Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura kusimamisha haki za uanachama wa Shirikisho la Urusi katika Baraza la Haki za Kibinadamu wakati wa Kikao Maalum cha Dharura kuhusu Ukrainia.

Baraza Kuu la UN limepitisha azimio Urusi isitishwe uanachama kwenye Baraza la Haki za Kibinadamu.

UN Photo/Manuel Elías
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura kusimamisha haki za uanachama wa Shirikisho la Urusi katika Baraza la Haki za Kibinadamu wakati wa Kikao Maalum cha Dharura kuhusu Ukrainia.

Baraza Kuu la UN limepitisha azimio Urusi isitishwe uanachama kwenye Baraza la Haki za Kibinadamu.

Haki za binadamu

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa , leo limepiga kura kupitisha azimio linalotaka Urusi isitishe uanachama kwenye Baraza la Haki za binadamu . 

Azimio hilo lilipata kura theluthi mbili zinazohitajika kwenye Baraza hilo lenye wajumbe 193, ambapo mataifa 93 yakipiga kura ya ndiyo na 24 yakipinga, huku mengine 58 yakijiengua kupiga kura katika mchakato huo. 

Mkutano huo umeashiria kurejeshwa kwa kikao maalum cha dharura kuhusu vita nchini Ukraine na kufuatia ripoti za ukiukaji wa sheria unaofanywa na vikosi vya Urusi. 

Baraza Kuu lapiga kura kusimamisha wanachama wa Urusi katika Baraza la Haki za Kibinadamu.
UN News
Baraza Kuu lapiga kura kusimamisha wanachama wa Urusi katika Baraza la Haki za Kibinadamu.

Mauaji ya kikatili 

Mwishoni mwa wiki iliyopita, picha za kutisha ziliibuka kutoka mji wa Bucha, kitongoji cha mji mkuu, Kyiv, ambapo mamia ya miili ya raia ilipatikana mitaani na kwenye makaburi ya halaiki kufuatia Urusi kujiondoa katika eneo hilo. 

Kabla ya kura hiyo, balozi wa Ukraine Sergiy Kyslytsya alizitaka nchi kuunga mkono azimio hilo. 
"Bucha na makumi ya miji na vijiji vingine vya Ukraine, ambapo maelfu ya wakaazi walioishi kwa amani wameuawa, kuteswa, kubakwa, kutekwa nyara na kuibiwa na Jeshi la Urusi, ni mfano wa jinsi Shirikisho la Urusi lilivyokengeuka dhidi ya maazimio yake ya awali katika suala la haki za binadamu. Ndiyo maana kesi hii ni ya kipekee na hatua ya leo ni dhahiri na inayojieleza,” amesema. 

Gennady Kuzmin, naibu balozi wa Urusi, alitoa wito kwa nchi "kupiga kura kupinga jaribio la nchi za magharibi na washirika wao kuharibu usanifu uliopo wa haki za binadamu." 

Baraza kuu la Umoja wa Mataifa  limepiga kura juu ya uanachama wa Urusi katika Baraza la Haki za Kibinadamu.
UN News
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limepiga kura juu ya uanachama wa Urusi katika Baraza la Haki za Kibinadamu.

Ufafanuzi wa azimio 

Katika azimio hili, Baraza Kuu linaonyesha "wasiwasi wake mkubwa katika mgogoro wa kibinadamu na haki za binadamu unaoendelea nchini Ukraine, hasa katika ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa sheria ya kimataifa ya kibinadamu na unaotekelerzwa na Shirikisho la Urusi". 

Katika muktadha huu, Baraza Kuu ambalo lina nchi wanachama 193, "limeamua kusimamisha haki ya uanachama wa Baraza la Haki za Kibinadamu ya Shirikisho la Urusi". 

Baraza la Haki za Kibinadamu lenye makao yake makuu mjini Geneva, Uswis lina mataifa 47 wanachama. 
Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, ambalo linachagua wajumbe wa Baraza la Haki za Kibinadamu, limeswahi kuisimamisha nchi nyingine moja tu huko nyuma,  ambayo ni Libya mnamo 2011. 

Sambamba na Rwanda 

Upigaji kura umefanyika katika siku ya kumbukizi ya mauaji ya kimbari ya Rwanda ya 1994 dhidi ya Watutsi, na balozi wa Ukraine alichora taswira inayoshabihiana na ukurasa huu wa giza katika historia ya hivi karibuni.

"Mauaji ya kimbari nchini Rwanda kwa kiasi kikubwa yalitokana na kutojali kwa jumuiya ya kimataifa, wakati Umoja wa Mataifa haukuitikia maonyo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na katika Baraza Kuu, mwaka mmoja kabla ya janga ambalo tunaadhimisha kumbukumbu yake siku hii," alisema. Mheshimiwa Kyslytsya. 

Ameongeza kuwa "Leo, kwa upande wa Ukraine, sio mwaka, kwa sababu janga linatokea hivi sasa mbele ya macho yetu." 

Mishingi ya kusitishwa haki ya uanachama 

Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa lina wajumbe 47 na makao yake makuu ni Geneva Uswis. 
Urusi ilijiunga na baraza hilo mwezi Januari 2021 kama moja ya nchi 15 zilizochaguliwa na Baraza Kuu kuhudumu kwa miaka mitatu. 

Chini ya azimio la mwaka 2006 lililoanzisha Baraza hilo, Baraza Kuu linaweza kusitisha uanachama wa nchi ikiwa itafanya ukiukaji mkubwa na wa kupangwa wa haki za binadamu. 

Baraza Kuu Lapiga Kura ya kusimamisha Urusi kutoka kwa Baraza la Haki za Kibinadamu. Pichani mwishoni mwa safu kulia, ni Naibu Mwakilishi Mkuu wa Urusi, Gennady Kuzmin.
UN Photo/Manuel Elías
Baraza Kuu Lapiga Kura ya kusimamisha Urusi kutoka kwa Baraza la Haki za Kibinadamu. Pichani mwishoni mwa safu kulia, ni Naibu Mwakilishi Mkuu wa Urusi, Gennady Kuzmin.

Urusi yajiengua kwenye Baraza 

Akizungumza baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Naibu Mwakilishi wa kudumu wa Urusi kwenye umoja wa Mataifa Kuzmin, ghafla alisema kwamba Urusi ilikuwa tayari imeamua siku hiyo, kujiengua kwenye Baraza kabla ya mwisho wa muda wake. 

Amedai kwamba Baraza hilo limehodhiwa na kundi la Mataifa yanayolitumia kwa malengo yao ya muda mfupi. 

"Mataifa haya kwa miaka mingi yamehusika moja kwa moja katika ukiukwaji wa wazi na mkubwa wa haki za binadamu, au kuunga mkono ukiukwaji huo," amesema, akizungumza kupitia mkalimani. 

Amongeza kuwa "Licha ya kuwa wanachama wa Baraza hilo, hawako tayari kuacha masilahi yao ya muda mfupi ya kisiasa na kiuchumi kwa ajili ya ushirikiano wa kweli na kuleta utulivu wa kweli wa hali ya haki za binadamu katika baadhi ya nchi." 

Mfano hatari: yasema China 

China ilikuwa miongoni mwa nchi zilizopiga kura kupinga azimio hilo. Balozi ZHANG Jun, alihofia hatua yoyote ya haraka katika Baraza Kuu itakuwa kama "kuongeza mafuta kwenye moto", kwani ingezidisha migawanyiko, kuzidisha mzozo, na kuhatarisha juhudi za amani. 

"Kushughulikia uwanachama wa Baraza la Haki za Kibinadamu kwa njia kama hiyo kutaweka historia mpya ya hatari, kuzidisha makabiliano katika uwanja wa haki za binadamu, kuleta athari kubwa katika mfumo wa utawala wa Umoja wa Mataifa, na kuleta madhara makubwa," amesema. 

EU yapongeza uamuzi adimu 

Kwa Muungano wa Ulaya (EU), ukubwa na uzito wa ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na Urusi nchini Ukraine, na wa uadilifu wa eneo na mamlaka ya nchi hiyo, unahitaji mwitikio thabiti na wa pamoja wa kimataifa. 

"Uamuzi adimu ambao Baraza hili limeuchukua leo unatoa ishara kali ya uwajibikaji na tunatumai utasaidia kuzuia na kukatisha tamaa ukiukaji zaidi wa haki za binadamu," amesema Balozi Olaf Skoog, mkuu wa wajumbe wa EU.