Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu anapaswa kulindwa kwa tahadhari ya mapema dhidi ya majanga:UN 

Mvulana akiwa amesimama mbele ya kisima wakati wa kiangazi nchini Bangladesh.
© WMO/Muhammad Amdad Hossain
Mvulana akiwa amesimama mbele ya kisima wakati wa kiangazi nchini Bangladesh.

Kila mtu anapaswa kulindwa kwa tahadhari ya mapema dhidi ya majanga:UN 

Tabianchi na mazingira

Ikiwa leo ni siku ya utabiri wa hali ya hewa duniani, malengo mapya ya Umoja wa Mataifa yalioyotangazwa leo yanataka katika miaka mitano ijayo kila mtu kote duniani alindwe kwa kupewa tahadhari ya mapema dhidi ya ongezeko la hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi. 

Kupitia ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelitaka shirika la Umoja wa Mataifa la utabiri wa hali ya hewa duniani, WMO kuongoza juhudi na kuwasilisha mpango wa hatua za kufikia lengo hilo kwenye mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Novemba nchini Misri. 

Guterres amesema “Nusu ya ubinadamu wote duniani tayari wko katika hatari. 

Kila ongezeko la joto duniani litaongeza zaidi marudio na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa. Ndiyo maana ni lazima tuweke kikomo cha kupanda kwa joto duniani kisizidi nyuzi joto 1.5.” 

Kuweka hai lengo hilo la kusalia na nyuzijoto 1.5 kunahitaji punguzo la asilimia 45 la uzalishaji wa hewa chafuzi duniani ifikapo mwaka 2030 ili kufikia hali ya kutozalisha kabisa hewa ukaa katikati mwa karne hii. 

Shaka na shuku ya kutimiza lengo 

Hata hivyo Katibu Mkuu amesema  kulingana na ahadi za sasa za kitaifa, uzalishaji wa gesi chafu duniani unatarajiwa kuongezeka kwa karibu asilimia 14 muongo huu. 

“Ulimwengu lazima ukomeshe uraibu wake kwa nishati ya mafuta kisukuku, hasa makaa ya mawe. Wakati huo huo, lazima tuwekeze kwa usawa katika kukabiliana na hali na kujenga mnepo. Hiyo inajumuisha maelezo ambayo huturuhusu kutarajia dhoruba, mawimbi ya joto, mafuriko na ukame.” 

Ameongeza kuwa “Leo hii , thuluthi moja ya watu wa dunia, hasa katika nchi zinazoendelea na visiwa vidogo vinavyoendelea, bado hawajafunikwa na hawajalindwa na mifumo ya tahadhari ya mapema. Barani Afrika, hali ni mbaya zaidi kwani asilimia 60 ya watu wanakosa ulinzi huo. Hili halikubaliki, haswa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi kuwa mbaya zaidi. Tahadhari ya mapema na hatua huokoa maisha.” 

Katibu Mkuu amesema kwa ajili hiyo, ndio maana leo ametangaza kuwa Umoja wa Mataifa utaongoza hatua mpya ya kuhakikisha kila mtu duniani analindwa na mifumo ya tahadhari ya mapema ndani ya miaka mitano ijayo. 

Mtazamo wa radi Istria, Croatia.
WMO/Boris Baran
Mtazamo wa radi Istria, Croatia.

Watu wanapaswa kufanya nini  

Katibu Mkuu wa shirika la utabiri wa hali ya hewa duniani WMO Petteri Taalas kwa upande wake amesema watu zaidi hukabiliwa na hatari nyingi ambazo mara kwa mara huibuka pamoja na kusababisha dhoruba kali.  

Na hivyo amesema “Utabiri wa hali ya hewa pekee utakuwa hautoshi tena badala yake, kinachohitajika ni kutabiri nini hali ya hewa itafanya na, muhimu zaidi, kile ambacho watu wanapaswa kufanya, hii ni muhimu kuokoa maisha na riziki.” 

WMO imeongeza kuwa mtu mmoja kati ya watatu bado hajahudumiwa vya kutosha na mifumo ya tahadhari ya mapema, na, mara nyingi sana, maonyo hayafikii wale wanaoyahitaji zaidi. 

Bwana Taalas amesisitiza kwamba "Tunahitaji uchunguzi mwingi ili kuweza kuendesha huduma hizi za maonyo ya mapema. Tunahitaji uchunguzi wa ndani wa msingi, ambao ni sahihi, unaoelezea hali ya hewa ya ndani. Kisha, tunahitaji sauti za puto ili kupata wasifu wima wa anga. Siku hizi, sisi pia tunatumia ndege. Kampuni nyingi za ndege zina vifaa vya hali ya hewa. Kisha, tuna programu za satelaiti ambazo hutolewa na wanachama wetu wakuu, na pia nchi za Ulaya zimejiunga na ubia. Unahitaji zote hizo kama nguzo ya miundo hii ya utabiri wa hali ya hewa. “ 

Ameongeza kuwa “Ikiwa huna, kwa mfano, uchunguzi wa ndani wa msingi, ubora wa utabiri unabaki kuwa duni. Hiyo ndiyo hali, kwa bahati mbaya, katika baadhi ya maeneo duniani kote, kwa mfano, barani Afrika, Visiwa vya Caribbea na Pasifiki, tumepunguza sana mitandao ya uchunguzi, na hiyo ina athari mbaya kwa usahihi wa utabiri wa hali ya hewa. Ukosefu huu wa uchunguzi una athari za ulimwengu.” 

Wajibu wa pamoja kukabili mabadiliko ya tabianchi 

WMO kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la mazingira UNEP na shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP wameunda utaratibu wa ufadhili unaoitwa SOFF - The Systematic Observations Financing Facility. SOFF itasaidia nchi zinazoendelea, ikilenga Nchi za Visiwa Vidogo zinazoendelea na nchi zilizo na maendeleo duni, ili kuziwezesha kuzalisha na kubadilishana takwimu muhimu za hali ya hewa na mabadiliko ya tabianchi.  

Kwa kuziba  mapengo haya ya takwimu WMO inasema SOFF italeta uboreshaji mkubwa wa utabiri bora wa hali ya hewa, mifumo ya tahadhari ya mapema, na taarifa za hali ya hewa katika wakati muhimu ambapo athari za mabadiliko ya tabianchi yanaongezeka.  

WMO imesisitiza kwamba utekelezaji wa SOFF utafaidi kila mtu na utakuwa na athari za kuokoa maisha katika nchi zilizo hatarini zaidi, ambapo miongo ya maendeleo yanaweza kufutwa na hali mbaya ya hewa au tukio la hali ya hewa.