Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO na WFP waungana kuepusha utegemezi wa chakula Nigeria

WFP
Wakimbizi wapokea mgao wa chakula kutoka kwa WFP.(Picha:WFP)

FAO na WFP waungana kuepusha utegemezi wa chakula Nigeria

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, likiwemo la chakula na kilimo FAO na mpango wa chakula duniani WFP wamezindua mkakati wa pamoja  wa kusaidia wakazi wa kaskazini-mashariki mwa Nigeria kukabiliana na tatizo la njaa na utegemezi wa chakula cha msaada.

 

Kupitia mradi huo FAO itatoa nafaka na mbolea ili kuzalisha  chakula kinachoweza kutosheleza kwa kipindi cha miezi minane ya msimu wa mvua kwa mwaka huu wa 2018 ilhali WFP itatoa msaada wa chakula wa kuweza kukidhi mahitaji hadi mavuno ya mwezi Septemba.

Mathalani wakulima huko Rann na katika maeneo mengine zaidi ya 30 wanaweza kupanda mahindi, mtama, uwele na njugumawe kufuatia mgao huo wa mbegu.

Katika maeneo mengine wamepokea mbegu za ufuta, karanga, pilipili na matikiti maji kwa ajili ya kujipatia kipato.

Fanna Kachella  mkazi wa Rann, ni mmoja wa wanufaika wa mradi huu, ambapo yeye, mume wake na watoto wao 8 wanasema wapo  tayari kuanza tena kilimo akisema, “kutokuwa na shughuli za kufanya imekuwa changamoto kubwa sana kwetu , kwani tumezoea kulima chakula chetu. Tunategemea kupata mazao kutokana na nafaka hizi mpya”

Myrta Kaulard  ambaye ni mwakilishi wa WFP nchini Nigeria amesema, familia nyingi zilizoko kaskazini mwa Nigeria zimeathirika na migogoro ya kivita iliyodumu kwa ziada ya miaka 9.

Hivyo amesema kuna umuhimu  wa kufanya jitihada ili kurejesha hali ya kujitegemea katika masuala ya chakula kwa jamii hii, na pia kuwasaidia kujenga maisha yao upya.

FAO inasema katika msimu wa mvua ambao huanza kati ya mwezi wa juni hadi septemba watakuwa wamewafikia zaidi ya watu milioni 1 katika ukanda huo katika jitihada za  kutokomeza tatizo la utegemezi wa nafaka kama za mahindi, soya, kunde.

WFP na FAO kwa pamoja wamekuwa wakitoa usaidizi kwa zaidi ya watu laki 6 kaskazini-mashariki mwa Nigeria ikijumuisha  majimbo ya Borno, Adamawa na Yobe