Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatma ya DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki mikononi mwa Mawaziri wa jumuiya hiyo

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki (kulia) akihojiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando mwa Mjadala Mkuu wa UNGA76
UN News/Assumpta Massoi
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Peter Mathuki (kulia) akihojiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa kando mwa Mjadala Mkuu wa UNGA76

Hatma ya DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki mikononi mwa Mawaziri wa jumuiya hiyo

Masuala ya UM

Wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa nchi duniani kuimarisha ushirikiano wa kimataifa iwe kikanda au kidunia unazidi kuitikiwa ambapo Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC inachukua hatua kupanua wigo wa uanachama wake kutoka 6 hadi 7 kwa kufanya kikao cha kujadili ombi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kujiunga na chombo hicho. 

 

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika MAshariki, Peter Mathuki ametoa taarifa hizo wakati akihojiwa na Leah Mushi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa kando mwa mjadala mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliomalizika jana jijini New York Marekani ambaye alitaka kufahamu mchakato wa DRC kuijunga na jumuiya hiyo umefikia wapi? 

“Nilikwenda DRC kuonana na Rais Felix Chisekedi na kufanya naye mazungumzo, akatupa baraka zake na kutueleza wako tayari kujiunga na Jumuiya.” 

Katibu Mkuu Mathuki amesema kikao cha Marauda wa Afrika Mashariki kilichokaa mwezi February mwaka huu 2021 waliiagiza Sekretarieti ya jumuiya kwenda nchini DRC na kuangalia ambavyo DRC imejitayarisha. 

“Nimetuma timu kule (DRC), timu ya makatibu wakuu ambao walienda wakakutana na wenzao kutoka nchini DRC wakaangalia mikakati na kuandika ripoti na tayari wameshanikabidhi na nimeitisha kikao cha Baraza la mawaziri tarehe 11-13 mwezi Octoba 2021 ili wakae waangalie hiyo ripoti na kuandika mapendekezo yao kwa Baraza la Marais. Wakishaweka hayo mapendekeoz basi ndio DRC itajiunga.” 

Alipoulizwa iwapo kwakuangalia ripoti hiyo kuna uwezekano wa DRC kujiunga Mathuki amesema 
“Nikiangalia, nikitazama vizuri naona kweli kuna uwezekano mkubwa sana kutoka kwa upande wa DRC na kutoka kwa uongozi kwa Afrika Mashariki kuona ni vizuri sana kwa DRC kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwahiyo hivi karibuni tutakuwa n anchi 7 katika jumuiya Inshallah. “ 

Mpaka sasa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.