Hali ya kibinadamu ikiwa bado tete Ukraine; Griffiths aanza jukumu aliliopewa na Guterres

29 Machi 2022

Hii leo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejulishwa kuwa Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura ya kibinadamu, OCHA Martin Griffiths tayari ameanza kuwasiliana na pande kinzani kwenye mzozo unaotokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, jukumu alilopatiwa na Umoja wa Mataifa.
 

Naibu Mkuu wa OCHA, Bi. Joyce Msuya ametoa taarifa hizo mbele ya wajumbe wa Baraza la Usalama waliokutana leo Jumanne jijini New York, Marekani kujadili hali ya kibinadamu nchini Ukraine wakati huu ambapo vita imeingia mwezi wa pili.

Bi. Msuya amesema kufuatia tamko la jana la Katibu Mkuu Antonio Guterres, tayari Bwana Griffiths amewasiliana na pande zote mbili ambazo zimekaribisha hatua hiyo na atasafiri kwenda kwenye eneo hilo siku chache zijazo.

Wananchi Ukraine wanashindwa kuzika wafu wao-  Bi. Msuya

Katika hotuba yake Naibu Mkuu huyo wa OCHA amefafanua hali mbaya ya kibinadamu inayokabili wananchi wa Ukraine ikiwemo miji kama vile Mariupol, Kharkiv, Chernihiv na mingine mingi ambayo mwezi moja uliopita ilikuwa imegubikwa na raha lakini sasa hali imebadilika. “Wamegubikwa na mashambulizi. Watu kwenye miji hii hawana chakula, maji, dawa, umeme na vifaa vya kuwapatia joto.”

Amesema katika baadhi maeneo, watu wanashindwa kuzika wafu wao.

Shehena ya vifaa vya matibabu ikiwasili katika hospitali ya wazazi nchini Ukraine
© UNICEF/Andriy Boiko
Shehena ya vifaa vya matibabu ikiwasili katika hospitali ya wazazi nchini Ukraine

Amesisitiza kuwa lazima kupata mbinu za sio tu kusitisha mapigano katika baadhi ya maeneo Ukraine bali pia maeneo yote ili kuokoa maisha, kulinda nyumba za raia zisishambuliwe, shule na hospital izao. “Wananchi wanaishiwa chakula, nishati na matumaini. Lengo letu ni rahisi: Weka silaha chini na okoa maisha.”

Vita imeongeza gharama za operesheni za WFP- Beasley

Akihutubia Baraza hilo kwa njia ya video, Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP David Beasley amesema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeongeza gharama za shirika hilo za kusambaza chakula siyo tu Ukraine bali maeneo mengine duniani kama vile Yemen ambako wanahitaji chakula cha msaada.

“Mwanzoni mwa mwaka 2022, mfumuko wa bei duniani tayari uliongeza bei ya chakula iliyogharimu WFP dola milioni 42 kwa mwezi. Mzozo nchini Ukraine umeibuka, bei za vyakula na mafuta imepanda na kuvuruga mnyororo wa usambazaji bidhaa na hivyo kuongeza dola nyingine milioni 29 za gharama kwa mwezi kwa WFP. Hii leo tunalazimika kulipa takribani dola milioni 71 zaidi kwa mwezi katika operesheni zetu kuliko ilivyokuwa mwaka 2019, ongezeko la asilimia 51.”

Bwana Beasley ametaka sitisho la mapigano ili misaada ifike sambamba na fedha zaidi ili kuwezesha operesheni hizo za kibinadamu ziweze kuendelea 

Mwanaume akiwa amembeba mbwa huku akipita kwenye nyumba iliyoharibiwa kwa mashambulizi huko Mariupol, Kaskazini mwa Ukraine
© UNICEF/Evgeniy Maloletka
Mwanaume akiwa amembeba mbwa huku akipita kwenye nyumba iliyoharibiwa kwa mashambulizi huko Mariupol, Kaskazini mwa Ukraine

Wajumbe watoa maoni yao

Wakichangia hoja zao wawakilishi kutoka nchi mbalimbali wametoa maoni yao ambapo kutoka Ufaransa, Mwakilishi wa taifa hilo Balozi  Nicolas de Rivière, ametaka Urusi iache visingizio vya vikwazo kutoka Ulaya kama sababu ya ongezeko la bei za vyakula duniani.

Marekani kwa upande wake imezungumzia uhaba wa chakula Dunia ikisema inatokana na Urusi kushambulia miundombinu ya kusafirisha nje ya Ukraine shehena za vyakula ikiwemo ngano. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Wendy Sherman amewaeleza wajumbe wa Baraza kuwa “vikwazo dhidi ya Urusi havizuii bidhaa kusafirishwa nje ya nchi bali mashambulizi yanayofanywa na Urusi.

Ili kukabili ongezeko la bei za vyakula duniani, Bi. Sherman amesema “Marekani imeahidi kutoa zaidi ya dola bilioni 11 katika kipindi cha miaka 5 ijayo kukabili ukosefu wa uhakika wa chakula duniani na mahitaji ya lishe duniani kote, ikiwemo nchi ambazo bei za vyakula vimeongezeka kutokana na uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.”

Usaidizi wa kibinadamu usifanyike kwa misingi yoyote ya kibaguzi- Kenya

Mwakilishi wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Martin Kimani amesihi utoaji wa huduma za kibinadamu usifaniyike kwa misingi ya kidini au rangi.

Ametolea mfano ubaguzi wa rangi unaokumba wanafunzi kutoka Afrika waliokwenda kusoma Ukraine wakati huu ambapo wanakimbia machafuko kusaka maeneo salama akisema, “wamegeuka kutoka wanafunzi wenye matumaini kuwa wakimbizi wenye uoga.”

Balozi Kimani amesema ofisi yao ilizungumza na mwanafunzi Korrine Sky raia wa Zimbabwe ambaye alipitia safari ya machungu akikimbia vita Ukraine. “Alitumia siku 4 hadi kuvuka mpaka na mpakani alikumbwa na ubaguzi usio na kipimo. Sasa ameunda taasisi ya kusaidia watu Weusi Ukraine. Tembeleeni wavuti wao.”

"Usaidizi wa kibinadamu usifanyike kwa misingi ya ubaguzi. Wanafunzi wa kiafrika Ukraine wamegeuka kutoka wanafunzi wenye matumaini hadi kuwa wakimbizi wenye hofu." Balozi Martin Kimani- Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya UN

Ukraine yasema bohari zinashambuliwa, Urusi yakana

Ukraine imejulisha Baraza kuwa imakombora ya Urusi yameshambulia mabohari ya vyakula mashariki ya nchi hiyo mbali na eneo la vita. “Leo makombora ya Urusi yameshambulia shamba la nafaka. Je sababu yake ni nini.? Bandari zote zilizoko baharini zimewekewa vizuizi na Urusi. Kuondoa kwa vizuizi hivi kunaweza kusaidia kusafirisha angalau asilimia 60 ya mazao nje ya nchi,” amesema Balozi Sergiy Kyslytsya.

Hata hivyo Urusi ikiwalishwa na Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nebenzia Vassily Alekseevich imesema, “leo tunadaiwa tunashambulia mabohari yenye nafaka na meli za kusafirisha nafaka. Si kweli. Mbona hamsemi kuhusu askari wa Urusi wanaoshikiliwa mateka? Hakuna kitisho chochote kwa raia wa Ukraine wasio na silaha.  Na kuna madai ya magari yenye alama ya kubeba vifaa vya afya yanabeba silaha.” 

Kutoka hofu ya usalama hadi hofu ya njaa

Kwa upande wake India imeendelea kusisitiza kuwa kadri hali ya usalama inavyoendelea kuzorota nchini Ukraie, ni vema kuweka sitisho la mapigano na kuruhusu misaada ifikie maeneo ambayo bado yamezingirwa.

Kwa Albania, Mwakilishi wake wa kudumu kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Ferit Hoxha, wananchi wa Ukraine sasa wameongezewa hovu nyingine kutoka ile ya usalama na sasa kuna ya njaa.

Mwakilishi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Barbara Woodward amemulika suala la ukosefu wa maji akisema watu hawana maji safi na salama,  wanalazimika kunywa siyo tu maji yasiyo salama bali majitaka. Kutakuwepo na uwajibikaji kwa uhalifu huu. Kuna umuhimu wa kuondoa machungu ya kibinadamu. “

Amesema njia pekee ya vita kuisha ni kwa Urusi kusitisha uvamizi wake Ukraine na kukumbusha kuwa “kila mwanachama wa Umoja wa Mataifa anataabika na madhara ya vita hii ya sasa. Na ari ya vita kutoka Urusi inachochea ongezeko la bei ya vyakula duniani kote.”

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter