Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuwezeshe wenye usonji wastawi katika jamii zao- Guterres

Wanafunzi katika shule ya watoto wenye usonji katika kituo cha jamii cha kujifunza Kenya, KCCL wakiwa kwenye picha iliyopigwa na mwenzao mwenye usonji kama mbinu za kujumuisha watoto kwenye elimu. (Maktaba)
UV Video

Afya

Leo ni siku ya kimataifa ya kuelimishana kuhusu usonji maudhui yakiwa kutoka kuishi kuelekea kwenye ustawi, kwa watu wenye usonji au kwa kiingereza Autism, ambapo kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO, usonji hukumba mtoto mmoja kati ya kila watoto 160 duniani.

Usonji ni tatizo la kibaiolojia analopata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake na dalili huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea na mtoto akiwa na tatizo hilo kasi yake ya kukua kiakili inakuwa ndogo kulingana na kasi ya kukua kimwili.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitangaza kwa kauli moja tarehe 2 Aprili kuwa Siku ya kimataifa ya kuelimisha kuhusu Usonji ili kuangazia hitaji la kusaidia kuboresha hali ya maisha ya wale walio na usonji.
United Nations

Watu wenye usonji wana mchango kwenye jamii

Ni kwa kutambua changamoto hizo zinazokumba watoto wanaozaliwa na usonji, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anasema siku hii ni fursa ya kutambua na kusherehekea michango muhimu ya watu wenye usonji katika kila nchi na kila jamii.

Licha ya uwezo walio nao, Katibu Mkuu anasema watu wenye usonji wanaendelea kukabiliwa na vikwazo wanapotaka kupata haki zao za msingi kama vile elimu, ajira na ujumuishwaji kijamii kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watu wenye Ulemavu, CRPD na Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs. 

Wajibu wa serikali ni upi?

Guterres anasema katika suala la haki za msingi, serikali lazima ziwekeze kwenye mifumo thabiti ya usaidizi, elimu jumuishi na mipango ya mafunzo na teknelojia wezeshi zitakazowezesha watu wenye usonji kufurahia haki kama watu wengine. 

Katibu Mkuu anasema kuongeza kasi ya usaidizi na uwekezaji kwenye jamii kunahitaji ushirikiano na watu wenye usonji na wadau wao. 

“Leo na kila siku, hebu na tuungane kufanikisha haki zao, na kuhakikisha tuna dunia jumuishi na yenye huduma zinazofikiwa na watu wote,” ametamatisha Katibu Mkuu. 

Mvulana aliye na usonji anacheza na vitalu vya kujengea vifaa vya kuchezea.
© Unsplash/Caleb Woods
Mvulana aliye na usonji anacheza na vitalu vya kujengea vifaa vya kuchezea.

Dalili za mtoto mwenye usonji ni zipi?

Kabla ya mtoto kutimiza umri wa miaka mitatu dalili zinazoweza kutanabaisha iwao mtoto ana usonji ni pamoja na mtoto hukosa mbinu za uhusiano, anashindwa kuzungumza na wakati mwingine kurukaruka na hata kujing’ata. 

Watoto hawa kutokana na tatizo hilo wengine hutekelezwa na jamii na kunyimwa haki zao za msingi ikiwemo kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa. 

Tukio makao makuu ya UN

Maadhimisho ya siku hii yatafanyika kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani kwa tukio litakaloleta watu wenye usonji na wadau wao ili kuonesha ni kwa jinsi gani wameweza kukabili na kustawi kwenye jamii zao licha ya kuwa na usonji.