Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi 30,000 wa Ukraine warejea nyumbani kila siku 

Familia zikihamishwa kutoka Irpin, Kyiv nchini Ukraine.
© UNICEF/Julia Kochetova
Familia zikihamishwa kutoka Irpin, Kyiv nchini Ukraine.

Wakimbizi 30,000 wa Ukraine warejea nyumbani kila siku 

Wahamiaji na Wakimbizi

Zaidi ya watu 870,000 ambao walikimbia Ukraine kufuatia uvamizi wa Urusi tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu, wamerejea nyumbani, imsema taarifa mpya ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya dharura, OCHA, wakati huu ambapo kuna hofu ya kuzorota kwa upatikanaji wa chakula nchini humo. 

Ikinukuu Ofisi ya Mipaka ya Ukraine, OCHA inasema watu 30,000 wanavuka mpaka kila siku na kurejea Ukraine, na wengi wao ni wanawake, watoto na wazee ikilinganishwa na idadi kubwa ya wanaume kurejea nyumbani vita ilipoanza. 

Changamoto ya kutoa misaada 

 "Takwimu hizo zinadokeza kuwa idadi ya wanaorejea Ukraine inaweza kuendelea kuongezeka na hivyo kuwa ni changamoto kwa utoaji wa huduma za kibinadamu kwa watu wanaohitaij misaada kujumuika tena na jamii zao, au kupata jamii sahihi ya wenyeji ya kuwahifadhi,” imesema OCHA, iwapo hakuna uwezekano kwa watu hao wanaorejea kufika katika makazi yao ya awali. 

Kwa mujibu wa OCHA, kati ya watu milioni 12 wenye uhitaji nchini Ukraine, watoa misaada wameweza kuwafikia watu milioni 2.1 pekee,, na ombi la Umoja wa Mataifa la dola bilioni 1.1 bado halijafadhiliwa ipasavyo. 

Kusini vita bado inapamba moto 

Katika maeneo ya MAshariki na kusini mwa Ukraine mashambulizi yanapamba moto, na kusababisha uharibifu wa miundombinu bila kusahau vifo na majeruhi miongoni mwa raia. 

OCHA imeripoti pia mashambulizi ya kutumia maroketi katika maeneo ya kati na kaskazini mwa Ukraine, na kueleza kuwa eneo la kilometa za mraba 300,000 la Ukraine, sawa na nusu ya eneo zima la taifa hilo litahitahi huduma ya kuteguliwa mabomu ya ardhini. 

Wafanyakazi wa misaada wauawa 

Katika ripoti yake mpya zaidi, OCHA inasema wafanyakazi wawili wa kutoa huduma za kibinadamu na ndugu zao watano wameuawa kwenye jimbo la Mashariki la Dontesk. 

Walikuwa wamesaka hifadhi kwenye ofisi ya Caritas huko Mariupol pindi jengo lao liliporipotiwa kushambuliwa kwa kifaru, tarehe 15 mwezi uliopita wa Machi, ijapokuwa taarifa hizo zimepatikana karibuni kwa kuwa mji huo uliokuwa haufikiki kwa wiki kadhaa. 

Wakati huo huo, shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo duniani, FAO limeonya kuweko kwa ukosefu wa uhakika wa kupata chakula katika maijmbo  10 ya Ukraine, huku asilimia 11 ya majimbo yaliyokumbwa na vita yakitabiriwa kukumbwa na uhaba wa chakula ndani ya miezi miwili ijayo. 

Usaidizi kwenye kilimo 

Jamii za vijijini na zile za pembezeno zimekumbwa zaidi na uhaba wa chakula, imesema FAO na inatangaza kuwa itasaidia wakulima kupanda mazao mashambani, kuokoa mifugo yao na kuzalisha chakula. 

Msaada wa haraka wa fedha umepangwa pia kwa wale walio hatarini zaidi, ikwemo kaya zinazoongozwa na wanawake, wazee na watu wenye ulemavu. 

Waliokimbilia Urusi kutoka Ukraine 

Wakati huo huo, OCHA, imepokea taarifa kuwa Urusi imeripoti kuwa zaidi ya watu 783,000, wakiwemo takribani watoto 150,000 wamevuka mpaka kuingia Urusi wakitokea Ukraine tangu tarehe 24 mwezi Februari mwaka huu, mashambulizi yalipoanza. 

Takwimu za hivi karibuni zaidi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR, zinadokeza kuwa zaidi ya watu milioni 7.4 wamekimbia Ukraine tangu kuanza kwa vita, wengine milioni 7 ni wakimbizi wa ndani ya nchi yao.