Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usonji isiwe sababu ya kutojumuishwa au kutopiga hatua maishani

Martha Gathara,  mwalimu katika kituo cha kijamii cha mafunzo, KCCL jijini Nairobi, Kenya akiandaa herufi maalum zinazotumiwa na watoto wenye usonji.
UN Video
Martha Gathara, mwalimu katika kituo cha kijamii cha mafunzo, KCCL jijini Nairobi, Kenya akiandaa herufi maalum zinazotumiwa na watoto wenye usonji.

Usonji isiwe sababu ya kutojumuishwa au kutopiga hatua maishani

Haki za binadamu

Siku ya usonji duniani huadhimishwa tarehe 2 Aprili  kila mwaka tangu mwaka 2007. 

 

Umoja wa Mataifa umeitenga siku hiyo ili kuielimisha jamii kuhusu usonji ambalo ni tatizo la kushindwa kusoma na kujieleza katika maisha ya kawaida. 

Kauli mbiu ya mwaka huu 2022 ni “Elimu bora inayowajumuisha wote”. Shule ya Kenya Community Centre for Learning, KCCL, iliyoko mtaani Roysambu jijini Nairobi ni moja ya zile zinazowapa elimu watoto walio na usonji na matatizo mengine ya kusoma. 

Hii ni shule ya kipekee kwani wanafunzi wa hapa wana changamoto za kusoma. Wanafunzi wanapewa  nafasi kubwa ya kucheza na kunyoosha viungo kila wanapohitaji. 

Eneo la mapokezi lina ishara za muongozo wa maisha wanaoufuata. Usonji unaweza kubainika mtoto anapokuwa mdogo kwa mfano umri wa miaka miwili. 

Wanafunzi katika shule ya watoto wenye usonji katika kituo cha jamii cha kujifunza Kenya, KCCL wakiwa kwenye picha iliyopigwa na mwenzao mwenye usonji kama mbinu za kujumuisha watoto kwenye elimu.
UV Video
Wanafunzi katika shule ya watoto wenye usonji katika kituo cha jamii cha kujifunza Kenya, KCCL wakiwa kwenye picha iliyopigwa na mwenzao mwenye usonji kama mbinu za kujumuisha watoto kwenye elimu.

Wataalam wa saikolojia na madaktari ndio wanaoweza kuigundua hali hii. Hata hivyo baadhi ya ishara hujitokeza mtoto anapotimiza miezi 9 hivi na anakuwa hawezi kujieleza kwa tabasamu au milio ya kawaida ya watoto wachanga.  

Morris Barasa ni mzazi na mwanawe aliye na umri wa miaka 13 anasoma katika kituo cha KCCL na anaelezea changamoto anazozipitia. 

Kwani mwanaye alibainika kuwa na usonji akiwa na umri wa miaka miwili,’’Kikubwa ni ile hali yake ya kushindwa kujieleza. Alichelewa sana hata sasa hajajua kujieleza. Tuliona kwamba amechelewa kujieleza na pia katika ile hali ya kucheza na watoto wengine hakuweza kucheza nao kawaida. Wengine wakicheza anafurahia lakini hachezi mwenyewe.” 

Watoto wenye usonji wakijifunza kwa msaada wa teknolojia mpya
Photo from U.Plus Academy
Watoto wenye usonji wakijifunza kwa msaada wa teknolojia mpya

Wanapatiwa mafunzo mbalimbali 

Baadhi ya wanavyojifunza Watoto hawa ni ujuzi wa kupika, kupiga picha, kwenda madukani kununua vitu na cha msingi ni kuweza kumudu mambo kama binadamu mwengine yeyote. 

Walimu wao hutumia mbinu mbalimbali darasani ili mwanafunzi aweze kujua herufi na kuzikumbuka, mwalimu anatumia viashiria au vifaa mbalimbali ambavyo akivitomasa anakumbuka umbo lake. 

Viashiria hivi vinatumiwa kuunda maneno ili mwanafunzi apatae ufahamu na pia kuyaona kwa kuvipangapanga. 

Martha Gathara ni mwalimu wa lugha na hisabati KCCL na anafafanua kuwa,”Natumia vyombo tofauti wakati ambapo nafundisha ndio viweze kusaidia zaidi kwa wanaoelewa kwa kugusa au kutomasa ili wakumbuke.Wakati mwingi wakati wa somo la kiswahili na kiingereza pale natumia (sauti ya karatasi au namba ni kadi maalum zilizo na msasa ambazo huwasaidia watoto kusoma kwa kutumia mfumo huo wa kugusa herufi au nambari.” 

Mafunzo kwa mtoto mwenye usonji.
UNICEF
Mafunzo kwa mtoto mwenye usonji.

Kadi maalum za kujifunzia 

Ili mwanafunzi aweze kujua herufi na kuzikumbuka, mwalimu anatumia viashiria na kadi maalum ambazo akizitomasa anakumbuka umbo lake. 

Kadi hizo zinatumiwa kuunda maneno ili mwanafunzi apatae ufahamu na pia kuyaona kwa kuzipangapanga. 
Mfumo huo unaoana na kauli mbiu ya siku ya Usonji duniani ambayo huadhimishwa tarehe 2 Aprili kila mwaka.  

Siku hii inadhamiria ya kuielimisha jamii kuwa mwanafunzi aliye na usonji ana changamoto za kusoma na kuelewa moja kwa moja. 

Utafiti umebaini kuwa ni rahisi zaidi kumgundua mtoto wa kiume aliye na usonji kuliko wa kike. 
Hali hii inaweza kumfanya mtoto kuwa na matatizo anapokula vyakula fulani kama vile vya ngano, maziwa, njugu karanga na vyengine na kumfanya kuhitaji mlo maalum. 

Mtoto aliye na usonji anakuwa na hali ya kurudiarudia tabia fulani. Hivyo basi ni muhimu kutumia mbinu maalum za mafunzo ili kumuelewesha. 

Teknolojia nayo ina nafasi muhimu katika elimu ya watoto walio na usonji kwani kadri wanavyotazama na kuelekezwa ndivyo wanavyopata kuelewa anasisitiza Dickson Mureithi  mwalimu wa KCCL,” Kama mwalimu unaweza kutumia aina ya video ama unarahisisha masomo kwa kutumia video na picha na vitu mbalimbali vya kutazama na kutumia mikono ili waweze kuelewa zaidi unachokifunza.Tunasoma kwa nusu saa kwa kila somo na katika muda huu kuna shughuli nyingi za kufanya darasani.” 

Usonji na kutangamana 

Usonji huwatatiza wahusika kwenye masuala ya uhusiano katika jamii,kujieleza na hata kupata marafiki maishani. 

Tweet URL

Kutokana na hilo masomo ya kila siku ya kuandika huwakanganya. Hata hivyo ujuzi unaotumia mikono unawasukuma mbele maishani kwani ni werevu. 

Kulingana na Esther Muchai ambaye ni mwalimu mkuu wa shule hii ya Kenya Community Centre for Learning, ni muhimu kwa mtoto aliye na usonji kufundishwa na kupata ujuzi wa kumsaidia maishani,”Tunawapa hawa watoto ujuzi wa kuweza kupika,kupiga picha, kutengeza vitu kwa mikono, kushona na hata kupiga muziki.Kila mwanafunzi anayekuja hapa lazima apate ujuzi na maarifa pamoja na masomo ya kuandika.” 

Siku ya Usonji iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 2007.Baraza Kuu la Umoja wa mataifa lilipitisha azimio hilo pasi na kura kwani ni sehemu ya harakati za Umoja wa Mataifa  za kulinda na kudumisha haki za binadamu.

Matarajio ya wahusika wa karibu ni kuwa na ushirikiano na uwiano kati ya serikali na Umoja wa mataifa kujaribu kutenga shule maalum zilizo na vifaa na mazingira ya kuwahudumia watoto na watu walio na usonji na matatizo mengine ya kusoma duniani. 

Lengo kubwa la Baraza kuu la Umoja wa Mataifa kutenga siku hiyo ni ili kutoa fursa kwa umma kuunga mkono juhudi za kuwasaidia walio na usonji kuishi maisha ya kawaida pamoja na utafiti ili kuwashirikisha karibu zaidi katika jamii. Siku hii ina umuhimu mkubwa kwa Umoja wa Mataifa kwani ni moja kati ya siku saba pekee zinazoyapa uzito masuala ya afya.