ya WFP hapa watoto wako kwenye kituo cha elimu Kibera, Kenya.
WFP/Challiss McDonough
Mpango wa mlo shuleni kwa hisani ya WFP hapa watoto wako kwenye kituo cha elimu Kibera, Kenya.

Watoto milioni 300 wanakosa mlo shuleni sababu ya COVID-19:WFP

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limesema takribani watoto milioni 300 sasa wanakosa huduma ya mlo shuleni kutokana na virisi vya corona, COVID-19 vilivyosababisha maelfu ya shule kufungwa kote duniani.

Shirika hilo linasema lina jukumu kubwa la kuhakikisha msaada wa chakula kwa watu milionin 87 kote duniani huku likisaidia juhudi za kukabiliana na mlipuko wa COVID-19.

Hivi sasa zaidi ya vijana na Watoto milioni 860, karibu nusu ya wanafunzi wote duniani wamelazimika kukaa nyumbani mbali na shule na vyuo vikuu kwa sababu ya COVID-19. Nchi zaidi ya 100 zimefunga shule zake zote nchi nzima na zingine zinaendelea kufuata nyayo. Akizungumxza na waandishi wa habari mjini Geneva hii leo msemahi wa WFP Elisabeth Byrs amesema,“Maendeleo haya yana athari kubwa kwa masomo ya watoto lakini pia kwa suala lingine muhimu la maisha yao kama mlo shuleni. Kwa sababu ya mlipuko wa COVID -19, watoto milioni 300 wa shule za msingi wanakosa mlo mashuleni ambao wanautegemea .“

Ameongeza kuwa, "karibu nchi 30 ambako WFP inaendesha programu ya mlo mashuleni kumeripotiwa shule kufungwa nchi zima au kwa sehemu kubwa  na hii inamaanisha kwamba karibu watoto milioni 9 hawapati tena mlo shuleni unaotolewa na WFP na kwamba idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka katika siku na wiki zijazo.

 

Nini kinafanyika sasa

Hivi sasa WFP inashirikiana na wadau na washirika wake kuhakikisha kwamba wanafunzi na familia zao wanaendelea kupokea msaada ambao unashughulikia mahitaji yao ya chakula na lishe wakati huu wa mgogoro wa COVID-19.

Na kwa shule ambazo bado hazijafungwa WFP inasema kipaumbele ni kuhakikisha usafi na kuzingatia viwango vya usalama wa chakula vinafuatwa ili kupunguza hatari ya maambukizi.

Shirika hilo linasema kwa nchi ambako shule zimefungwa linafanya tathimini ya uwezekano wa njia mbadala ya kuwasaidia watoto. Njia hizo ni pamoja na kutoa mgao wa chakula wa kwenda nao nyumbani, kuwafikishia chakula nyumbani na kutoa fedha taslim au vocha.

Pia kwa nchi ambako programu za dharura zimeanzishwa na serikali WFP inapigia chepuo ujumuishwaji wa watoto wa shule za msingi katika programu hizo.

Mpango wa WFP wa mlo mashuleni unaendeshwa katika nchi 61 duniani na unatumika kama ngao muhimu ya ulinzi  wa kijamii hasa kwa Watoto masikini na familia zisizojiweza.