Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yahuzunishwa na mamlaka ya Mali kumfukuza mwakilishi wake nchini humo

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk
UN Photo/Violaine Martin
Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu Volker Türk

UN yahuzunishwa na mamlaka ya Mali kumfukuza mwakilishi wake nchini humo

Haki za binadamu

Kamishna Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk Jumatatu ameeleza kusikitishwa na uamuzi wa mamlaka ya Mali kumtangaza Mwakilishi Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu nchini humo kama mtu asiyefaa au persona non grata.

Katika taarifa yake iliyotolewa leo jijini Geneva Uswisi Turk amesema, “Nimehuzunishwa na uamuzi uliochukuliwa na mamlaka ya Mali kumtangaza mwakilishi wangu, Guillaume Ngefa, kama mtu asiyefaa na kumwamuru kuondoka nchini humo ndani ya saa 48. Nimekuwa nikifadhaishwa sana na vitisho na unyanyasaji ambao amekumbana nao katika mitandao ya kijamii katika miezi ya hivi karibuni.”

Mkuu huyo wa masuala ya haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa hawapaswi kamwe kutishiwa au kuwekewa vikwazo kwa kufanya kazi yao, ambayo inayotokana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.

"Nina imani kamili na taaluma na kujitolea kwake katika kukuza na kulinda haki za binadamu nchini Mali. Natoa wito kwa uongozi wa mpito nchini Mali kubatilisha uamuzi huu wa kusikitisha bila kuchelewa ” amesema Turk.

Uamuzi huo wa kumtaka Ngefa kuondoka nchini Mali kwakuwa ni mtu asiyefaa ulitangazwa katika taarifa ya Serikali iliyotolewa hapo jana tarehe 5 Februari, 2023  ikisisitiza kwamba Ngefa, ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Haki za Kibinadamu cha ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA na Mwakilishi wa Kamishna Mkuu nchini Mali.

Uamuzi huo ulitangazwa wakati Ngefa alikuwa tayari nje ya Mali.

Umoja wa Mataifa kwa muda mrefu umeshikilia uamuzi wake kuwa kutangazwa kwa mtu asiyefaa au persona non grata hakupaswi kutumika kwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa. Ni kinyume na wajibu wa Nchi Wanachama chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na matakwa yanayohusu haki na kinga za Umoja wa Mataifa na wafanyakazi wake.

“Haki za binadamu ni muhimu katika kulinda amani," Türk alisisitiza katika taarifa hiyo na kuongeza kuwa “Ninaomba mamlaka kuweka mazingira ya heshima, usalama na wezeshi kwa ajili ya kufanya kazi ya haki za binadamu nchini Mali, ambayo ni muhimu zaidi kuliko hapo awali katika muktadha wa sasa".

Turk alihitimisha taarifa yake kwa kuiomva mamlaka ya Mali kuhakikisha watetezi wa haki za binadamu wana heshimiwa na kuna mazingira bora ya kulinda watetezi wa haki za binadamu “Hakuna mtu anayepaswa kukabiliwa na kisasi kwa kuzungumza juu ya maswala ya haki za binadamu.”