Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakulima walioathirika na kimbunga Haiti kupigwa jeki na IFAD

Uharibifu uliosababishwa na kimbunga Matthew Haiti. Picha: UM

Wakulima walioathirika na kimbunga Haiti kupigwa jeki na IFAD

Msaada wa Kibinadamu

Mfuko wa kimataifa wa ufadhili kwa maendeleo ya kilimo IFAD, na serikali ya Haiti leo wametia saini makubaliano ya kifedha ambayo yatasaidia kufufua shughuli za kilimo katika maeneo yaliyoathirika na kimbunga Matthew mwezi Oktoba 2016 nchini Haiti.

Muafaka huo unajumuisha dola milioni 10.8 za uwekezaji wa programu za ubunifu na teknolojia katika masuala ya kilimo na misitu (PITAG)

Kwa ujumla programu hiyo ya PITAG itawekeza dola milioni 76.8 katika kuboresha maisha ya wakulima wadogowadogo nchini Haiti.

Makundi ya wakulima watakaolengwa zaidi na mradi huo ni yasiyojiweza kama vile wanawake na vijana na kaya zaidi ya 65,000 zinatarajiwa kufaidika na mradi huo.

PITAG itahakikisha kunakuwepo teknolojia na mifumo ya kilimo kwa wakulima wadogowadogo ambayo inaendana na mazingira waliyopo. Kwa mfano kilimo mchanganyiko cha miti ya matunda na mbogamboga kitasaidia kupata mavuno mengi na kuweza kuwalisha watu wengi zaidi.