Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Buriani walinda amani 8 wa Umoja wa Mataifa nchini DRC

Bintou Keita (kulia) ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC akiwa na Waziri wa Ulinzi wa DRC, Gilbert Kabanda wakati wa tukio la kuaga miili ya walinda amani 8 waliokufa baada ya  helikopta yao kuanguka tarehe 29 mwezi Machi mwaka huu
MONUSCO/ Yves Ntole
Bintou Keita (kulia) ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa UN nchini DRC akiwa na Waziri wa Ulinzi wa DRC, Gilbert Kabanda wakati wa tukio la kuaga miili ya walinda amani 8 waliokufa baada ya helikopta yao kuanguka tarehe 29 mwezi Machi mwaka huu wa 2022 huko Kivu Kaskazini.

Buriani walinda amani 8 wa Umoja wa Mataifa nchini DRC

Amani na Usalama

Nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC kumefanyika tukio la kuaga miili ya walinda amani wanane wa Umoja wa Mataifa waliokuwa wakihudumu kwenye ujumbe wa Umoja huo wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO. Walipoteza maisha baada ya helikopta waliyokuwa wakisafiria kuanguka tarehe 29 mwezi uliopita wa Machi. 

 

Walinda amani wanatoka Pakistani, Urusi na Serbia ambapo simanzi ilitawala katika tukio hilo mjini Goma jimboni Kivu Kaskazini, wakati miili ya walinda amani hao wanane wa Umoja wa Mataifa ilibebwa na walinda amani wenzao tayari kuagwa.

Shughuli iliafanyika kwa gwaride maalum huku majeneza yao yakiwa yamefunikwa kwa bendera mbili: Ya Umoja wa MAtaifa na taifa la mlinda amani.

Wakati mauti yanawakuta, walikuwa kwenye operesheni ya kuimarisha ulinzi kwenye eneo laTshanzu, kusini-mashariki mwa mji wa Rutshuru jimboni humo. 

Viongozi waandamizi wa MONUSCO akiwemo Mkuu wake Bintou Keita pamoja na mabalozi wa Pakistani, Urusi na Serbia sambamba na wa serikali ya DRC walishiriki tukio hili la huzuni.

Mkuu wa Idara ya Umoja wa Mataifa inayohusika na ulinzi wa amani, Jean-Pierre Lacroix akasema, “hii leo tunaketi hapa tukitafakari, siyo tu kwa huzuni iliyotughubika, bali pia kwa jinsi tukio kama hili linaongeza juhudi zetu kwa wananchi wa DRC na pia urafiki wao umeimarisha maisha kwenye MONUSCO na pia kujituma kwao katika kusongesha amani kwenye nchi hii na duniani kwa ujumla.”

Ameongeza kuwa kila mara tukio kama hilo linapofanyika wanatambua ni jinsi gani walinda amani wanajitoa uhai wao kwa wengine.

“Yeyote kati yetu ambaye amehudumu MONUSCO na kutangamana na walinda amani au kushuhudia kiwango cha changamoto ambazo wananchi wa DRC wanakumbana nazo kila siku, atatambua fika kuwa ulinzi wa amani unahitaji uzingatiaji mkubwa wa misingi ya Umoja wa Mataifa,” ametamatisha Bwana Lacroix.

Miili ya walinda hao imesafirishwa kwenda makwao.