Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yaleta nuru kwa watoto na wanawake Yobe na Borno nchini Nigeria

Mtoto akiwekewa alama kwenye kucha yake, alama ya kuonesha amepewa chanjo huko Maiduguri, Borno, Nigeria.
UNICEF/Page
Mtoto akiwekewa alama kwenye kucha yake, alama ya kuonesha amepewa chanjo huko Maiduguri, Borno, Nigeria.

UNICEF yaleta nuru kwa watoto na wanawake Yobe na Borno nchini Nigeria

Afya

Kwa miaka 13 wanawake na watoto kwenye majimbo Yobe na Borno nchini Nigeria wameathirika kiafya kutokana na mashambulizi kwenye eneo la Kaskazini-Mashariki mwa Nigeria, mashambulizi ambayo si tu yanasababisha vifo bali pia yanazuia uwezo wa wanawake na watoto kupata huduma za afya. Sasa Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la kuhudumia watoto, UNICEF limechukua hatua kwa kunyoosha mkono wa usaidizi.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo huko Maiduguri nchini Nigeria inasema wamepatia serikali za majimbo hayo mawili dawa muhimu zenye thamani ya zaidi yad ola 430,000 kwa lengo la kuimarisha huduma kwa wajawazito, afya ya mama na watoto wachanga pamoja uhai wa mtoto kwenye jamii zilizoathiriwa na mapigano hayo.

UNICEF imesema pamoja na fedha hizo, itasaidia pia utekelezaji wa makubaliano ya huduma ya afya ya msingi yaliyotiwa saini kati yake na majimbo hayo makubaliano ambayo utekelezaji wake unahitaji nyongeza ya dola 500,000.
 
Kutokana na mashambulizi kwenye eneo hilo la Nigeria, mwaka 2020 pekee kila siku watoto 170 walikufa kwa sababu ya mashambulizi au kukosa huduma za afya.
 
Robo ya vituo vya afya kaskazini-mashariki mwa Nigeria vimeshambuliwa na kuharibiwa kabisa au havifanyi kazi, ilhali uhaba wa wahudumu wa afya na dawa muhimu umekwamisha harakati za kutoa huduma za afya za msingi kwa wajawazito na watoto wachanga.

Mapigano hayo pia yamechangia katika milipuko ya magonjwa na kufanya hali ya utapiamlo kuwa mbaya zaidi.
 
“Tunaweka msingi wa afya bora kwa watoto waliozaliwa na ambao bado hawajazaliwa,” amesema Phuong T. Nguyen Mkuu wa UNICEF ofisi ya Maiduguri.
 
Amesema kwa hatua hizi walizochukua, wajawazito kwenye majimbo ya Borno na Yobe wataweza kupata huduma za msingi kwenye jamii zao na kupokea huduma za msingi za matibabu karibu na nyumbani kwao.

Dawa ambazo wamepatiwa ni pamoja na za kukinga Malaria, viuavijasumu au Antibiotics pamoja na vifaa na lengo ni kuhakikisha watoto wachanga na wale wenye umri wa chini ya miaka mitano wanapata kinga dhidi ya Malaria, kipindupindu na magonjwa mengine hatari kwa watoto.