Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za usaidizi Ukraine zaendelea ,IAEA nayo yaingia kunusuru nyuklia 

Mwanamume akitembea kwenye magovu ya jengo baada ya mlipuko wakati wa mzozo Kyiv, Ukraine.
© UNICEF/Anton Skyba for The Globe and Mail
Mwanamume akitembea kwenye magovu ya jengo baada ya mlipuko wakati wa mzozo Kyiv, Ukraine.

Harakati za usaidizi Ukraine zaendelea ,IAEA nayo yaingia kunusuru nyuklia 

Msaada wa Kibinadamu

Hatimaye mji wa Kharkiv nchini Ukraine ambao umegubikwa na mapigano umefikiwa na misaada ya dhaura ya kibinadamu huku wakazi walio kwenye mji wa Mariupol wanakabiliwa na kile kinachoitwa uamuzi wa kufa au kupona iwapo waondoke mjini humo au la, mwezi mmoja tangu Urusi ivamie taifa hilo la Ulaya ya Kati. 

Msemaji wa ofisi ya  Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura ya kibinadamu, OCHA, Jens Laerke amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi hii leo kuwa misaada ya chakula, vifaa vya matibabu na vya majumbani vilifikia maelfu ya wakazi wa mji huo kaskazini-mashariki mwa Ukraine. 

Misaada hiyo ilifikishwa na msafara ulioongozwa na Mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Ukraine, Osnat Lubrani ikijumuisha misaada kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF kwa ajili ya watu 6,000. 

Kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR misaada kwa kaya 500 kama vile mahema, taa za sola na blanteki huku shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP likisambaza mgao wa wiki mbili wa chakula kwa watu 3,325. Kutoka WHO ilikuwa vifaa vya matibabu kwa wagonjwa 10,000 kwa kipindi cha miezi mitatu. 

Palanca, Maldova katika mpaka na Ukraine, mvulana akipumzika.
© UNICEF/Vincent Tremeau
Palanca, Maldova katika mpaka na Ukraine, mvulana akipumzika.

Mariupol hali bado tete 

Hata hivyo kwa mji wa Mariupol ulioko kusini na kwingineko, ambako bado kumezingirwa na majeshi na kukabiliwa na mashmbulizi yasiyochagua maeneo, hali ni mbaya, imesema Kamati ya Kimataifa ya msalaba mwekundu, ICRC huko Geneva, Uswisi. 

Msemaji wa ICRC Eva Watson amewajulisha wanahabari kuwa “kiwango cha vifo na uharibifu pamoja na machungu ambayo tunashuhudia kwa raia kinachukiza na hakikubaliki.” 

Amesisitiza hofu yao kuhusu raia ambao hawana njia ya kukimbia mapigano na ambao bado wanakumbwa na mashambulizi ya makombora huku wakiwa hawana huduma za maji safi na salama pamoja na huduma nyingine muhimu. 

Kwa mujibu wa OCHA, asilimia 90 ya majengo ya makazi mjini Mariupol, yakiwemo majengo 2,600 ya makazi, yameharibiwa. 

Idadi ya vifo miongoni mwa raia inakaribia 5,000. 

Bi. Watson anasema “raia wanachukua uamuzi wa kufa au kupona wanapotaka kukimbia eneo ambalo halina sitisho la mapigano au makubaliano yoyote yale ya kuwawezesha kuondoka salama. Muda unayoyoma kwa wakazi wa Mariupol na maeneo mengine ya mapigano ambao wamepitisha wiki kadhaa bila msaada wowote wa kibinadamu.” 

IAEA nayo yachukua hatua kuepusha janga la nyuklia 

Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, IAEA, Rafael Mariano Grossi ametimiza ahadi yake ya kufika Ukraine na sasa anashauriana na viongozi waandamizi wa serikali juu ya mpango wa shirika hilo wa kupeleka usaidizi wa kiufundi kuhakikisha usalama kwenye  mitambo ya nyuklia. 

“Msaada huo ni pamoja na kupeleka wataalamu wa IAEA na vifaa vya usalama na ulinzi ikiwemo vifaa vya kufuatilia usalama kwenye mitambo hiyo,” imesema taarifa ya IAEA iliyotolewa Vienna, Austria hii leo. 

“Vita inaweka mitambo ya nyuklia nchini Ukraine na mitambo mingine yenye minururisho katika hatari. Lazima tuchukue hatua ya haraka kuhakikisha mitambo inaweza kuendelea kufanya kazi kwa usalama na kupunguza hatari ya ajali yoyte inayoweza kuwa na madhara kiafya na kimazingira kwa Ukraine na kwingineko,” amesema Bwana Grossi.