Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mauaji yanayofanywa na jeshi la Myamnar yanaweza kuwa ya kimbari

Wasichana wadogo katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Myanmar wanachota maji kutoka kwenye kisima.
UNOCHA/Z. Nurmukhambetova
Wasichana wadogo katika kambi ya wakimbizi wa ndani nchini Myanmar wanachota maji kutoka kwenye kisima.

Mauaji yanayofanywa na jeshi la Myamnar yanaweza kuwa ya kimbari

Haki za binadamu

Jumuiya ya kimataifa zimehimizwa kuchukua hatua za pamoja na za haraka ili kukomesha wimbi la ghasia nchini Myanmar kwakile kilichoelezwa kuwa jeshi limejihusisha na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu ambao baadhi yao unaweza kuwa uhalifu.

Kauli hiyo imetolewa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet hii leo jijini Geneva Uswisi wakati ikitolewa ripoti ya 49 ya kikao cha kawaida cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

 Ripoti hiyo imetanabaisha kuwa jeshi na vikosi vya usalama vya Myanmar vimeonesha kutojali kabisa maisha ya binadamu, huku wakishambulia maeneo yenye wakazi wengi kwa mashambulizi ya anga na silaha nzito na kuwalenga kwa makusudi raia, ambao wengi wao wamekuwa wakiuawa.

Wananchi kupigwa risasi kichwani, kuchomwa moto hadi kufa, kukamatwa kiholela, kuteswa au kutumika kama ngao za binadamu ni baadhi ya matukio yaliyoripotiwa kwenye ripoti hiyo.

Mauaji ya watu wengi nayo yameripotiwa kufanyika ambapo mwezi Julai mwaka 2021 katika Mkoa wa Sagaing, askari waliwaua watu 40 katika mfululizo wa mashambulizi, wanakijiji walipata mabaki ya baadhi ya wahanga wakiwa bado wamefungwa mikono na miguu migongoni.

Mwezi Disemba katika Jimbo la Kayah, wanajeshi walichoma moto takriban miili ya watu 40 wakiwemo wanaume, wanawake na watoto. Wanakijiji walieleza kugundua mabaki hayo kwenye malori kadhaa, huku miili ikipatikana katika sehemu zinazoonyesha kuwa walijaribu kutoroka na kuteketezwa wakiwa hai.

Wafungwa nao waliripoti kukabiliwa na mateso na aina zingine za unyanyasaji wakati wa mahojiano ya muda mrefu katika vituo vya kijeshi kote Myanmar.

Ikiwa hayo ni baadhi tuu ya matukio yaliyoainishwa kwenye ripoti Kamishna Bachelet ameseme ”Hatua za maana za jumuiya ya kimataifa zinahitajika haraka kuchukuliwa ili kukomesha watu wengine zaidi kupokonywa haki zao, maisha yao na riziki zao.”

Amehitimisha ripoti yake kwakueleza ukiukwaji wa haki za binadamu ni mpana sana nchini Myanmar pamoja na ukioukwaji wa sheria za kimataifa na watu wa Myanmara wanateseka hivyo jumuiya za kimataifa zinahitajika kutoa mwitikio thabiti na kwa umoja.