Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Picha kutoka angani ya eneo la Goroka, Papua New Guinea

Hatari ya kutetea wanawake wanaotuhumiwa kwa uchawi nchini Papua New Guinea

© Lake Media
Picha kutoka angani ya eneo la Goroka, Papua New Guinea

Hatari ya kutetea wanawake wanaotuhumiwa kwa uchawi nchini Papua New Guinea

Haki za binadamu

Nchini Papua New Guinea, suala la kuwatetea wanawake wanaotuhumiwa kwa uchawi, imekuwa kazi ya kutishia maisha. 

Umoja wa Mataifa na Muungano wa Ulaya kupitia mradi wao wa “Spotlight Initiative”, wanahamasisha utungaji wa sheria ambayo italinda watetezi wa haki za binadamu walio hatarini nchini humo, ambao wapo hatihati ya kufanyiwa vurugu, mateso na hata kifo.

"Tunapojaribu kuwasaidia wengine, au tunapokwenda mahakamani kusimamia kesi ya mtu, tunakabiliana na vitisho na vitu ya kuogofya," anasema Mary Kini, kutoka Mitandao ya Watetezi wa Haki za Kibinadamu wa Nyanda za Juu.

Gharama ya kibinafsi

Kwa zaidi ya miaka 14, Mary Kini amekuwa akifanya kazi ya kuwasaidia wathirika wa unyanyasaji unaohusiana na uchawi, na unyanyasaji wa kijinsia, huko Papua New Guinea (PNG), licha ya kazi hiyo kuwa na gharama kubwa ya kibinafsi ambayo mara nyingi huja nayo.

Hivi majuzi Kini alijiunga na watetezi wenzake wa haki za binadamu Eriko Fuferefa, wa Chama cha Wanawake wa Kafe Mjini Settlers, na Angela Apa, wa Kup Women for Peace huko Mount Hagen, kwa mashauriano ya siku tatu kuhusu maendeleo ya shughuli yao muswada wa Ulinzi wa Watetezi wa Haki za Kibinadamu.

“Kwa miaka mingi hatujalindwa, na baadhi ya watetezi wa haki za binadamu wameuawa,” alisema Fuferefa. “Baadhi yao wananyanyaswa, au kuteswa. Tuna alama za mapigo mingi sana.”

Kufuatia juhudi za zinazopigiwa chepuo na Spotlight Initiative, sasa kuna ushawishi mkubwa wa kisiasa wa masuala ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, uliodhihirishwa na uchunguzi wa kwanza wa Bunge Maalum la nchi kuhusu ukatili wa kijinsia, ambao uliwasilisha mapendekezo bungeni na kutunga sheria katika eneo hilo. unyanyasaji unaohusiana na tuhuma za uchawi.

Mtetezi wa haki za binadamu Mary Kini, Papua New Guinea
© Spotlight Initiative/Rachel Donovan
Mtetezi wa haki za binadamu Mary Kini, Papua New Guinea

Walitaka kuniua

Shughuli za kuwatambua wanaoshutumiwa kwa uchawi hutofautiana baina ya wilaya, lakini kwa ujumla, mtu anapofariki bila kutarajiwa, familia ya marehemu itawasiliana na Glasman (mwanaume) au Glasmeri (mwanamke) ili kubaini ni nani katika jamii anayehusika.

Kitendo cha kushutumiwa kwa uchawi na Glasman au Glasmeri kunasababisha kuteswa na kuuawa kwa makumi ya wanawake kote PNG. Ingawa shutuma zinaweza kutolewa kwa wanaume na wanawake, wengi wa waathirika wa unyanyasaji ni wanawake.

“Mume wangu alipofariki tulimpeleka kijijini kwake na huko familia yake ilianza kunishuku kuwa nilimuua hivyo wakapanga kunikata kichwa na kunizika pamoja na marehemu mume wangu,” anaeleza mmoja wa manusura. “Haikuwa kweli, walitaka kuniua tu.”

“Watu wana kanuni hizi, imani hizi,” alisema Bi Kini. “Wakati Glasman au Glasmeri anakuja na kusema jambo, watu huitikia moja kwa moja kile wanachosema.”

Mabadiliko ya muda mrefu

Marekebisho yaliyofanywa kwenye kanuni ya Jinai yanaifanya kuwa kinyume cha sheria kutumia, kujaribu kutumia au kutishia kutumia huduma zao. Adhabu ni pamoja na hadi miaka 10 jela na faini ya hadi 10,000 PGK.

Katika mawasilisho ya Uchunguzi wa Bunge Maalum la mwaka 2021, Kikundi cha mradi wa Spotlight Civil Society (ambacho Bi. Kini ni mwenyekiti mwenza) kilipendekeza Serikali kupitia upya sera na sheria zinazoshughulikia kanuni za kijamii zinazoruhusu unyanyasaji unaohusiana na uchawi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya Glasman na Glasmeri.

“Hili ni muhimu sana, na nimefurahishwa sana kwamba hili limepita kwani hili ni jambo ambalo tumekuwa tukiomba kwa muda mrefu,” akamalizia Bi Kini.

Waelimishaji rika wanasambaza kondomu na taarifa za Afya ya uzazi katika masoko ya Kokopo, Papua New Guinea
© Spotlight Initiative/Rachel D
Waelimishaji rika wanasambaza kondomu na taarifa za Afya ya uzazi katika masoko ya Kokopo, Papua New Guinea

Vurugu inayohusiana na uchawi

Mashauriano yaliyofanyika kwa ushirikiano na Spotlight Initiative na Tume ya Kurekebisha Katiba na Sheria, yalikuwa ya kwanza kati ya manne yaliyofanyika mwezi Machi nchini kote Papua New Guinea, ili kuendeleza sheria ambayo inawalinda vyema watetezi wa haki za binadamu dhidi ya kulipiza kisasi au vitisho wakati wa utekelezaji wao wa kazi.

Watetezi wa haki za binadamu mara nyingi hulengwa wanapomsaidia mtu aliyenusurika katika unyanyasaji unaohusiana na shutuma za uchawi kwa sababu wanaonekana kuwa wanaingilia desturi za kimila, au wanapowasaidia waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia kuhama majimbo, kwa sababu wanachukuliwa kuwa wanaingilia kati. suala la familia.

Kwa mujibu wa ripoti zilizo tolewa na vyombo vya habari, wastani wa kesi 388 za unyanyasaji unaohusiana na shutuma za uchawi huripotiwa katika mikoa minne ya Nyanda za Juu kila mwaka, lakini hofu ya kulipiza kisasi inamaanisha kuwa idadi halisi ya waathirika huenda ikawa kubwa zaidi.